APRILI 20, 2021; JUMANNE: JUMA LA 3 LA PASKA

Nyeupe
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Mdo 7:51 – 8:1
Stefano aliwaambia wakuu wa Makuhani: Enyi wenye shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote Mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo. Ni yupi katika manabii ambaye baba zenu hawakumwudhi? Nao waliwaua wale waliotabiri habari za kuja kwake yule Mwenye Haki; ambaye ninyi sasa mmekuwa wasaliti wake, mkamwua; ninyi mliyoipokea torati agizo la malaika msiishike. Basi waliposikia maneno haya, wakachomwa mioyo, wakamsagia meno. Lakini yeye akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu. Akasema, Tazama, naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu. Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja, wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli. Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu. Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa kuuawa kwake.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 31:2-3, 5, 7, 16, 20

 1. Uwe kwangu mwamba wa nguvu,
  Nyumba yenye maboma yakuniokoa.
  Ndiwe genge langu na ngome yangu:
  Kwa ajili ya jina lako uniongoze,unichunge.
  (K) Mikononi mwako naiweka roho yangu, ee Bwana.
 2. Mikononi mwako naiweka roho yangu:
  Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli.
  Bali mimi namtumaini Bwana.
  Na nishangilie, nizifurahie fadhili zako. (K)
 3. Umwangaze mtumishi wako
  Kwa nuru ya uso wako;
  Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako.
  Utawaficha katika hema
  Na mashindano ya ndimi. (K)

INJILI: Yn 6:30-35
Siku ile, Wayahudi walimwambia Yesu: Unafanya ishara gani basi, ili tuione tukakuamini? Unatenda kazi gani? Baba zetu waliila mana jangwani, kama vile ilivyoandikwa, Aliwapa chakula cha mbinguni ili wale.
Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambieni, Siye Musa aliyewapa chakula kile cha mbinguni, bali Baba yangu anawapa ninyi chakula cha kweli kitokacho mbinguni. Kwa maana chakula cha Mungu ni kile kishukacho kutoka mbinguni na kuupa ulimwengu uzima.
Basi wakamwambia, Bwana, siku zote utupe chakula hiki. Yesu akawaambia, Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe.

TAFAKARI:
TUPENDE KUTOA USHAHIDI WA KWELI, KUTENDA HAKI NA KUSAMEHE: Wakati Stefano anauawa alisema “Baba usiwahesabie dhambi hii.” Nasi tujifunze kuwa watu wa msamaha hasa pale tunapokosewa. Sauli akishuhudia mauaji ya Stefano aliona ni sawa. Hapa alisimama kama shuhuda. Tunapopata nafasi ya kutoa ushuhuda kwa jambo fulani tujitahidi kutenda haki na siyo kupindisha ukweli wa jambo lilivyo. Tukimwamini Yesu ipasavyo kama Injili inavyotudai, kamwe hatutaweza kusimamia uovu kama Sauli alivyofanya. Sauli na lile kundi lake walikosa imani kwa Mungu ndiyo maana walifurahia uovu wao.

SALA: Mtakatifu Stefano shahidi uliyemfia Kristo kwa kumwaga damu yako, utuombee.