MEI 9,2021; DOMINIKA: DOMINIKA YA 6 YA PASKA

Mwaka B
Nyeupe
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Mdo 10: 25-26, 34 -35, 44-48
Petro alipokuwa akiingia Kornelio akatoka amlaki akamwangukia miguu, akamsujudia. Lakini Petro akamwinua, akasema, Simama, mimi nami ni mwanadamu Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo, bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye. Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno. Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu. Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu, Ni nani awezaye kukataza maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vile vile kama sisi? Akaamuru wabatizwe kwa jina lake Yesu Kristo. Ndipo wakamsihi azidi kukaa siku kadha wa kadha.

WIMBO WA KATIKATI: Zab 98: 1 – 4

 1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
  Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
  Mkono wa kuume wake mwenyewe,
  Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
  (K) Bwana ameufunua wokovu wake, Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
 2. Bwana ameufunua wokovu wake,
  Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
  Amezikumbuka rehema zake,
  Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)
 3. Miisho yote ya dunia imeuona
  Wokovu wa Mungu wetu.
  Mshangilieni Bwana, nchi yote,
  Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)

SOMO 2: 1 Yoh 4: 7-10
Wapenzi, na tupendane; kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu, na kila apendaye amezaliwa na Mungu, naye anamjua Mungu. Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo. Katika hili pendo la Mungu lilionekana kwetu, kwamba Mungu amemtuma Mwanawe pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kwa yeye. Hili ndilo pendo, si kwamba sisi tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa kipatanisho kwa dhambi zetu.

SHANGILIO: Yn 14:23
Aleluya, aleluya,
Yesu alisema: Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake.
Aleluya.

INJILI: Yn 15: 9-17
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu. Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe. Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu. Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni. Haya nawaamuru ninyi, mpate kupendana.

TAFAKARI:
TAMBUA UPENDO WA YESU MAISHANI MWAKO: Tafakari ya neno la Bwana katika Dominika yetu ya leo inasisitiza juu ya upendo. Yesu anatupatia upendo wake kama kielelezo. Yeye hachoki kutupenda na alikubali kuutoa uhai wake kwa ajili yetu. Yeye anatuita rafiki; na anategemea tuwe wa kwanza kumwiga katika upendo na kuupeleka kwa wenzetu. Huu ndio ujumbe mkuu katika Dominika yetu leo.
Injili yetu leo ni sehemu ya wosia alioutoa Yesu kwa wanafunzi wake, saa chache kabla ya mateso na kifo chake. Katika wosia huu, Yesu anakiri mbele ya wafuasi wake kwamba Baba anampenda kwa mapendo ya ajabu. Na mapendo haya anayopokea amewaonesha pia wanafunzi wake na hatua kubwa ya dhihirisho la upendo huu ni kwa kukubali kuutoa uhai wake kwa ajili yao na wote wale watakaomfuata. Hivyo anawataka nao pia waige mfano wake kwa kupendana wao kwa wao. Upendo Yesu anaousisitizia ni ule usiojifikiria mwenyewe; wa kujitoa kwa ajili ya wengine. Wataalamu hutumia jina “agape” kuufafanua upendo huu. Ni upendo usio na ubinafsi wa kujitoa kwa ajili ya wengine na Yesu ndiye kielelezo cha huu upendo kwani alikuwa tayari kujitoa kwa ajili ya wengine. Sifa nyingine ya upendo huu ni kwamba hauna kikomo, hauchoki kupenda. Yesu alipokuwa akielekea Kalvari, hakukomea njiani bali alisafiri hadi Kalvari; alitupenda upeo.
Yesu anawaita wanafunzi wake kwa jina lenye cheo; hawaiti watumwa bali rafiki. Katika Injili ya Dominika iliyopita, aliwaita matawi na yeye akiwa shina (la mzabibu). Anawaita kwa cheo hiki kwa sababu amekwishawafunulia mengi toka kwa Baba; siri nyingi za ufalme wa mbinguni, na atawakabidhi utume ule alioufanya yeye. Hivyo, alitegemea kwa sababu ni rafiki zake-wasimwangushe, wawe tayari kuonesha upendo wa “agape”; wa kupenda bila kuchoka. Yesu anazidi kusisitiza kwamba ni kwa njia hii ya upendo watafanikiwa kuzaa matunda. Matunda yanamaanisha vitu viwili: mosi, yanamaanisha matendo mema yanayomtangaza Kristo na yenye kuwafadhili watu. Pili, matunda yanamaanisha idadi ya wafuasi watakaozaliwa katika ufalme wa mbinguni kutokana na utume wa wafuasi wa Yesu. Yesu anamalizia kwa kusisitizia kwamba upendo utawafanya wabakie katika muunganiko naye na kwa njia hii lolote watakaloomba kwa Baba kwa jina la Yesu watalipokea.
Katika somo pili, mtume Yohane katika barua yake ya kwanza anasisitizia kile kilichosemwa katika Injili. Anasema sisi kama wafuasi wa Kristo, hatuna budi kupendana kwani Mungu ambaye ni Baba yetu sote ni upendo. Na yeye hachoki kutupenda. Tusipoonesha upendo basi hatuwezi kujiita wana wake kwani Mungu ni upendo. Hivyo, Mungu anategemea tupendane sisi kwa sisi. Na kigezo cha kumjua mtu anayemfahamu Mungu ni upendo. Asiyependa hamjui Mungu wala hawezi kusema kwamba anashika amri yoyote ya Mungu kwani Mungu ni upendo.
Sisi ndugu zangu kwa ubatizo wetu, tunakuwa wana wa Mungu na wafuasi wa Kristo. Hivyo ni lazima tupendane kama sehemu ya utambulisho wetu kama wana wa Mungu na wafuasi wa Kristo. Zaidi ni kwamba upendo wetu lazima uwe wa matendo. Lazima tuwe tayari kujitoa kwa ajili ya wenzetu. Upendo siyo lazima utoe fedha lakini kauli yako ya kumtuliza au kumtia mtu moyo tayari ni upendo tosha (Mama Theresa wa Calcuta).
Katika Injili Yesu, ametupatia cheo cha rafiki. Hatumii uhusiano uliopo kati ya mtumwa na bwana wake; mtumwa hana uchungu na mali ya bwana wake lakini rafiki hachoki kuitunza mali ya rafiki yake. Hapa Yesu anatualika tuyaone maisha yetu katika mtazamo mpya, yaani agano kati yetu na yeye ni la kirafiki na hivyo ni lazima tulipende. Katika uhusiano wetu na Kristo, tusiwaige watumwa, tupende amri za Kristo, tupende na mali zake pia, yaani kondoo wake.
Upendo ni kiunganishi kati yetu na Yesu na pia Baba. Tukiwa katika upendo sisi kwa sisi, tunaunganika na Yesu, na hapa lolote tuombalo kwa jina lake hakika tutalipata kwani tutajifunza namna ya kuomba, halafu tutaomba kwa nia njema.
Somo la kwanza ni hotuba ya Paulo mbele ya Korneli. Huyu alikuwa akida wa Kirumi. Ingawa hakuwa Myahudi, alimcha Bwana Mungu wa Israeli na malaika alimwongoza Petro aende nyumbani mwake apate kumhubiria Habari Njema. Alipokuwa katika kunena, ghafla Roho Mtakatifu alimshukia Kornelio na watu wa nyumba yake na kuanza kutangaza matendo makuu ya Mungu. Tukio hili lilimshangaza Petro; alishangaa kuona kwamba Roho Mtakatifu anawashukia watu wa Mataifa (wapagani) kabla hata ya kubatizwa. Hapa Petro alijifunza kwamba Mungu hana ubaguzi bali yuko tayari kumkubali yeyote ajinyenyekezae na kuja kwake. Hili lilimfumbua macho Petro na kumwona Yesu kama Masiha wa wote.

SALA: Ee Bwana, ninakuaomba nijifunze lugha yako ya upendo. Ninakuomba niongee na wote ninaokutana nao na wote wanaonizunguka.