MEI 7,2021; IJUMAA: JUMA LA 5 LA PASKA

Nyeupe
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Mdo 15: 22-31
Siku zile, baada ya mtaguso wa Yerusalemu, ikawapendeza mitume na wazee na Kanisa lote kuwachagua watu miongoni mwao na kuwapeleka Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba; nao ni hawa, Yuda aliyeitwa Barnaba, na Sila, waliokuwa watu wakuu katika ndugu. Wakaandika hivi na kupeleka kwa mikono yao, mitume na ndugu wazee, kwa ndugu zetu walioko Antiokia na Shamu na Kilikia, walio wa mataifa; SalAmu Kwa kuwa tumesikia ya kwamba watu waliotoka kwetu wamewasumbua kwa maneno yao, wakipotosha roho zenu, ambao sisi hatukuwaagiza; sisi tumeona vema, hali tumepatana kwa moyo mmoja, kuwachagua watu na kuwapeleka kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo, watu waliohatarisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Basi tumewatuma Yuda na Sila, watakaowaambia wenyewe maneno yayo hayo kwa vinywa vyao. Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo lazima, yaani, mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo, mtafanya vema. WasalAmu Hata hao wakiisha kupewa ruhusa wakatelemkia Antiokia; na baada ya kuwakusanyia jamii yote wakawapa ile barua. Nao walipokwisha kuisoma, wakafurahi kwa ajili ya faraja ile.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 57 :7-11

 1. Ee Mungu, moyo wangu u thabiti,
  Moyo wangu u thabiti.
  Nitaimba, nitaimba zaburi,
  Amka, utukufu wangu.
  Amka, kinanda na kinubi,
  Nitaamka alfajiri.
  (K) Ee Bwana, nitakushukuru kati ya watu.
 2. Ee Bwana, nitakushukuru kati ya watu,
  Nitakuimbia zaburi kati ya mataifa.
  Maana fadhili zako ni kubwa hata mbinguni,
  Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu,
  Na juu ya nchi yote uwe utukufu wako. (K)

INJILI: Yn 15:12-17
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.
Ninyi mmekuwa rafiki zangu, mkitenda niwaamuruyo. Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.
Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni. Haya nawaamuru ninyi, mpate kupendana.

TAFAKARI:
SISI TUMEITWA RAFIKI: Katika somo la kwanza leo tunaona sasa wajumbe waliotumwa wanapeleka ujumbe wa mtaguso wa Yerusalemu, wakifikisha kwa watu ujumbe ule na jamii ya Wakristo pale Antokia inafurahi mno wanapopata ujumbe. Sasa vikwazo vya kuwa Wakristo vimeondolewa na tunaona Ukristo unawavutia watu wengi bila kujali mila na desturi zao ilmradi wafuate kile Kristo anawaambia katika Injili ya leo. Anatupatia amri yake ya upendo. Anatuwekea kigezo cha kupendana kwa namna yeye alivyotupenda sisi. Zaidi sana, anatuita sisi rafiki na sisi tutaendelea kuwa rafiki tukitenda yale ambayo ametuamuru. Sisi tutende na katika kutenda hatuwi tena watumwa wa kushika mila na desturi. Kwa mfano tutakuwa huru kabisa tukifuata amri ya upendo ambayo kwayo tutakuwa tumeziishi amri zote. Hivyo basi tutakaposhika amri ya upendo, tukipendana tunajenga urafiki na Kristo. Tuendelee kupata rafiki wengi, yaani kuwaalika wengi katika Ukristo, na sisi wenyewe tujaribu kuishi Ukristo ambao kweli ni katika kuishi kwake ndio tunatengeneza urafiki na Kristo na Mungu mwenyewe.

SALA: Ee rafiki yetu Bwana Yesu, ukomaze urafiki wetu kwa kutuwezesha kuishi vema amri ya mapendo.