MEI 2,2021; DOMINIKA: DOMINIKA YA 5 YA PASKA

Mwaka B
Nyeupe
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Mdo 9: 26-31
Sauli alipofika Yerusalemu, alijaribu kujiunga na wanafunzi, nao walikuwa wakimwogopa wote, wasisadiki ya kuwa yeye ni mwanafunzi. Lakini Barnaba akamtwaa, akampeleka kwa mitume akawaeleza jinsi alivyomwona Bwana njiani, na ya kwamba alisema naye, na jinsi alivyohubiri kwa ushujaa katika Dameski kwa jina lake Yesu. Naye akawa pamoja nao katika Yerusalemu akiingia na kutoka. Akahubiri kwa jina la Bwana kwa ushujaa, akinena na kuhojiana na Wayahudi wa Kiyunani. Nao wakajaribu kumwua. Lakini ndugu walipopata habari wakamchukua mpaka Kaisaria, wakampeleka aende Tarso. Basi Kanisa likapata raha katika Uyahudi wote na Galilaya na Samaria, likajengwa, likiendelea na kuongezeka katika kicho cha Bwana, na faraja ya Roho Mtakatifu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab 22: 25- 27, 29-31

  1. Nitaziondoa nadhiri zangu
    Mbele yao wamchao.
    Wapole watakula na kushiba,
    Wamtafutao Bwana watamsifu;
    Mioyo yenu na iishi milele.
    (K) Kwako, Bwana, zinatoka sifa zangu katika kusanyiko kubwa.
  2. Miisho yote ya dunia itakumbuka
    Na watu watamrejea Bwana;
    Jamaa zote za mataifa watamsujudia.
    Wakwasi wote wa dunia watakula na kusujudu,
    Humwinamia wote washukao mavumbini. (K)
  3. Naam, yeye asiyeweza kujihuisha nafsi yake,
    Wazao wake watamtumikia.
    Zitasimuliwa habari za Bwana,
    Kwa kizazi kitakachokuja,
    Nao watawahubiri watakaozaliwa haki yake,
    Ya kwamba ndiye aliyefanya. (K)

SOMO 2: 1 Yoh. 3: 18-24
Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli. Katika hili tutafahamu ya kwamba tu wa kweli, nasi tutaituliza mioyo yetu mbele zake, ikiwa mioyo yetu inatuhukumu; kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu naye anajua yote. Wapenzi, mioyo yetu isipotuhukumu, tuna ujasiri kwa Mungu; na lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake. Na hii ndiyo amri yake, kwamba tuliamini jina la Mwana wake Yesu Kristo, na kupendana sisi kwa sisi, kama alivyotupa amri. Naye azishikaye amri zake hukaa ndani yake yeye, naye ndani yake. Na katika hili tunajua ya kuwa anakaa ndani yetu, kwa huyo Roho aliyetupa.

SHANGILIO: Yn 15:4-5
Aleluya, aleluya,
Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu, akaaye ndani yangu, huyo huzaa sana.
Aleluya.

INJILI: Yn 15:1- 8
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Mimi ndimi mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima. Kila tawi ndani yangu lisilozaa huliondoa; na kila tawi lizaalo hulisafisha, ili lizidi kuzaa. Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya lile neno nililowaambia. Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu. Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi; akaaye ndani yangu nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamuwezi kufanya neno lo lote. Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea. Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. Hivyo hutukuzwa Baba yangu, kwa vile mzaavyo sana; nanyi mtakuwa wanafunzi wangu.

TAFAKARI:
KUUNGANIKA NA YESU: Ujumbe wa neno la Bwana katika Dominika ya leo unaongozwa na Injili yetu inayotusisitizia sisi kama matawi tubakie katika muungano na Yesu (anayefananishwa na mzabibu) ili tuweze kuzaa matunda. Katika somo la pili, mtume Yohane anatuambia kwamba matunda yetu lazima yadhihirike si kwa maneno tu bali kwa matendo yetu mema kwa kuzishika amri za Mungu. Katika somo la kwanza, tunapewa mfano wa Barnaba ambaye kwa matendo yake mema aliweza kumfanya Paulo akubalike kwa Wakristo wa mwanzo na kumruhusu aanze kutumia karama zake kwa ajili ya faida ya Wakristo wote. Kumbe, sisi nasi tunaalikwa kubakia katika muungano na Yesu na kuishi imani yetu kwa matendo kama alivyofanya Barnaba. Huu ndio ujumbe mkuu wa neno la Bwana leo.
Injili ya leo ni sehemu ya wosia uliotolewa na Yesu kabla ya mateso na kifo chake. Katika Injili hii, Yesu anaeleza muunganiko uliopo kati yake na wafuasi wake kwa kutumia mfano wa mzabibu na matawi. Yesu anajifananisha na mzabibu na wafuasi wake kama matawi. Matawi hutegemea kila kitu toka kwa shina ili yaweze kuishi na kuzaa matunda. Yesu anasema kwamba yale matawi yakizaa matunda bora, Mungu hupata sifa. Siku ile tulipobatizwa, sisi tulipata kuwa matawi katika mzabibu (ambao ni Yesu). Matawi hupata kila kitu toka kwa shina ili yaweze kuzaa, ndivyo hivyo na sisi tunavyopaswa kuwa. Lazima tutambue kwamba sakramenti tupokeazo toka kwa Yesu na ibada zote tuzifanyazo ni kama utomvu unaotoka katika shina, yaani Yesu ili kutuwezesha sisi matawi kuishi. Tukikosa utomvu huu, hakika tutanyauka na kushindwa kuzaa chochote. Yesu anatuonya kwamba ipo mizabibu mingine (kama ya ubinafsi, uasherati, kiburi, uchu wa mali) inayotaka sisi kama matawi tujiunganishe nayo lakini tukifanya hivyo tutanyauka kwani tutashindwa kupata virutubisho kwa ajili ya kuyatunza maisha yetu.
Katika Injili ya leo, tunagundua kwamba Yesu anatumia picha ya mzabibu kuelezea taifa la Mungu na katika taifa la Israeli, picha ya mzabibu ilikuwa ikitumiwa kuwakilisha taifa la Israeli (Isaya 5:1-7, Jer 2:21, Eze 15, Ps 80:9-16). Hapa, Yesu anasema kwamba yeye na wafuasi wake ndilo taifa jipya la Mungu. Hivyo, yale yaliyotabiriwa katika Agano la Kale kuhusu huyu mzabibu sasa yametimia kwani sisi ni matawi ya mzabibu kwa ubatizo wetu; sisi kama matawi tuliunganishwa na mzabibu, Yesu Kristo. Hivyo, anazidi kutuambia tubakie siku zote katika muungano naye. Yesu ndiye anayefungua mlango wa neema kati ya mwanadamu na Mungu na ndiyo maana bila muunganiko naye, hatutafika popote. Na ndiyo maana Yesu anasema mtu wa namna hii aliyekatika muunganiko naye, ataomba chochote na kupata kwani sala yake itakuwa katika muungano na Mungu.
Katika somo la pili, mtume Yohane anaendelea kufanya maelezo ya kile alichokisema katika Injili. Anawaambia Wakristo wamwamini Yesu na kuwapenda binadamu wenzao. Upendo wetu kwa Mungu udhihirike kwa matendo yetu mema. Hii ndiyo namna tuwezayo kusema kwamba sisi ni watoto wa Mungu. Na anaendelea kusema kwamba pale ujisikiapo dhamiri yako ikisuta mwenendo wako wa maisha, basi isikilize; usiende kinyume nayo. Wakati mwingi tunakosa amani maishani mwetu na kutenda mabaya kwa sababu ya kukataa kuzitii dhamiri zetu.
Somo la kwanza linatupatia mfano wa Barnaba na baadaye Paulo ambao waliishi imani yao kwa matendo na kuwezesha uzaaji wa matunda. Barnaba anaonesha imani yake kwa matendo kwa kumtetea Paulo na kumtambulisha kwa Kanisa la Yerusalemu pale lilipoonesha kumkataa Paulo. Huyu Paulo aliyeletwa na Barnaba alilisaidia sana Kanisa na umisionari wake uliwaleta wengi kwa Kristo.
Sisi yafaa tujiulize, je, mimi kama Mkristo, nimekwishazaa tunda lolote? Labda Yesu akija kwangu leo, ni tunda gani nitajaribu kumpatia na kumwambia hili ndilo nililozaa? Aidha, kila mmoja leo anaalikwa kuwa Barnaba mpya. Ushuhuda ni jambo muhimu sana. Mfano mbaya wa kimaisha humwangusha mwenzako. Mfano mzuri huwainua wenzako kiimani. Mfano mbaya wa kiimani ni hatari sana tena kwa nyakati zetu hizi ambapo katika vyombo vyetu vya habari, matendo maovu ya watu na dhambi za watu hupewa nafasi zaidi kuliko matendo yao mema. Ukitenda jambo baya linasambaa zaidi kuliko jema. Kumbe, matamanio yetu yawe ni kuwaona wenzetu wakimjia na kumwabudu Mungu.

SALA: Bwana kama vile matawi yanavyojiunga na shina, ninakuomba mimi nijiunge nawe, Ee Bwana.