APRILI 17, 2021; JUMAMOSI: JUMA LA 2 LA PASKA

Nyeupe
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Mdo 6:1-7
Siku zile wanafunzi walipokuwa wakiongezeka hesabu yao, palikuwa na manung’niko ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku. Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani. Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili; na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile neno. Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia; ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu yao. Neno la Mungu likaenea; na hesabu ya Wanafunzi ikazidi sana katika Yerusalemu; jamii kubwa ya makuhani wakaitii ile imani.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 33:1-2, 4-5, 18-19

 1. Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki,
  Kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.
  Mwimbieni wimbo mpya,
  Pigeni kwa ustadi kwa sauti ya shangwe.
  (K) Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi, Kama vile tulivyokungoja Wewe.
 2. Kwa kuwa neno la Bwana lina adili,
  Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
  Huzipenda haki na hukumu,
  Nchi imejaa fadhili za Bwana. (K)
 3. Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao,
  Wazingojeao fadhili zake.
  Yeye huwaponya nafsi zao na mauti,
  Na kuwahuisha wakati wa njaa. (K)

INJILI: Yn 6:16-21
Jioni wanafunzi walitelemka baharini; wakapanda chomboni, wakaanza kuivuka bahari kwenda Kapernaumu. Nako kumekwisha kuwa giza, wala Yesu hajawafikia. Na bahari ikaanza kuchafuka kwa kuvuma upepo mkuu. Basi wakavuta makasia kadiri ya maili tatu nne, wakamwona Yesu anakwenda juu ya bahari na kukikaribia chombo; wakaogopa. Naye akawaambia, Ni mimi, msiogope. Basi wakataka kumpokea chomboni; na mara hiyo chombo kikaifikilia nchi waliyokuwa wakiiendea.

TAFAKARI:
HOFU KATIKA MAISHA HUSABABISHA AMANI KUTOWEKA: Katika imani yetu, utume wa Kanisa unamwalika kila mwamini katika jukumu fulani ambapo katika kutimiza hayo vyema tunakamilisha ule utume wa Kristo tulioachiwa. Ndiyo maana tunaona katika somo la kwanza mitume baada ya kuona idadi inaongezeka, wanaomba kuongezewa nguvu. Nasi leo hii kila mmoja ajiulize, anatimiza utume gani katika Kanisa? Tuelewe pia katika kutimiza utume huo, misukosuko, vipingamizi havitakosekana. Injili inaweka wazi hili, kuwa bahari ilichafuka na mitume wakawa wanahangaika. Yesu anadhihirisha kuwa akiwa nasi katika majukumu yetu hatutashindwa. Tumtegemee yeye, tusiogope wala kuwa na hofu. Tutavuka salama kama tutakuwa naye, tusitegemee nguvu zetu wala uzoefu wetu.

SALA: Twakuomba, ee Yesu, utuvushe salama pale tunapokumbwa na vipingamizi wakati wa kutimiza majukumu yetu.