APRILI 18, 2021; DOMINIKA: DOMINIKA YA 3 YA PASKA

Mwaka B
Nyeupe
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Mdo 3: 13-15, 17-19a.
Petro aliwaambia watu wote: Mungu wa Ibrahimu na wa Isaka na wa Yakobo, Mungu wa baba zetu, amemtukuza mtumishi wake Yesu; ambaye ninyi mlimsaliti na kumkana mbele ya Pilato, alipokuwa ametoa hukumu yake afunguliwe. Bali ninyi mlimkana yule mtakatifu, yule mwenye haki, mkataka mpewe mwuaji; mkamwua yule mkuu wa uzima, ambaye Mungu amemfufua katika wafu; na sisi tu mashahidi wake. Basi sasa, ndugu, najua ya kuwa mliyatenda haya kwa kutokujua kwenu, kama na wakuu wenu walivyotenda. Lakini mambo yale aliyohubiri Mungu tangu zamani kwa kinywa cha manabii wake wote, ya kwamba Kristo wake atateswa, ameyatimiza hivyo. Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe.

WIMBO WA KATIKATI: Zab 4: 1, 3, 6, 8

 1. Ee Mungu wa haki yangu, uniitikie niitapo;
  Umenifanyizia nafasi wakati wa shida;
  Unifadhili na kuisikia sala yangu.
  (K) Bwana, utuinulie nuru ya uso wako.
 2. Bali jueni ya kuwa Bwana amejiteulia mtauwa;
  Bwana atasikia nimwitapo. (K)
 3. Wengi husema, Nani atakayetuonesha mema?
  Bwana, utuinulie nuru ya uso wako. (K)
 4. Katika amani nitajilaza na kupata usingizi mara,
  Maana wewe, peke yako Bwana, peke yeko,
  Ndiwe unijaliaye kukaa salama. (K)

SOMO 2: 1 Yoh 2: 1- 5a
Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki, naye ndiye kipatanisho kwa dhambi zetu; wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote. Na katika hili twajua ya kuwa tumemjua yeye, ikiwa tunashika amri zake. Yeye asemaye, Nimemjua, wala hazishiki amri zake, ni mwongo, wala kweli haimo ndani yake. Lakini yeye alishikaye neno lake, katika huyo upendo wa Mungu amekamilika kweli kweli.

SHANGILIO: Lk 24:32
Aleluya, aleluya,
Bwana Yesu, utufunulie maandiko; uwashe mioyo yetu unaposema nasi.
Aleluya.

INJILI: Lk 24: 35- 48
Wafuasi waliwapa habari ya mambo yale ya njiani, na jinsi alivyotambulikana nao katika kuumega mkate. Na walipokuwa katika kusema habari hiyo, yeye mwenyewe alisimama katikati yao, akawaambia, Amani iwe kwenu. Wakashituka, wakaogopa sana, wakidhani ya kwamba wanaona roho. Akawaambia, mbona mnafadhaika? Na kwa nini mnaona shaka mioyoni mwenu? Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kuwa ni mimi mwenyewe. Nishikeni shikeni, mwone; kwa kuwa roho haina mwili na mifupa kama mnavyoniona mimi kuwa nayo. Na baada ya kusema hayo aliwaonesha mikono yake na miguu yake. Basi walipokuwa hawajaamini kwa furaha, huku wakistaajabu, aliwaambia, mna chakula chochote? Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa. Akakitwaa, akala mbele yao. Kisha akawaambia, hayo ndiyo maneno yangu niliyowaambia nilipokuwa ningali pamoja nanyi. Ya kwamba ni lazima yatimizwe yote niliyoandikiwa katika Torati ya Musa, na katika Manabii, na Zaburi. Ndipo akawafunulia akili zao wapate kuelewa na maandiko. Akawaambia, ndivyo ilivyoandikwa, kwamba Kristo atateswa na kufufuka siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi, kuanza tangu Yerusalemu. Nanyi ndinyi mashahidi wa mambo hayo.

TAFAKARI:
KUKUTANA NA YESU MFUFUKA, EPUKA NDOTO ZISIZO NA UHALISIA: Kulikuwa na dereva treni aliyefanya safari za kwenda na kurudi kila siku kupitia barabara hiyo hiyo. Aliweza kuizoea barabara kiasi kwamba aliweza kufanya kazi hiyo akiwa amefunga macho. Akiwa kama dereva, aliweza kufahamu mengi yaliyokuwa kando ya barabara hii. Kando ya barabara, kulikuwa na kijumba kdogo kilichomvutia sana. Kilijengwa mbali kidogo na njia ya treni. Alikipenda sana na kusema “ooh sehemu nzuri ilioje kuishi?”, “Ooh, pengine siku moja nikistaafu kazi nitaishi sehemu kama hii!” alijisemea. Kuta za kijumba hicho pamoja na maua yaliyokizunguka zilimfurahisha sana. Siku moja mchana alipita katika eneo hilo na kumuona mtoto akicheza mbele ya kile kijumba. Yule mtoto akampungia mkono, naye alimjibu kwa kumpigia honi. Siku iliyofuata ikatokea tena hivyo hivyo. Na palitokea urafiki kati yake na yule mtoto. Kila mchana alikuwa pale akimpungia dereva naye alimjibu kwa kumpigia honi. Wakati mwingine dereva alimkuta mtoto akiwa pamoja na mama yake mbele ya kijumba hicho na hivyo walijikuta wakimpungia mkono wote na dereva aliwajibu kwa kuwapigia honi. Kitendo hiki kilimfurahisha sana dereva. Kilizifanya safari zake za kila siku kuonekana fupi. Kila wakati alikuwa anasubiria kuwaona mama na mtoto wakimpungia mkono. Na kama ikitokea mmoja wao kati ya mama au mtoto hakujitokeza, dereva alijisikia vibaya sana. Moyo wake ulipata huzuni na safari kuwa ndefu na ya kuchosha. Miaka ikapita mtoto akakua. Umoja uliotengenezwa kwa miaka ulizidi kuendelea. Mwishowe, dereva alistaafu na kwenda kuishi sehemu ya mbali. Lakini ilimwia vigumu kuwasahau rafiki zake hawa. Hivyo siku moja akaamua kuwatembelea.

Alipofika karibu na nyumba ile, mambo yalikuwa tofauti na alivyotegemea. Kuta za kile kinyumba hazikuwa nyeupe kama alivyotegemea. Nyufa zilikuwa zinaonekana. Yale maua hayakuwa mazuri kama alivyofikiria kwanza. Kiukweli yalikuwa ya kawaida kabisa Hata ile bustani ilikuwa na magugu makubwa kuzunguka ile nyumba. Miti ile haikuwa mizuri kama alivyodhani. Mbaya zaidi alikata tamaa kabisa alivyokutana na yule mama na mtoto. Walikuwa wapole kwake alivyojitambulisha kwao. Walimkaribisha sehemu ya kawaida kabisa Ilikuwa pia vigumu kwao kuanzisha mazungumzo. Dereva alijisikia vibaya sana. Alilaumu uamuzi wake wa kupanga safari ya kuja kuwatembelea. Taratibu alianza kuondoka huku akijisikia mtupu sana. Ndoto aliyoijenga ndani ya akili yake na kuishikilia kwa muda mrefu aliiona kama zawadi iliyokimbia kutoka katika mikono yake. Umoja uliokuwapo kabla kati yao na ambao ulimpa maana na kuburudisha maisha yake aliona kaupoteza. Lakini alivyokuwa akiondoka alitambua kwamba shida siyo wao bali ni yeye mwenyewe. Hapa hatuna la kusema bali kumuonea huruma huyu dereva. Lakini je, haikuwa kosa kwake kuishi katika ulimwengu wa ndoto na kuacha kuishi katika maisha ya kweli? Ulimwengu wake wa ndoto ulikuwa mzuri sana lakini ulikuwa pia na hisia zenye kukosa uhalisia. Lakini ni wazi kwamba hata ulimwengu halisi unaweza kuwa mzuri zaidi ikiwa tutajitahidi kuondokana na ndoto potofu.

Yaliyomtokea huyu dereva ndiyo yaliyowatokea na mitume pia. Wengi walifuata zaidi hisia za mioyo yao. Kwani kwa miaka mitatu walitegemea na kufikiria mambo yasiyo na uhalisia. Walimtegemea Masiha atakayetawala dunia kama viongozi wengine wa kidunia, Masiha asiyepatwa na mateso au kifo (Mt 16:22). Hivyo baada ya kifo, walikata tamaa kabisa na kubakia katika hofu kuu. Hii siyo namna nzuri ya kuishi. Bila kutiwa moyo na Yesu, hakika wangaliacha ufuasi wao kwa Yesu. Katika Injili yetu leo, Yesu anawafundisha uhalisia kuhusu Masiha na kubadili ndoto zao. Ukweli ni kwamba Yesu, kwa njia ya mateso na kifo cha aibu, aliingia katika utukufu wake. Yesu anapofufuka, anawaonesha vidonda vyake na hata kushiriki chakula pamoja nao. Ilichukua muda kwa hili kuingia katika akili zao. Baada ya kupata ufahamu kamili, walipata kutambua kwamba mateso au kifo haviwezi kuvunja urafiki wao na Masiha.
Yesu anapowatokea wanafunzi wake na kushiriki nao katika kuumega mkate (jambo ambalo aliwahi kufanya akiwa pamoja nao) ni udhibitisho kwamba hakika amefufuka. Tunapokutana na Bwana Yesu katika Ekaristi Takatifu, tunakutana na Yesu, Neno wa Mungu. Yesu huja kwetu kwa njia ya neno na sakramenti na kutupatia tumaini jipya na kutuongezea imani. Tunapaswa kumtambua katika kuumega mkate. Ubaya ni kwamba sisi tuna tabia ya kuuona ufufuko kama tukio la zamani lililotokea katika eneo na muda fulani. Ekaristi Takatifu inapaswa kutufanya tufurahie furaha iliyoletwa na ufufuko wa Bwana wetu. Ekaristi Takatifu itufanye tuone uhalisia wa ufufuko wa Bwana wetu.

Ukweli ni kwambaYesu mfufuka anaendelea kuleta amani na furaha katika maisha ya waamini wake. Yupo tayari kushirikisha maisha yake mapya pamoja na rafiki zake. Ufufuko wake uliwafanya mitume waanze maisha mapya ya upendo na majitoleo kama inavyotokea kwa Petro na mitume wenzake katika somo la kwanza. Mitume wapo tayari kuuchukua mwanga wa Pasaka na kuupeleka katika giza la maisha ya watu. Nasi turuhusu Kristo mfufuka aingie ndani mwetu na kutuondolea roho ya uchoyo, woga, kisasi na tamaa.

SALA: Ee Bwana, ninakushukuru wewe kwa kutembea nami katika safari yangu. Ninakuomba nitambue maana ya ufufuko katika maisha yangu. Ninakuomba nikutane nawe katika maisha yangu.