APRILI 13, 2021; JUMANNE: JUMA LA 2 LA PASAKA

Mt. Martino I, Baba Mt. Shahidi
Nyeupe
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Mdo 4:32-37
Jamii ya watu walioamini walikuwa na moyo mmoja na roho moja; wala hapana mmoja aliyesema ya kuwa kitu cho chote alicho nacho ni mali yake mwenyewe; bali walikuwa na vitu vyote shirika. Na mitume wakatoa ushuhuda wa kufufuka kwake Yesu kwa nguvu nyingi, na neema nyingi ikawa juu yao wote. Wala hapakuwa na mtu mmoja miongoni mwao mwenye mahitaji; kwa sababu watu wote waliokuwa na viwanja au nyumba waliviuza, wakaileta thamani ya vitu vile vilivyouzwa, wakaiweka miguuni pa mitume; kila mtu akagawiwa kwa kadiri ya alivyohitaji. Na Yusufu, aliyeitwa na mitume Barnaba, (maana yake, Mwana wa faraja), Mlawi, asili yake ni mtu wa Kipro, alikuwa na shamba akaliuza, akaileta fedha, akaiweka miguuni pa mitume.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 93:1-2, 5

 1. Bwana ametamalaki, amejivika adhama,
  Bwana amejivika, na kujikaza nguvu.
  (K)Bwana ametamalakai, amejivika adhama.
 2. Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike;
  Kiti chako kimekuwa thabiti tokea zamani;
  Wewe ndiwe uliye tangu milele. (K)
 3. Shuhuda zako ni amini sana;
  Utakatifu ndio uifaao nyumba yako.
  Ee Bwana, milele na milele. (K)

INJILI: Yn 3:7-15
Yesu alimwambia Nikodemo: Usistaajabu kwa kuwa nilikuambia, Hamna budi kuzaliwa mara ya pili. Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda; kadhalika na hali yake kila mtu aliyezaliwa kwa Roho.
Nikodemo akajibu, akamwambia, Yawezaje kuwa mambo haya?
Yesu akajibu, akamwambia, Je, wewe u mwalimu wa Israeli, na mambo haya huyafahamu? Amin, amin, nakuambia kwamba, Lile tulijualo twalinena, na lile tuliloliona twalishuhudia; wala ushuhuda wetu hamwukubali. Ikiwa nimewaambia mambo ya duniani, wala hamsadiki, mtasadiki wapi niwaambiapo mambo ya mbinguni? Wala hakuna mtu aliyepaa mbinguni, ila yeye aliyeshuka kutoka mbinguni, yaani, Mwana wa Adamu Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye.

TAFAKARI:
USHIRIKIANO HULETA FURAHA KATIKA JAMII: Somo la kwanza linatualika tuwe watu wa kushirikiana na kushirikishana makuu ya Mungu. Jamii yetu ya leo wengi tunajikuta tunahangaikia mali hadi kujisahau. Unakuta mtu ana biashara kila kona, mashamba kila mahali, magari mbalimbali na hii imesababisha wengine hata kuwasahau wazazi na ndugu zao. Jamii aliyoiacha Yesu haikuwa hivi. Leo hii ubinafsi umetawala, watu wana mageti, zio za umeme na mbwa wakali. Hii yote ni kutokana na roho wa umimi, hakuna aliye tayari kushirikiana na mwingine. Dhana hii ndiyo anayoambiwa Nikodemo katika Injili kuwa mwanadamu ni mkaidi, hata ukimweleza jambo zuri hakubali. Ukimweleza ubaya wa ubinafsi na kujilundikia mali kulikokithiri inakuwa ni kuzua ugomvi usioisha. Hapo ni kuziba masikio ya usikivu wa ndani, tunasahau kuwa hapa duniani ni mahali pa mpito na ndiyo maana Yesu anasema, “Mtasadiki wapi niwaambiapo mambo ya mbinguni?’ Na ndiyo maana tena kuna mtu yuko tayari akeshe kwenye biashara zake lakini kanisani hakanyagi. Vibaya kweli!

SALA: Tunaomba Baba utujalie neema ya kutumia vyema yale uliyotujalia ili yatustahilishe uzima wa milele.