MEI 10,2021; JUMATATU: JUMA LA 6 LA PASKA

Nyeupe
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Mdo 16:11-15
Tuling’oa nanga kutoka Troa, tukafika Samothrake kwa tanga moja, na siku ya pili tukafika Neapoli; na kutoka hapo tukafika Filipi, mji wa Makedonia, mji ulio mkuu katika jimbo lile, mahali walipohamia Warumi; tukawa katika mji huu, tukikaa siku kadha wa kadha. Hata siku ya Sabato tukatoka nje ya lango, tukaenda kando ya mto, ambapo tukadhani ya kuwa pana mahali pa kusali; tukaketi, tukasema na wanawake waliokutana pale. Mwanamke mmoja, jina lake Lidia, mwenye kuuza rangi ya zambarau, mwenyeji wa Thiatira, mcha Mungu, akatusikiliza, ambaye moyo wake ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo. Hata alipokwisha kubatizwa, yeye na nyumba yake, akatusihi, akisema, kama mmeniona kuwa mwaminifu kwa Bwana, ingieni nyumbani mwangu mkakae. Akatushurutisha.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 149:16, 9

 1. Aleluya.
  Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
  Sifa zake katika kusanyiko la watauwa.
  Israeli na amfurahie Yeye aliyemfanya,
  Wana wa Sayuni na wamshangilie mfalme wao.
  (K)Bwana awaridhia watu wake.
 2. Na walisifu jina lake kwa kucheza,
  Kwa matari na kinubi wamwimbie.
  Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake,
  Huwapamba wenye upole kwa wokovu. (K)
 3. Watauwa na waushangilie utukufu,
  Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao.
  Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao,
  Hiyo ndiyo heshima ya watauwa wote. (K)

INJILI: Yn 15:26-16:4
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia. Nanyi pia mnashuhudia, kwa kuwa tangu mwanzo mmekuwapo pamoja nami. Maneno hayo nimewaambia, msije mkachukizwa. Watawatenga na masinagogi; naam, saa yaja atakapodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada. Na hayo watawatenda kwa sababu hawakumjua Baba wala mimi. Lakini nimewaambia hayo, ili makusudi saa ile itakapokuja myakumbuke ya kuwa mimi naliwaambia.

TAFAKARI:
LIDIA WA ULAYA: Leo katika Injili, Bwana wetu Yesu Kristo anaongea kabla ya kuwaaga wanafunzi wake. Anawadokeza juu ya Roho Mtakatifu, msaidizi ambaye anatuletea kutoka kwa Baba. Anasema huyo Roho Mtakatifu atamshuhudia Kristo na kutujalia uwezo wa kumshuhudia Kristo. Kumbe, sisi wafuasi wake Kristo tutakuwa na jukumu hilo la kumshuhudia Kristo, kazi ambayo mtume Paulo anaifanya vizuri kama tunavyoona katika somo ya kwanza, ambapo anaanza utume wake katika bara la Ulaya. Huko anafanikiwa kupata mfuasi wa kwanza anayejulikana kwa jina la Lidya. Lidya ni mama aliyekuwa anafanya bishara ya kuunza rangi za zabarau. Biashara hii ilimuingizia kipato cha kutosha. Hivyo alikuwa ni mama mwenye uwezo kiuchumi. Huyu anamkaribisha Paulo na wamisionari wengine nyumbani kwake na yeye anaamini neno na anakuwa Mkristo wa kwanza kuongoka katika bara la Ulaya. Katika safari hii ya pili ya kimisionari ya mtume Paulo anaingia Ulaya, na Ulaya sasa inaunganishwa si kwa siasa au uchumi bali kwa imani moja, na kuwekwa chini ya Kristo.

SALA: Tunamwomba Mwenyezi Mungu aendelee kutupatia nguvu ya kuwa mashuhuda wake ulimwenguni kote.