MEI 1,2021; JUMAMOSI: JUMA LA 4 LA MWAKA

MT. YOSEFU MFANYAKAZI
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO I: Mwa 1:26-2:3
Mungu alisema, Na tufanye mtu kwa mfano wetu; kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi. Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi. Mungu akasema, tazama, nimewapa kila mche utoao mbegu, uliojuu ya uso wa nchi yote pia, na kila mti ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu; na chakula cha kila mnyama wa nchi, na cha kila ndege wa angani, na cha kila kitu kitambaacho juu ya nchi, chenye uhai; majani yote ya miche ndiyo chakula chenu; ikawa hivyo. Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita. Basi mbingu na nchi zikamalizika, na jeshi lake lote. Na siku ya saba Mungu alimaliza kazi yake yote aliyoifanya; akastarehe siku ya saba, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoifanya. Mungu akaibarikia siku ya saba, akaitakasa kwa sababu katika siku hiyo Mungu alistarehe, akaacha kufanya kazi yake yote aliyoiumba na kuifanya.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 90:2- 4, 12-14, 16

 1. Kabla haijazaliwa milima, wala hujaiumba dunia,
  Na tangu milele hata milele ndiwe Mungu.
  (K) Kazi ya mikono yetu uithibitishe, Ee Bwana.
 2. Wamrudisha mtu mavumbini,
  Usemapo, Rudini, enyi wanadamu.
  Maana miaka elfu machoni pako
  Ni kama siku ya jana ikiisha kupita,
  Na kama kesha la usiku. (K)
 3. Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu,
  Tujipatie moyo wa hekima.
  Ee Bwana, urudi, hata lini?
  Uwahurumie watumishi wako. (K)
 4. Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako,
  Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote.
  Matendo yako na yaonekane kwa watumishi wako.
  Na adhama yako kwa watoto wako. (K)

INJILI: Mt 13:54-58
Yesu alipofika nchi yake, akawafundisha makutano katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii? Huyu si mwana wa seremala? mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, naYusufu, na Simoni, na Yuda? Na maumbu yake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote? Wakachukizwa naye. Yesu akawaambia, Nabii hakosi kupata heshima, isipokuwa katika nchi yake, na nyumbani mwake mwenyewe. Wala hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu ya kutokuamini kwao.

TAFAKARI:
ASIYEFANYA KAZI NA ASILE: Leo ni sikukuu ya wafanyakazi ulimwenguni. Kwa kutambua umuhimu wa kufanya kazi Kanisa likamuweka Mtakatifu Yosefu kuwa msimamizi wa wafanyakazi wote ulimwenguni. Hivyo Kanisa linathamini na kuipenda kazi. Katika somo la kwanza tunasoma simulizi la kuumbwa kwa ulimwengu. Kumbe Mungu mwenyewe alifanya kazi ya kuumba. Katika Injili tunamsikia Kristo akitambulika kuwa mwana wa seremala, ndiye Yosefu. Kumbe Yosefu anatambulika kwa kazi aliyokuwa anaifanya, hivyo Yosefu naye alifanya kazi. Mtoto wa nyoka ni nyoka. Kama Kristo ni mwana wa seremala basi ni wazi kuwa katika utoto wake alishirikishwa kazi hiyo kama urithi pekee ambayo baba yake angeweza kumrithisha kwa urahisi. Hivyo, Kristo naye alifanya kazi. Mitume wa Yesu wengi wao walikuwa wavuvi, hivyo walifanya kazi. Mtume Paulo naye kwa taaluma alikuwa mtengeneza mahema. Kumbe, yeye naye alifanya kazi na akasisitiza watu wafanye kazi akisema, “Asiyefanya kazi na asile.”

SALA: Ee Mungu Baba Mwenyezi, leo, kwa maombezi ya Mtakatifu Yosefu, seremala, tunawaombea wafanyakazi wote ulimwenguni ili waipende na kuithamini kazi.