APRILI 21, 2021; JUMATANO: JUMA LA 3 LA PASKA

Mt. Anselmo, Askofu na Mwalimu wa Kanisa
Nyeupe
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Mdo 8:1-8
Siku ile kulitukia adha kuu ya Kanisa lililokuwa katika Yerusalemu; wote wakatawanyika katika nchi ya Uyahudi na Samaria, isipokuwa hao mitume. Watu watauwa wakamzika Stefano, wakamfanyia maombolezo makuu. Sauli akaliharibu Kanisa, akiingia kila nyumba, na kuwaburuta wanaume na wanawake na kuwatupa gerezani. Lakini wale waliotawanyika wakaenda huko na huko wakilihubiri neno. Filipo akatelemka akaingia mji wa Samaria, akawahubiri Kristo. Na makutano kwa nia moja wakasikiliza maneno yale yaliyosemwa na Filipo walipoyasikia na kuziona ishara alizokuwa akizifanya. Kwa maana pepo wachafu wakawatoka wengi waliopagawa nao, wakilia kwa sauti kuu; na watu wengi waliopooza, na viwete, wakaponywa. Ikawa furaha kubwa katika mji ule.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 66:1-7

  1. Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote,
    Imbeni utukufu wa jina lake,
    Tukuzeni sifa zake.
    Mwambieni Mungu, Matendo yako yatisha kama nini!
    (K) Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote.
  2. Nchi yote itakusujudia na kukuimbia,
    Naam, italiimbia jina lako.
    Njoni yatazameni matendo ya Mungu;
    Hutisha kwa mambo awatendeayo wnadamu. (K)
  3. Aligeuza bahari kuwa nchi kavu;
    Katika mto walivuka kwa migoo;
    Huko ndiko tulikomfurahia.
    Atawala kwa uweza wake milele;
    Macho yake yawaangalia mataifa;
    Waasio wasijitukuze nafsi zao. (K)

INJILI: Yn 6:35-40
Yesu aliwaambia: Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe. Lakini naliwaambia ya kwamba mmeniona wala hamwamini. Wote anipao Baba watakuja kwangu; wala ye yote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe. Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka. Na mapenzi yake aliyenipeleka ni haya, ya kwamba katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho. Kwa kuwa mapenzi yake Baba yangu ni haya, ya kwamba kila amtazamaye Mwana na kumwamini yeye, awe na uzima wa milele; nami nitamfufua siku ya mwisho.

TAFAKARI:
ULINZI WA UHAKIKA UKO KWA YESU: “Wala yeyote ajaye kwangu sitamtupa nje kamwe” Jamii ya mwanzo ni wazi haikuwa inaishi maisha tunayoishi sasa: mageti kila kona, uzio wa tofali, “mifumo ya alamu” na kadhalika. Yesu anatuambia leo twende kwake ndiko kwenye usalama halisi na wa kweli. Tutahangaika na mengi lakini ni bora tusimsahau Yesu. Lengo lake kuu ni kuwa tusipotee milele. Ndiyo maana anasema, “Katika wote alionipa nisimpoteze hata mmoja, bali nimfufue siku ya mwisho.” Kufufuliwa kwetu kutategemea sana imani yetu kwa Kristo. Tunapomzika Mkristo mwenzetu pale mwishoni kuna sala isemayo, “Wewe ni uvumbi, utarudia kuwa uvumbi, lakini Bwana atakufufua siku ya mwisho.” Sala hii tunaisali tukimkabidhi mwenzetu huyo aliyetutangulia kwa Muumba tukimuombea ufufuko kwa uzima wa milele, asipotee bali abaki salama katika Bwana.

SALA: Twakuomba, Ee Yesu, utujalie tufikie kifo tukiwa na imani kwako na tufike salama kwako mbinguni.