MEI 6,2021; ALHAMISI: JUMA LA 5 LA PASKA

Nyeupe
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Mdo 15:7-21
Wakati wa mtaguso wa Yerusalemu, baada ya hoja nyingi Petro alisimama, akawaambia, Ndugu zangu, ninyi mnajua ya kuwa tangu siku za kwanza Mungu alichagua miongoni mwenu ya kwamba Mataifa walisikie neno la Injili kwa kinywa changu na kuliamini. Na Mungu, ajuaye mioyo ya watu, akawashuhudia, akiwapa Roho Mtakatifu vile vile kama alivyotupa sisi; wala hakufanya tofauti kati yetu sisi na wao, akiwasafisha mioyo yao kwa imani. Basi sasa mbona mnamjaribu Mungu na kuweka kongwa juu ya shingo za wanafunzi, ambalo baba zetu wala sisi hatukuweza kulichukua. Bali twaamini kwamba tutaokoka kwa neema ya Bwana Yesu vile vile kama wao. Basi mkutano wote wakanyamaza, wakawasikiliza Barnaba na Paulo wakiwapasha habari za ishara na maajabu, ambayo Mungu aliyafanya kwa ujumbe wao katika Mataifa. Na hao walipokwisha kunyamaza Yakobo akajibu, akisema, Ndugu zangu, nisikilizeni. Simeoni ametueleza jinsi Mungu hapo kwanza alivyowaangalia Mataifa ili achague watu katika hao kwa ajili ya jina lake. Na maneno ya manabii yapatana na hayo, kama ilivyoandikwa. Baada ya mambo haya nitarejea, nami nitaijenga tena nyumba ya Daudi iliyoanguka. Nitajenga tena maanguko yake, nami nitaisimamisha; ili wanadamu waliosalia wamtafute Bwana, na mataifa yote ambao jina langu limetajwa kwao; asema Bwana, ajulishaye hayo tangu milele. Kwa sababu hiyo mimi naamua hivi; tusiwataabishe wale waliomgeukia Mungu katika mataifa; bali tuwaandikie kwamba wajiepushe na unajisi wa sanamu, na uasherati, na nyama zilizosongolewa, na damu Kwa maana tangu zamani za kale Musa anao watu wahubirio mambo yake; katika kila mji husomwa kila Sabato katika masinagogi.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 96:1-3, 10

 1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
  Mwimbieni Bwana nchi yote.
  Mwimbieni Bwana, libarikini jina lake.
  (K) Wahubirini mataifa habari za utukufu wake.
 2. Tangazeni wokovu wake siku kwa siku.
  Wahubirini mataifa habari za utukufu wake,
  Na watu wote habari za maajabu yake. (K)
 3. Semeni katika mataifa, Bwana ametamalaki;
  Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike,
  Atawahukumu watu kwa adili. (K)

INJILI: Yn 15:9-11
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu. Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake. Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe.

TAFAKARI:
TUKAE KATIKA PENDO LA KRISTO: Katika somo la kwanza tunaona yale yaliyojiri katika mtaguso huko Yerusalemu, na namna ambavyo mtaguso ule ulilenga kusaidia watu kuwa karibu na Kristo na wala haukuwa na lengo la kuwawekea watu kongwa shingoni. Tunaweza kusema kuwa dini ya Kikristo msingi wake mkubwa ni upendo. Upendo ndiyo amri kuu kuliko zote. Tunaona ukweli kabisa kuwa upendo unabeba na kufunika sheria zote. Hivyo mtaguso wa Yerusalemu uliishia kwa kutoa maelekezo yaliyokuwa na lengo la kuendelea kudumisha upendo na si kuleta utengano kati ya wanajumuiya. Katika Injili ya leo tunamsikia Kristo mwenyewe akisema mtu akimpenda atazishika amri zake naye atakaa katika pendo lake. Ndiyo kusema kwamba tunahitaji kumpenda Kristo na tunapompenda ndio basi tutazishika amri zake na tutakuwa tayari kushika yale ambayo anatuagiza. Hivyo basi katika kufanya hivyo tutakuwa tumeepukana na zile mila na desturi nyingine ambazo pengine zimewekwa na watu na zinazoweza kutuzuia sisi kuukaribia upendo wa Kristo.

SALA: Ee Bwana, tunakuomba utujalie kukaa katika pendo lako kwa kuzishika amri zako na hivyo tuweze kudumu katika kukufuata.