APRILI 27,2021; JUMANNE: JUMA LA 4 LA PASKA

Nyeupe
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Mdo 11:19-26
Siku zile, wale waliotawanyika kwa sababu ya ile dhiki iliyotukia kwa habari ya Stefano, wakasafiri hata Foinike na Kipro na Antiokia, wasilihubiri lile neno ila kwa Wayahudi peke yao. Lakini baadhi ya hao walikuwa watu wa Kipro na Kirene, nao walipofika Antiokia wakasema na Wayahudi wa Kiyunani, wakihubiri Habari Njema za Bwana Yesu. Mkono wa Bwana ukawa pamoja nao; watu wengi wakaamini, wakamwelekea Bwana. Habari hizo za watu hao zikafika masikioni mwa Kanisa lililokuwako katika Yerusalemu; wakamtuma Barnaba, aende hata Antiokia. Naye, alipokwisha kufika na kuiona neema ya Mungu akafurahi, akawasihi wote waambatane na Bwana kwa kusudi la moyo. Maana alikuwa mtu mwema amejaa Roho Mtakatifu na imani; watu wengi wakaongezeka upande wa Bwana. Kisha akatoka akaenda Tarso kumtafuta Sauli; hata alipokwisha kumwona akamleta Antiokia. Ikawa kwa muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na Kanisa na kuwafundisha watu wengi. Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 87:1-7

 1. Msingi wake upo
  Juu ya milima mitakatifu.
  Bwana ayapenda malango ya Sayuni
  Kuliko maskani zote za Yakobo.
  Umetajwa kwa mambo matukufu,
  Ee Mji wa Mungu.
  (K) Enyi mataifa yote, msifuni Bwana.
 2. Nitataja Rahabu na Babeli
  Miongoni mwao wanaonijua.
  Tazama Filisti, na Tiro, na Kushi;
  Huyu alizaliwa humo.
  Naam, mintarafu Sayuni itasemwa,
  Huyu na huyu walizaliwa humo. (K)
 3. Na Yeye Aliye juu
  Ataufanya imara.
  Bwana atahesabu, awaandikiapo mataifa,
  Huyu alizaliwa humo.
  Waimbao na wachezao na waseme,
  Visima vyangu vyote vimo mwako. (K)

INJILI: Yn 10: 22-30
Huko Yerusalemu ilikuwa Sikukuu ya Kutabaruku; ni wakati wa baridi. Naye Yesu alikuwa akitembea hekaluni, katika ukumbi wa Sulemani. Basi Wayahudi walimzunguka, wakamwambia, Hata lini utatuhangaisha nafsi zetu? Kama wewe ndiwe Kristo, utuambie waziwazi. Yesu akawajibu, Naliwaambia, lakini ninyi hamsadiki. Kazi hizi ninazozifanya kwa jina la Baba yangu ndizo zinazonishuhudia. Lakini ninyi hamsadiki, kwa sababu hammo miongoni mwa kondoo wangu. Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. Baba yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba yangu. Mimi na Baba tu umoja.

TAFAKARI:
NI JAMBO JEMA KUWA MSIKIVU KATIKA MAISHA: Kristo anaonekana kutokueleweka kwa ile jamii aliyokuwa nayo, amejaribu kwa namna mbalimbali lakini hamna mafanikio, ametenda miujiza na ishara mbalimbali kama kufufua wafu, kuponya wagonjwa, kuwalisha wenye njaa na mengineyo lakini bado wengine hawamwamini ndiyo maana swali hili linajitokeza leo, “Hata lini utatuhangaisha nafsi zetu?” Hapa kuna shida ya kukosa usikivu na hii wakati mwingine inachangiwa na ugumu wa mioyo ya wahusika. Unakuta mtu anakuwa na msimamo wake hataki kubadilika, anaona anachofahamu yeye ndicho sahihi tu na si vinginevyo. Unakuta mtu katika maisha yake anashauriwa na watu wengi tu, lakini anakuwa mkaidi, hataki kukubali ushauri. Lakini wahenga walisema, “Asiyesikia la mkuu, huvunjika guu.” Tuombe tujaliwe neema ya kuwa wasikivu na hasa pale tunapoelekezwa jambo lenye kutujenga au lenye manufaa.

SALA: Tunakuomba, Baba, utujalie neema ili tuweze kuwa na usikivu hasa wa ndani ambao ndio wenye kukutafakari wewe zaidi.