Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku
SOMO 1: Mdo 10:34, 37-43
Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Jambo lile ninyi mmelijua, lililoenea katika Uyahudi wote likianzia Galilaya, baada ya ubatizo aliohubiri Yohane; habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu; naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye. Nasi tu mashahidi wa mambo yote aliyoyatenda katika nchi ya Wayahudi na katika Yerusalemu; ambaye walimwua wakamtundika mtini. Huyo Mungu alimfufua siku ya tatu, akamjalia kudhihirika, si kwa watu wote, bali kwa mashahidi waliokuwa wamekwisha kuchaguliwa na Mungu, ndio sisi, tuliokula na kunywa naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu. Akatuagiza tuwahubiri watu na kushuhudia ya kuwa huyu ndiye aliyeamriwa na Mungu awe Mhukumu wa wahai na wafu. Huyo manabii wote humshuhudia, ya kwamba kwa jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi.
WIMBO WA KATIKATI: Zab 118:1-2, 16-17, 22-23
- Aleluya.
Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema,
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Israeli na aseme sasa,
Ya kwamba fadhili zake ni za milele
(K) Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, Tutashangilia na kuifurahia. - Mkono wa kuume wa Bwana umetukuzwa;
Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.
Sitakufa bali nitaishi,
Nami nitayasimulia matendo ya Bwana. (K) - Jiwe walilokataa waashi
Limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Neno hili limetoka kwa Bwana,
Nalo ni ajabu machoni petu. (K)
SOMO 2: Kol 3:1-4
Mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu.
SHANGILIO: 1 Kor 5:7-8
Aleluya, aleluya,
Kristo, Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka;
Basi na tuifanye karamu katika Bwana!
Aleluya.
INJILI: Yn 20:1-9
Hata siku ya kwanza ya juma Maria Magdalene alikwenda kaburini alfajiri, kungali giza bado; akaliona lile jiwe limeondolewa kaburini. Basi akaenda mbio, akafika kwa Simoni Petro na kwa yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, Wamemwondoa Bwana kaburini, wala hatujui walikomweka. Basi Petro akatoka, na yule mwanafunzi mwingine, wakashika njia kwenda kaburini. Wakaenda mbio wote wawili; na yule mwanafunzi mwingine akaenda mbio upesi kuliko Petro, akawa wa kwanza wa kufika kaburini. Akainama na kuchungulia, akaviona vitambaa vya sanda vimelala; lakini hakuingia. Basi akaja na Simoni Petro akimfuata, akaingia ndani ya kaburi; akavitazama vitambaa vilivyolala; na ile leso iliyokuwako kichwani pake; haikulala pamoja na vitambaa, bali imezongwazongwa mbali mahali pa peke yake. Basi ndipo alipoingia naye yule mwanafunzi mwingine aliyekuwa wa kwanza wa kufika kaburini, akaona na kuamini. Kwa maana hawajalifahamu bado andiko, ya kwamba imempasa kufufuka.
TAFAKARI:
UFUFUKO NI CHANZO CHA MATUMAINI: Leo ni siku kubwa na muhimu sana kwetu sisi Wakristo. Ni siku ya ufufuko wa Kristo. Kitendo cha Yesu kufufuka katika wafu ni tendo kuu kwetu na hivyo tumshukuru Mwenyezi Mungu. Maneno ya wimbo wa kwanza leo yanatoka katika Zaburi ya 139. Hii ni zaburi iliyoimbwa na Daudi alipojaribu kustaajabia uwezo wa Mungu ulivyo wa ajabu kwake, jinsi Mungu anavyojua kila kitu kuhusiana na maisha yake. Sisi tunatumia zaburi hii leo kama sala ya ushindi kwa Kristo, kwamba Kristo amepata ushindi juu ya aibu ya kifo. Baba yupo upande wa Kristo na hivyo tunastaajabia ushindi wake. Sisi tutumie nyimbo hizi kumpatia Kristo wetu sifa kwa ushindi anaoupata juu ya kifo.
Kiitikio cha sekwensia yetu kinatoka katika waraka wa kwanza wa mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor 5:7-8). Haya ni maneno aliyoyatumia Paulo kuonesha kwamba Kristo amekwisha kutuletea uzima mpya kwa kufufuka kwake na hivyo yatubidi nasi kuishi katika upya huo, hakika yatupasa tuache dhambi. Mtume Paulo alitumia maneno haya akiwaonya Wakorintho kwamba wasijiweke tena chini ya nira ya yule mwovu. Anasisitiza kwamba Kristo amekwishajitoa sadaka, hivyo tuachane na dhambi. Kwetu sekwensia hii ni wimbo wa ushindi wenye kushuhudia ufufuko wa Kristo. Inatutaka kuachana na dhambi na kumgeukia Kristo. Tuepuke kuchanganya Ukristo na dhambi kama walivyofanya Wakorintho. Tumpokee Kristo.
Kristo aliyefufuka kutoka wafu ni mwanga unaoangaza dunia yote na kufukuza giza. Tulianza ibada yetu ya mkesha wa usiku wa vijilia kwa kuwasha moto. Makabila ya kaskazini mwa Ujerumani yalikuwa na tamaduni ya kuwasha moto kipindi cha mwaka ambacho usiku ulikuwa mrefu kuliko mchana. Waliamini kwamba kwa kufanya hivyo kwa muda mrefu, kipindi hiki cha giza hutoweka na kuja kipindi cha mwanga. Lakini kwetu Wakristo, moto wa Pasaka ni ishara kwamba Kristo amefufuka. Mshumaa unaowaka ni ishara ya Kristo mfufuka na ufufuko wake umefukuza giza lote. Giza ni ishara ya dhambi na mauti. Mshumaa wa Pasaka karibu na altare yetu ni ishara ya Kristo mfufuka aliyeko mbele yetu akituangaza.
Maneno ya somo letu la kwanza yalisemwa na mtume Petro kwa Korneli, aliyekuwa afisa wa Kirumi huko Kaisarea. Hii ni hotuba ya kwanza ya Mtume Petro kwa watu wa mataifa na cha kuvutia katika hotuba hii, yeye anaufanya ufufuko uwe fundisho kuu na udhibitisho mahiri wa imani ya Kikristo kwamba kama Kristo hakufufuka, imani yetu ni bure. Anaelezea jinsi Yesu alivyoteswa, kuuawa na siku ya tatu kufufuka. Kama mtume Paulo, Petro anaelezea ukweli wa ufufuko kwa kuonesha idadi kubwa ya watu walioshuhudia ufufuko, waliokula na kunywa pamoja naye baada ya ufufuko wake. Walikunywa pamoja naye, si kwamba mwili wa utukufu wa ufufuko ulihitaji chakula bali lengo lilikuwa ni kutoa ushuhuda kwamba ni kweli amefufuka. Walipewa amri ya kuwahubiria wote; huu ndio utume tupewao katika siku ya ufufuko.
Katika Injili yetu leo, tunakutana na Maria Magdalena akienda kaburini. Yeye kama ilivyokuwa kwa wanafunzi na wafuasi wengine, walikwenda kaburini bila matumaini lengo likiwa ni kuupaka mwili wa Yesu manukato. Walifikiria kwamba kaburi lilimeza matumaini yote. Wengi walikata tamaa na kutaka kuondoka; ufufuko ulibadili yote haya. Ufufuko unamfanya Kristo kuwa mshindi na suala hili linawatia moyo mitume wote na watalifanya kuwa mhimili wa imani ya Kikristo popote watakapokwenda (1Kor 15:12-19). Ndilo lililowafanya wavumilie shida, taabu na dhiki zote kwani walijua kwamba Kristo hakika hatawaacha, atakuja kuwaokoa na kuwapatia ufufuko na kuwapeleka alipo. Kama alivyokuwa tayari kuwashirikisha mamlaka mbalimbali ya uponyaji na kutoa pepo, vivyo hivyo atawashirikisha na ufufuko wake pia.
Katika somo la pili, mtume Paulo analinganisha ufufuko na ubatizo. Ubatizo huondoa dhambi ya asili. Ufufuko wa Yesu ulileta ushindi dhidi ya mauti iliyoletwa na dhambi ya asili. Ubatizo hutufanya tushiriki neema zilizoletwa na ufufuko wa Kristo. Tunapomwagiwa maji na kubatizwa, ni ishara ya kushiriki katika kifo cha Kristo na pia katika ufufuko wake. Kama sehemu ya kushiriki neema zitolewazo katika sherehe hii ya ufufuko, katika misa ya vijilia ya Pasaka tunapata tena nafasi ya kurudia maagano yetu ya ubatizo kuonesha kwamba kweli tumeshiriki katika neema ziletwazo na Kristo mfufuka na kuwa viumbe vipya. Hivyo, sisi kama Wakristo Pasaka kwetu ni siku takatifu na kama ilivyokuwa kosa kubwa kwa wana wa Israeli kuacha kuiadhimisha Pasaka, ndivyo ilivyo na kwetu sisi. Hatuwezi kuacha kuiadhimisha Pasaka. Kwa Waisraeli, Pasaka ilikuwa mwanzo wa miaka kwao kwani ndio siku walioiona hadharani nguvu ya Mungu ikiwaokoa. Na waliamriwa kuiadhimisha Pasaka kila mwaka ili waendelee kuiona nguvu hii ya Mungu maishani mwao hali wakitegemea ukombozi mkuu zaidi toka kwa Bwana. Ndivyo ilivyo kwetu sisi ndugu zangu, lazima tuiadhimishe Pasaka yetu ya Kikristo, ili tuweze kushiriki neema zilizotolewa katika usiku ule mtakatifu Kristo alipofufuka katika wafu.
SALA:
Ee Bwana, umeijaza nchi fadhili zako. Unisaidie niweze kushirikisha wenzangu fadhili hizo ulizoijalia ulimwengu.