MEI 21, 2021; IJUMAA: JUMA LA 7 LA PASKA

Nyeupe
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Mdo 25:13-21
Siku zile, Agripa mfalme wa Bernike walifika Kaisaria, wakimwamkia Festo. Na walipokuwa wakikaa huko siku nyingi, Festo akamweleza mfalme habari za Paulo, akisema, Yupo hapa mtu mmoja aliyeachwa na Feliki kifungoni; ambaye nilipokuwa Yerusalemu wakuu wa makuhani na wazee wa Wayahudi wakaniarifu habari zake, wakinitaka hukumu juu yake. Nikawajibu kwamba si desturi ya Warumi kumtoa mtu awaye yote, kabla mtu yule aliyeshitakiwa hajaonana na washitaki wake uso kwa uso, na kupewa nafasi ya kujitetea katika mashitaka yake. Basi walipokutanika hapa sikukawia; bali siku ya pili nikaketi katika kiti cha hukumunikaamuru mtu huyo aletwe. Na wale waliomshitaki waliposimama hawakuleta neno lo lote baya, kama nilivyodhani, bali walikuwa na maswali mengine mengine juu yake katika dini yao wenyewe, na katika habari ya mtu mmoja Yesu, aliyekuwa amekwisha kufa, ambaye Paulo alikaza kusema kwamba yu hai. Nami nikaona shaka jinsi ya kutafuta hakika ya habari hii, nikamwuliza kama anataka kwenda Yerusalemu ahukumiwe huko katika mambo haya. Lakini Paulo alipodai kuwekwa ahukumiwe na Kaisari, nikaamuru alindwe hata nitakapompeleka kwa Kaisari.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.103:1-2, 11-12, 19-20

 1. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
  Naam, vyote vilivyo ndani yangu
  Vilihimidi jina lake takatifu.
  Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
  Wala usizisahau fadhili zake zote.
  (K)Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni.
 2. Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi,
  Kadiri ileile rehema zake ni kuu kwa wamchao.
  Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi,
  Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi. (K)
 3. Bwana ameweka kiti chake cha enzi mbinguni,
  Na ufalme wake unavitawala vitu vyote.
  Mhimidini Bwana, enyi malaika zake,
  Ninyi mlio hodari, mtendao neno lake,
  Mkiisikiliza sauti ya neno lake. (K)

INJILI: Yn 21:15-19
Walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je! Simoni wa Yohane, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia, Naam, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha wanakondoo wangu. Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohane wanipenda? Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu. Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohane, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu. Akasema, Amin, amin, nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine atakufunga na kukuchukua usikotaka. Akasema neno hilo kwa kuonesha ni kwa mauti gani atakayomtukuza Mungu. Naye akiisha kusema hayo, akamwambia, Nifuate.

TAFAKARI:
UFUASI KWA VITENDO: Katika Injili ya leo tunamwona Kristo akijihakikishia upendo wa Simoni Petro ambaye awali alimkana mara tatu. Anamwuliza swali kama anampenda mara tatu kama ambavyo alimkana mara tatu. Katika kukiri kwake mara zote hizo kwamba anampenda Kristo, Kristo anampa majukumu ya kuchunga au kulisha kondoo wake. Anamwambia ukweli kwamba alipokuwa kijana alikuwa anajifunga na kwenda anapotaka lakini atapokuwa mtu mzima au mzee basi watu wengine watamfunga na kumchukua asipotaka. Tunaambiwa maneno haya aliambiwa kuonesha ni mauti gani atakayomtukuza Mungu kwayo. Na kweli alimtukuza Mungu kwa kifo cha msalaba ambapo yeye alichagua kusulibiwa kichwa chini miguu juu. Katika somo la kwanza tunaona vilevile namna ambavyo ufuasi wa kweli unaleta mahangaiko. Tunaona namna Paulo alivyobadilishwa kutoka kwa mfalme mmoja kwenda kwa mfalme mwingine katika hukumu. Yote hayo yanafanyika kutokana na ufuasi wake. Ufuasi si lelemama, ufuasi unahitaji uvumilivu ambao unaonesha upendo kwa Kristo kwa vitendo.

Sala: Ee Mungu, tunakuomba utujalie fadhila ya uvumilivu wa kuvumilia magumu yote yanayotokana na ufuasi wetu kwa Kristo.