APRILI 24,2021; JUMAMOSI: JUMA LA 3 LA PASKA

Mt. Fideli wa Sigmaringen, Padre na Shahidi
Nyeupe
Zaburi: Juma 1

SOMO I: Mdo 9:31-42
Kanisa lilipata raha katika Uyahudi wote na Galilaya na Samaria, likajengwa, likiendelea na kuongezeka katika kicho cha Bwana, na faraja ya Roho Mtakatifu. Hata Petro alipokuwa akizunguka-zunguka pande zote akawatelemkia na watakatifu waliokaa Lida. Akamwona mtu mmoja huko, jina lake Ainea, mtu huyo amelala kitandani miaka minane; maana alikuwa amepooza. Petro akamwambia, Ainea, Yesu Kristo akuponya; ondoka, ujitandikie. Mara akaondoka. Na watu waliokaa Lida na Sharani wakamwona, wakamgeukia Bwana. Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa. Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani. Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Usikawie kuja kwetu. Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu orofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao. Petro akawatoa nje wote, akapiga magoti, akaomba, kisha akaelekea yule maiti, akanena, Tabitha, ondoka. Naye akafumbua macho yake na alipomwona Petro akajiinua, akaketi. Akampa mkono, akamwinua, hata akiisha kuwaita wale watakatifu na wajane akamweka mbele yao, hali yu hai. Ikajulikana katika mji mzima wa Yafa; watu wengi wakamwamini Bwana.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 116:12-17

  1. Nimrudishie Bwana nini
    Kwa ukarimu wake wote alionitendea?
    Nitakipokea kikombe cha wokovu;
    Na kulitangaza jina la Bwana.
    (K)Nimrudishie Bwana nini
    kwa ukarimu wake wote alionitendea?
  2. Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana,
    Naam, mbele ya watu wake wote.
    Ina thamani machoni pa Bwana
    Mauti ya wacha Mungu wake. (K)
  3. Ee Bwana, hakika mimi ni mtumishi wako,
    Mtumishi wako, mwana na mjakazi wako,
    Umenifungua vifungo vyangu.
    Nitakutolea dhabihu ya kushukuru;
    Na kulitangaza jina la Bwana. (K)

INJILI: Yn 6:60-69
Siku ile, watu wengi miongoni mwa wanafunzi wake waliposikia maneno ya Yesu juu ya mkate wa uzima, walisema: Neno hili ni gumu, ni nani awezaye kulisikia? Naye Yesu akafahamu nafsini mwake ya kuwa wanafunzi wake wanalinung’unikia neno hilo, akawaambia, Je, neno hili linawakwaza? Itakuwaje basi, mmwonapo Mwana wa Adamu akipaa huko alikokuwako kwanza? Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.
Lakini kuna wengine miongoni mwenu wasioamini. Kwa maana Yesu alijua tangu mwanzo ni nani wasioamini, naye ni nani atakayemsaliti. Akasema, Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu. Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena.
Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.

TAFAKARI:
HATUPASWI KUKATA TAMAA KATIKA MASWALA YA IMANI: Kuna usemi usemao “Bata ukimchunguza sana hutamla.” Jamii ilifikia kusema usemi huu kutokana na tabia ya bata, ni mnyama anayeonekana kuwa mchafu na kupenda kukaa katika mazingira ya uchafu, lakini nyama yake ikishaandaliwa ni safi na nzuri. Kwa nini nimegusia usemi huu! Katika maswala ya imani, kuna mambo ambayo haitasaidia kama tutaingia kwenye kuyachunguza sana tukitarajia kupata jibu la uhakika kwa upeo wetu wa kibinadamu. Ni afadhali kuomba tu neema ya kuyakubali na kuona matokeo yake. Ndiyo maana mitume walipoanza kujiuliza maswali mengi kuhusu alichosema Yesu, ilikuwa sawa na kutaka kuchunguza inakuwaje. Na Yesu anawauliza “Mmekwazika?” Wapendwa, inatakiwa tufike mahali tukubali kuwa Mungu yupo na anatenda, haina haja ya kujiuliza sana, hata Petro aliweza kumponya Ainea na kumfufua Dorkasi kwa vile alisimama imara katika kuamini, hakubaki katika kuendelea kujiuliza kama inawezekana au la.

SALA: Yesu mwema, tunaomba utuongezee imani katika maisha yetu.