Mt. Petro Shanel, Padre na Shahidi
Nyeupe
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: Mdo 12:24, 13:5
Siku zile, neno la Bwana likazidi na kuenea. Na Barnaba na Sauli, walipokwisha kutimiza huduma yao, wakarejea kutoka Yerusalemu, wakamchukua pamoja nao Yohane aitwaye Marko. Na huko Antiokia katika Kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli. Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia. Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao. Basi watu hao, wakiisha kupelekwa na Roho Mtakatifu wakatelemkia Seleukia, na kutoka huko wakasafiri baharini hata Kipro. Na walipokuwa katika Salami wakalihubiri neno la Mungu katika masinagogi ya Mayahudi.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 67:1-2, 4, 5, 7
- Mungu na atufadhili na kutubariki,
Na kutuangazia uso wake.
Njia yake ijulike duniani,
Wokovu wake katikati ya mataifa yote.
(K) Watu na wakushukuru, Ee Mungu,
Watu wote na wakushukuru. - Mataifa na washangilie,
Naam, waimbe kwa furaha,
Maana kwa haki utawahukumu watu,
Na kuwaongoza mataifa walioko duniani. (K) - Watu na wakushukuru, Ee Mungu,
Watu wote na wakushukuru.
Mungu atatubariki sisi;
Miisho yote ya dunia itamcha Yeye. (K)
INJILI: Yn 12:44-50
Siku ile Yesu alipaza sauti, Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi bali yeye aliyenipeleka. Naye anitazamaye mimi amtazama yeye aliyenipeleka. Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani. Na mtu akiyasikia maneno yangu, asiyashike, mimi simhukumu; maana sikuja ili niuhukumu ulimwengu, ila niuokoe ulimwengu. Yeye anikataaye mimi, asiyeyakubali maneno yangu, anaye amhukumuye; neno hilo nililolinena ndilo litakalomhukumu siku ya mwisho. Kwa sababu mimi sikunena kwa nafsi yangu tu; bali Baba aliyenipeleka, yeye mwenyewe ameniagiza nitakayonena na nitakayosema. Nami najua ya kuwa agizo lake ni uzima wa milele; basi hayo ninenayo mimi, kama Baba alivyoniambia, ndivyo ninenavyo.
TAFAKARI:
KUWAHESHIMU WAJUMBE WANAOTUMWA KWETU KUNALETA UELEWANO: Katika utaratibu wa kiserikali, tunao wakuu wa mkoa au wilaya na hawa kwa mujibu wa taratibu husika, wanamwakilisha rais wa nchi husika. Wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao, wanatenda kwa kadiri rais anavyowaelekeza au anachowatarajia wao kutenda ili mradi lengo husika la maendeleo na ustawi wa wananchi na nchi kwa ujumla vinakuwa ndivyo vya kipaumbele. Ikitokea umekiuka kutofuata utaratibu wao, inachukuliwa ni dharau kwa rais. Kristo naye leo hii anatuambia wazi kuwa yeye ni mwakilishi wa Mungu Baba. Kuna usemi wa wahenga usemao, “Mjumbe hauawi” ndani ya usemi huu kuna maana kwamba, huwezi kumhukumu mjumbe kutokana na analokuambia kwani siyo lake, yeye katumwa tu na wala siyo wa kuhojiwa sana kwani maelezo mengine yako kwa aliyemtuma. Kuna siku niliona gari limeandikwa kwa nyuma “Paka siyo mchawi, katumwa tu” niliweza kupata ujumbe kuwa hapa paka ni mjumbe tu, mhusika halisi ni yule anayemtumia paka huyo katika mazingira yanayoelezwa kuwa ya ovyo.
SALA: Baba wa mbinguni, tunaomba neema ya utii hasa kwa Mwanao uliyemtuma kwetu.
2021 APRILI 29 ALHAMISI: JUMA LA 4 LA PASKA
Mt. Katarina wa Siena, Bikira na Mwalimu wa Kanisa
Kumbukumbu
Nyeupe
Zaburi: Juma 3
SOMO 1: Mdo 13: 13-25
Paulo na wenziwe wakang’oa nanga wakasafiri kutoka Pafo, wakafika Perge katika Pamfilia. Yohane akawaacha akarejea Yerusalemu. Lakini wao wakatoka Perge, wakapita kati ya nchi, wakafika Antiokia, mji wa Pisidia, wakaingia katika sinagogi siku ya Sabato, wakaketi. Kisha, baada ya kusomwa torati na chuo cha manabii, wakuu wa sinagogi wakatuma mtu kwao, na kuwaambia, Ndugu, kama mkiwa na neno la kuwafaa watu hawa lisemeni. Paulo akasimama, akawapungia mkono, akasema, enyi waume wa Israeli, nanyi mnaomcha mungu, sikilizeni. Mungu wa watu hawa Israeli aliwachagua baba zetu, akawatukuza watu hao, walipokuwa wakikaa kama wageni katika nchi ya Misri, na kwa mkono ulioinuliwa akawatoa, akawaongoza. Na kwa muda wa miaka kama arobaini akawavumilia katika jangwa. Na alipokwisha kuwaharibu mataifa saba katika nchi ya Kanaani akawapa nchi yao iwe urithi kwa muda wa miaka kama mia nne na hamsini; baada ya hayo akawapa waamuzi hata zamani za nabii Samweli. Hatimaye wakaomba kupewa mfalme; Mungu akawapa Sauli mwana wa Kishi, mtu wa kabila ya Benyamini, kwa muda wa miaka arobaini. Na alipokwisha kumwondoa huyo, akamwinua Daudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia, akisema, Nimemwona Daudi, mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayefanya mapenzi yangu yote. Katika uzao wake mtu huyo Mungu amewaletea Israeli Mwokozi, yaani, Yesu, kama alivyoahidi; Yohane alipokuwa amekwisha kuwahubiri watu wote wa Israeli habari za ubatizo wa toba, kabla ya kuja kwake. Naye Yohane alipokuwa akimaliza mwendo wake alinena, Mwanidhani mimi kuwa nani? Mimi siye. Lakini , angalieni, anakuja mmoja nyuma yangu ambaye mimi sistahili kumlegezea viatu vya miguu yake.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 89:1-2, 20-21, 26-27
- Kwa kinywa changu
Nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.
Maana nimesema, Fadhili zitajengwa milele;
Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako.
(K) Fadhili zako, ee Bwana, nitaziimba milele. - Nimemwona Daudi, mtumishi wangu,
Nimempaka mafuta yangu matakatifu.
Ambaye mkono wangu utakuwa thabiti kwake,
Na mkono wangu utamtia nguvu. (K) - Yeye ataniita, Wewe baba yangu,
Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu.
Nami nitamjalia kuwa mzaliwa wangu wa kwanza,
Kuwa juu sana kuliko wafalme wa dunia. (K)
INJILI: Yn 13:16-20
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Amin, amin, nawaambia ninyi, Mtumwa si mkuu kuliko bwana wake; wala mtume si mkuu kuliko yeye aliyempeleka. Mkiyajua hayo, heri ninyi mkiyatenda. Sisemi habari za ninyi nyote; nawajua wale niliowachagua; lakini andiko lipate kutimizwa, aliyekula chakula changu ameniinulia kisigino chake. Tangu sasa nawaambia kabla hayajatukia, ili yatakapotukia mpate kuamini ya kuwa mimi ndiye. Amin, amin, nawaambieni, Yeye ampokeaye mtu ye yote nimpelekaye, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi ampokea yeye aliyenipeleka.
TAFAKARI:
NI JAMBO JEMA KUWA MTU WA SHUKRANI: “Aliyekula chakula changu ameniinulia kisigino chake.” Maneno kama haya yanaonesha ndani yake kutokuwa na shukrani baada ya kutendewa mema. Hata maneno yaliyotangulia, “Mtumwa si mkuu kuliko bwana wake; wala mtumwa si mkuu kuliko yeye aliyempeleka” Hapa tujifunze kuwa wapole, kutojikweza, kutokutamba na kuwa na dharau. Tujifunze kushukuru kwa kuelewa au kuelekezwa jambo lenye manufaa. Ndiyo maana, kwa wale wanaofanya ukatili badala ya kushukuru vizuri, wahenga husema, “Shukrani ya punda ni mateke.” Tunashuhudia ulimwenguni humu siku hizi, kwa mfano, kijana anasaidiwa na wazazi au walezi wake kimasomo hadi anapata kazi lakini baada ya hapo anawatelekeza wazazi au walezi wake wala hawajali, anakuwa mtu wa kuponda maisha tu na marafiki zake wakati wazazi au walezi wake wana hali ngumu. Huko ni kukosa shukrani, ni kujisahau na kujiona mkuu kuliko aliyekulea na kukusaidia hadi ukafikia hatua uliyo nayo.
SALA: Bwana tujalie tuwe watii na kuwa watu wa shukrani.