MEI 3,2021; JUMATATU: JUMA LA 5 LA PASKA

WAT. FILIPO NA YAKOBO, MITUME
Sikukuu
Nyekundu
Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO I: 1 Kor 15:1-8
Ndugu zangu, nawaarifu ile Injili niliyowahubiri; ambayo ndiyo mliyoipokea, na katika hiyo mnasimama, na kwa hiyo mnaokolewa; ikiwa mnayashika sana maneno niliyowahubiri; isipokuwa mliamini bure. Kwa maana naliwatolea ninyi hapo mwanzo yale niliyoyapokea mimi mwenyewe, ya kuwa Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alizikwa; na ya kuwa alifufuka siku ya tatu, kama yanenavyo maandiko; na ya kuwa alimtokea Kefa; tena na wale Thenashara; baadaye aliwatokea ndugu zaidi ya mia tano pamoja; katika hao wengi wanaishi hata sasa, ila baadhi yao wamelala; baadaye akamtokea Yakobo; tena na mitume wote; na mwisho wa watu wote, alinitokea mimi, kama ni mtu aliyezaliwa si kwa wakati wake.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 19:1-4

 1. Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu,
  Na anga laitangaza kazi ya mikono yake.
  Mchana husemezana na mchana,
  Usiku hutolea usiku maarifa.
  (K) Sauti yao imeenea duniani mwote.
 2. Hakuna lugha wala maneno,
  Sauti yao haisikilikani.
  Sauti yao imeenea duniani mwote,
  Na maneno yao hata miisho ya ulimwengu.
  Katika hizo ameliwekea jua hema. (K)

INJILI: Yn 14:6-14
Yesu alimwambia Tomaso: Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi. Kama mngalinijua mimi, mngalimjua na Baba, tangu sasa mnamjua, tena mmemwona. Filipo akamwambia, Bwana, utuoneshe Baba, yatutosha. Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuoneshe Baba? Husadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu? Hayo maneno niwaambiayo mimi siyasemi kwa shauri langu; lakini Baba akaaye ndani yangu huzifanya kazi zake. Mnisadiki ya kwamba mimi ni ndani ya Baba, na Baba yu ndani yangu; la! hamsadiki hivyo, sadikini kwa sababu ya kazi zenyewe. Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba. Nanyi mkiomba lolote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.

TAFAKARI:
AMWONAYE KRISTO AMEMUONA BABA: Yakobo anayekumbukwa leo ni Yakobo Mdogo, ambaye ni ndugu wa Bwana wetu Yesu Kristo. Filipo ni mmoja kati ya mitume ambaye alikuwa karibu kabisa na watu wa mataifa na hivyo kupitia Filipo watu wengi waliweza kujongea kwa Kristo. Filipo alimwomba Kristo awaoneshe Baba, lakini Yesu anamwambia tukimwona yeye yatosha, ni sawa na kumwona Baba. Kuna muunganiko kati ya Kristo na Mungu Baba katika ule umoja wa Utatu Mtakatifu, na hivyo watatu hawa wanafanya kazi kwa pamoja. Kazi ambazo Kristo anazifanya na kazi ambazo Baba anamwagiza ndiyo kazi hizo hizo Roho anafanya katika nguvu ambayo ipo ndani ya Kristo, na hivyo Utatu Mtakatifu upo pamoja daima katika utendaji wa kazi. Hivyo tusidhani kuwa Kristo yupo yeye pekee anapofanya utume wake, hapana, nafsi zote za Mungu zipo katika utendaji wa kazi. Kile kinachofanyika kinamdhihirisha Mungu Baba na Roho Mtakatifu. Hivyo basi hawa wameungana na Kristo. Kristo kwa umwilisho amekuja ili kuvipatanisha vitu vyote katika muungano. Kama vile Utatu walivyo umoja, nasi tunaitwa katika umoja.

SALA: Ee Mungu Mwenyezi, tuweze kufikia umoja ule ambao Kristo aliuleta, tusiwe sababu ya kuleta utengano katika kujenga mwili wa fumbo wa Kristo.

2021 MEI 4 JUMANNE: JUMA LA 5 LA PASKA
Nyeupe
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Mdo14:19-28
Wayahudi walifika toka Antiokia na Ikonio, wakawashawishi makutano hata wakampiga kwa mawe Paulo, wakamburuta nje ya mji, wakidhani ya kuwa amekwisha kufa. Lakini wanafunzi walipokuwa wakimzunguka pande zote, akasimama, akaingia ndani ya mji; na siku ya pili yake akatoka, akaenda zake pamoja na Barnaba mpaka Derbe. Hata walipokwisha kuhubiri Injili katika mji ule, na kupata wanafunzi wengi, wakarejea mpaka Listra na Ikonio na Antiokia, wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile imani, na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi. Na walipokwisha kuwachagulia wazee katika kila Kanisa, na kuomba pamoja na kufunga, wakawaweka katika mikono ya Bwana waliyemwamini. Wakapita kati ya Pisidia wakaingia Pamfilia. Na baada ya kuhubiri lile neno katika Perge wakatelemka mpaka Atalia. Na kutoka huko wakahubiri kwenda Antiokia. Huko ndiko walipoombewa neema ya Mungu kwa ile kazi waliyokwisha kuitimiza. Hata walipofika wakalikutanisha Kanisa, wakawaeleza mambo yote aliyoyafanya Mungu pamoja nao, na ya kwamba amewafungulia mataifa mlango wa imani. Wakaketi huko wakati usiokuwa mchache, pamoja na wanafunzi.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 145:10-13, 21

 1. Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru,
  Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
  Wataunena utukufu wa ufalme wako,
  Na kuuhadithia uweza wako,
  Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu,
  Na utukufu wa fahari ya ufalme wake.
  (K) Watawajulisha watu matendo yake makuu,
  Na utukufu wa fahari wa zamani zote.
 2. Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
  Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote. (K)
 3. Kinywa changu kitazinena sifa za Bwana;
  Wote wenye mwili na walihimidi jina lake takatifu
  milele na milele. (K)

INJILI: Yn 14:27-31
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga. Mlisikia ya kwamba mimi naliwaambia, Naenda zangu, tena naja kwenu. Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba; kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi. Na sasa nimewaambia kabla halijatokea, kusudi litakapotokea mpate kuamini. Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu. Lakini ulimwengu ujue ya kuwa nampenda Baba; na kama vile Baba alivyoniamuru; ndivyo nifanyavyo. Ondokeni, twendeni zetu.

TAFAKARI:
WAZEE WA KANISA: Kanisa kamwe halijawahi kubaki na ukiwa. Katika Injili twamsikia Bwana wetu Yesu Kristo akiongelea habari za kuondoka kwake. Anasema kwamba anaenda kwa Baba. Ila anatusihi tusiwe na woga. Tena anatuahidia msaidizi mwingine wa kuliongoza Kanisa hapa duniani. Ahadi hiyo ilitimia. Katika somo la kwanza tunamuona Mtume Paulo pamoja na wamisionari wenzake wakimaliza safari ya kwanza ya kimisionari. Wanapokuwa wakirudi wanayatembelea yale makanisa waliyoyaanzisha katika safari hiyo. Katika kila Kanisa wanawachagua wazee na kuwaweka kuwa waangalizi wa makanisa hayo. Wazee hawa hawachaguliwi kienyeji tu bali kwa umakini mkubwa, kwa kusali na kufunga. Wazee hawa ndiyo tunawasikia katika waraka wa Yakobo akisema mtu wa kwenu hawezi, basi apelekwe kwa wazee ambao watasali na kuwapaka mafuta na hivyo kuwarudishia afya na kupata msamaha wa dhambi. Hawa si wengine ni mapadre. Tuwapende, tushirikiane na mapadre ili kuendelea kuujenga ufalme wa Mungu kuanzia hapa ulimwenguni.

SALA: Ee Mungu Baba Mwenyezi, tunakushukuru kwa zawadi ya watenda kazi katika Kanisa lako. Kwa namna ya pekee tunawaombea mapadre wote moyo wa kujitoa kwa ajili ya kuchunga vyema kundi lako.