APRILI 25,2021; DOMINIKA: DOMINIKA YA 4 YA PASKA

Mwaka B
Nyeupe
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Mdo 4:8-12
Ndipo Petro, akijaa Roho Mtakatifu, aliwaambia, Enyi wakubwa wa watu na wazee wa Israeli, kama tukiulizwa leo habari ya jambo jema alilofanyiwa yule mtu dhaifu, jinsi alivyoponywa, jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.

WIMBO WA KATIKATI: Zab 117: 1,8-9, 21-23, 26, 28,29.

 1. Aleluya.
  Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni Mwema,
  Kwa maana fadhili zake ni za milele.
  Ni heri kumkimbilia Bwana
  Kuliko kuwatumainia wanadamu
  Ni heri kumkimbilia Bwana
  Kuliko kuwatumainia wakuu.
  (K) Jiwe walilokataa waashi, Limekuwa jiwe kuu pembeni.
 2. Nitakushukuru kwa maana umenijibu,
  Nawe umekuwa wokovu wangu.
  Jiwe walilolikataa waashi
  Limekuwa jiwe kuu la pembeni.
  Neno hili limetoka kwa Bwana,
  Nalo ni ajabu machoni petu. (K)
 3. Na abarikiwe yeye ajaye kwa jina la Bwana;
  Tumewabarikia toka nyumbani mwa Bwana.
  Ndiwe Mungu wangu, nami nitakushukuru,
  Ndiwe Mungu wangu, nami nitakutukuza.
  Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema,
  Kwa maana fadhili zake ni za milele. (K)

SOMO 2: 1 Yoh. 3:1-2
Tazameni, ni pendo la namna gani alilotupa Baba, kwamba tuitwe wana wa Mungu; na ndivyo tulivyo. Kwa sababu hii ulimwengu haututambui, kwa kuwa haukumtambua yeye. Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo.

SHANGILIO: Yn 10:14
Aleluya, aleluya,
Mimi ndimi mchungaji mwema;
nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi.
Aleluya.

INJILI: Yn 10: 11-18
Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mimi ndimi mchungaji mwema, Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwamwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwamwitu huwakamata na kuwatawanya. Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wala mambo ya kondoo si kitu kwake. Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi; kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya Kondoo. Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja. Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena. Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena. Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu.

TAFAKARI:
MCHUNGAJI MWEMA! Tazama ni upendo wa namna gani alionao Baba kwetu kwamba sisi tuitwe wana wake na kweli ndivyo tulivyo (somo la 2). Kila mmoja anapaswa kutafakari juu ya maneno haya. Yohane anaongea kuhusu wewe na mimi! Katika Dominika ya leo, Yesu anatupatia ujumbe wa matumaini kwamba yeye ndiye mchungaji mwema. Anajitofautisha na mtu wa mshahara; yeye hajawa mchungaji kwa kutafuta maslahi binafsi bali amesukumwa na upendo. Huu ndio ujumbe mkuu wa Dominika yetu ya leo. Yesu anatutegemea tushiriki naye katika kazi hii ya uchungaji. Tuwe tayari kushirikiana naye.
Zaburi yetu ya wimbo wa katikati inatoka katika Zaburi ya 117. Hii ni zaburi itumikayo katika shangilio la vijilia ya Pasaka. Zaburi hii huimbwa baada ya somo la waraka na hutumika kushangilia kwamba hakika Kristo amefufuka. Zaburi hii ni ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa fadhili alizoutendea ulimwengu. Pia ina maneno yasemayo, “Jiwe walilolikataa waashi limekuwa jiwe kuu la msingi.” Maneno haya hupeleka ujumbe kwa baadhi ya viongozi wa Kiyahudi hasa wale waliopinga mamlaka ya Yesu. Sasa amefufuka na hakika anakabidhiwa mamlaka yote. Kwetu sisi Yesu ndiye jiwe kuu la pembeni. Tumsadiki ili tuweze kufurahia neema zipatikanazo katika ufufuko wake. Tumfanye kuwa mchungaji wetu.
Katika Injili yetu, Yesu anasisitiza kwamba yeye ndiye mchungaji mwema na anatoa sababu za kwa nini yeye ni mchungaji mwema. Kwanza, anasema kwamba yeye anautoa uhai wake kwa ajili ya kondoo. Hii ni kweli. Yesu ndiye Mwana Kondoo aliyeutoa uhai wake kuwatetea kondoo wake. Anasisitiza kwamba yeye si kama mtu wa mshahara; lengo lake ni kuwaokoa kondoo wasipate kuangamia. Yeye yupo tayari kupambana na mbwamwitu wakali, hawezi kukubali kondoo wateswe na mbwamwitu. Yesu ndiye aliyepambana na viongozi potofu wa Kiyahudi na baadhi ya Mafarisayo waliotetea mafundisho potofu (Lk 11:37-54). Pia Yesu anajitangaza kwamba yeye anawajua kondoo wake wote; anajua shida zao na mahangaiko yao yote. Na hata wale kondoo ambao siyo wake anataka nao waingie katika kundi lake. Hakika Yesu ni mwenye mapendo makubwa. Yupo tayari kuutoa uhai wake kwa ajili ya Kondoo.
Yesu aliwaachia mitume wake wosia wa kuwa wachungaji wema. Katika somo la kwanza, Petro na Yohane wanajidhihirisha kuwa wachungaji wema. Wanakuwa tayari kumponya kiwete bila kudai fedha au sifa binafsi. Hakika wanafunzi wa Yesu walimuiga Yesu katika kazi ya uchungaji. Mbele ya Baraza la Wazee wa Kiyahudi (Sanhedrin) wanakiri uwezo wa Yesu katika kuponya. Waliwataka wazee wa baraza la kiyahudi wageuke ili na wao wawe wachungaji wema. Waache kuwaumiza na kuwadhulumu kondoo na kuthamini sifa binafsi. Petro anawaambia kwamba Yesu ndiye jiwe kuu lililodharauliwa na wao waashi.
Ndugu zangu, tukichunguza masomo haya, tunajifunza yafuatayo: fundisho la mchungaji mwema linatoa changamoto kubwa sana kwetu. Wengi wetu hatujafaulu bado kuwa wachungaji wema. Yesu alikuwa tayari kutoa uhai kwa ajili ya kondoo, mitume walikuwa tayari kufa kwa ajili ya wao kuwa wachungaji wema. Wengi kati yetu bado hatujafaulu kuwa wachungaji wema. Kwa mfano, baadhi ya wazazi wakipatwa na shida kidogo, hutelekeza familia zao, wapo wanandoa waliotalakiana baada ya kupata changamoto katika ndoa kama magonjwa na umaskini. Hakika bado hatujafaulu kuwa tayari kutoa uhai wetu kwa ajili ya wapendwa wetu na wenzetu. Tuzidi kumwomba Mwenyezi Mungu atuongoze.
Fundisho la pili tunalolipata lawahusu wale waliokabidhiwa madaraka na rasilimali katika jamii. Tunabarikiwa na Mwenyezi Mungu ili tukawe wachungaji wema. Wengi wetu tunatapanya rasilimali tunazopewa, tupo tayari hata kutumia elimu na vipaji vyetu kuidhulumu jamii. Hatupaswi kutenda hivi. Tunapewa vipaji na madaraka ili tuisadie jamii na siyo kuwatesa wenzetu. Pia pale tunapotumia rasilimali zetu kuwasaidia wenzetu, hatupaswi kuwanyanyasa. Tunapaswa tutoe kwa moyo usiodai chochote cha ziada toka kwa yule tunayemsaidia. Tuepuke kutumia fedha au rasilimali zetu kuwadhalilisha wenzetu.
Maneno ya zaburi yetu ya wimbo wa mwanzo leo yamesema, “Nchi imejaa fadhili za Bwana.” Hakika Bwana ameijaza nchi fadhili zake. Tutumie fadhili za Bwana zipatikanazo katika ulimwengu kuwasaidia wenzetu. Tuepuke uchoyo; uchoyo ni adui wa jamii na ni chanzo cha umaskini na mateso kwa wenzetu. Tumia nafasi yako kuwa mchungaji. Tuwe tayari kuwahudumia hata wale wasioweza kutupatia kitu.
Tuwaombee pia wenzetu waliokuwa tayari kujitolea kuwa wachungaji wema kwa ajili yetu. Wapo maraisi, maaskofu na viongozi mbalimbali waliokuwa tayari hata kutoa uhai wao ili watupatie uhuru. Tuwakumbuke hao leo.

SALA: Ee Bwana, dumisha ndani ya jumuiya zetu majitoleo ya kutoa katekesi na kuitika wito wa kujiweka wakfu kwako. Wajalie hekima inayohitajika katika maamuzi ya kufuata wito wako ili waweze kung’ara katika huduma zako.