Nyeupe
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Mdo 15:1-6
Siku zile, walishuka watu waliotoka Uyahudi wakawafundisha wale ndugu ya kwamba, msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamwezi kuokoka. Basi baada ya Paulo na Barnaba kushindana na watu hawa na kuhojiana nao sana, ndugu wakaamuru kwamba Paulo na Barnaba na wengine miongoni mwao wapande kwenda Yerusalemu kwa mitume na wazee kwa habari ya swali hilo. Basi, wakisafirishwa na Kanisa, wakapita kati ya nchi ya Foinike na Samaria, wakitangaza habari za kuongoka kwao mataifa; wakawafurahisha ndugu sana. Walipofika Yerusalemu wakakaribishwa na Kanisa na mitume na wazee, nao wakawaeleza mambo yote Mungu aliyoyafanya pamoja nao. Lakini baadhi ya madhehebu ya Mafarisayo walioamini wakasimama wakisema, Ni lazima kuwatahiri na kuwaagiza kuishika torati ya Musa. Mitume na wazee wakakusanyika wapate kulifikiri neno hilo.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 122:1-5
- Nalifurahi waliponiambia
Na twende nyumbani kwa Bwana.
Miguu yetu imesimama
Ndani ya malango yako, ee Yerusalemu.
(K)Nalifurahi waliponiambia,
Na twende nyumbani kwa Bwana. - Ee Yerusalemu uliyejengwa
Kama mji ule ulioshikamana,
Huko ndiko walikopanda kabila,
Kabila za Bwana. (K) - Ushuhuda kwa Israeli,
Walishukuru jina la Bwana.
Maana huko viliwekwa viti vya hukumu,
Viti vya enzi vya mbari ya Daudi. (K)
INJILI: Yn 15:1-8
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa. Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia. Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu.
Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi; akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote. Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea.
Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.
TAFAKARI:
MKULIMA, MTI NA TAWI: Mazingira ya kilimo ni kati ya mazingira yanayoweza kueleweka na watu wengi kwani ni uti wa mgongo wa uchumi wa mataifa mengi. Sote twafahamu walau kwa kiasi fulani shughuli za kilimo. Twafahamu namna mmea unavyojitegemea katika ukuaji na ustawi wake ukijumlisha mizizi, shina na matawi yake. Kristo katika Injili anazungumzia muungano uliopo kati ya mti na tawi. Ili tawi liwe na uhai ni lazima liwe limejishikanisha na mti. Huo mti nao humtegemea sana mkulima katika ustawi wake. Sisi ni matawi ya mti ndiye Kristo. Ili kuwa na uhai twahitaji sana kujiunga na mti ili tujipatie mahitaji yetu. Kristo ndiye uhai wetu. Wote wanahitaji kujiunga naye ili kupata uzima. Ndiyo maana katika kumhubiri Kristo mitume walienda kwa watu wote, Wayahudi kwa watu wa Mataifa. Wote tunahitaji wokovu. Kama mitume, nasi tufurahie kuona watu wengi zaidi wakimtambua na kumfuata Kristo. Tusiweke vizingiti kwa wale wanaomfuata Kristo. Tuwasaidie watu kuungana na mti wa uzima. Tuwe manabii wa uhai.
SALA: Ee Kristo, mti wa uzima, unijalie niwe nabii wa uhai niwavutie wengi kwako wewe uliye uzima wetu.