MACHI 31, 2021; JUMATANO: JUMA KUU

Urujuani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Isa 50:4-9
Bwana Mungu amenipa ulinzi wa hao wafundishwao, nipate kujua jinsi ya kumtegemea kwa maneno yeye aliyechoka, huniamsha asubuhi baada ya asubuhi; huniamsha, sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao. Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma. Niliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang’oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate. Maana Bwana Mungu atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya. Yeye anipatiaye haki yangu yu karibu; ni nani atakayeshindana nami? Na tusimame pamoja; ni nani aliye hasimu yangu? Na anikaribie basi. Tazama, Bwana Mungu atanisaidia; ni nani atakayenihukumu kuwa mkosa?

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 69:7-9, 20-21, 30, 32-33

 1. Kwa ajili yako nimestahimili laumu
  Fedheha imenifunika uso angu.
  Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu,
  Na msikwao kwa wana wa mama yangu.
  Maana wivu wa nyumba yako umenila,
  Na laumu zao wanaokulaumu zimenipata.
  (K)Kwa wingi wa fadhili zako unijibu, ee Bwana.
 2. Laumu imenivunja moyo,
  Nami ninaugua sana.
  Nikangoja aje wa kunihurumia, wala hakuna;
  Na wa kunifariji, wala sikumwona mtu.
  Wakanipa uchungu kuwa chakula changu;
  Nami nilipokuwa na kiu wakaninywesha siki. (K)
 3. Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo,
  Nami nitamtukuza kwa shukrani.
  Walioonewa watakapoona watafurahi;
  Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.
  Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji,
  Wala hawadharau wafunga wale. (K)

INJILI: Mt 26:14-25
Wakati huo mmoja wa wale Thenashara, jina lake Yuda Iskariote, aliwaendea wakuu wa makuhani, akasema, Ni nini mtakachonipa, nami nitamsaliti kwenu? Wakampimia vipande thelathini vya fedha. Tokea wakati huo akawa akitafuta nafasi apate kumsaliti. Hata siku ya kwanza ya mikate isiyotiwa chachu, wanafunzi wake wakamwendea Yesu, wakamwambia, Ni wapi utakapo tukuandalie uile Pasaka? Akasema, Enendeni mjini kwa mtu fulani, mkamwambie, Mwalimu asema, Majira yangu ni karibu; kwako nitafanya Pasaka pamoja na wanafunzi wangu. Wanafunzi wakafanya kama Yesu alivyowaagiza, wakaiandaa Pasaka. Basi kulipokuwa jioni aliketi chakulani pamoja na wale Thenashara. Nao walipokuwa wakila, alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu atanisaliti. Wakahuzunika sana, wakaanza kumwuliza mmoja mmoja, Ni mimi, Bwana? Akajibu akasema, Yeye aliyetia mkono wake pamoja nami katika kombe, ndiye atakayenisaliti. Mwana wa Adamu aenda zake, kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu! Ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa. Yuda, yule mwenye kumsaliti, akajibu, akasema, Ni mimi, Rabi? Akamwambia, Wewe umesema.

TAFAKARI:
RUSHWA NI ADUI WA HAKI NA MAENDELEO: Tunamwona Yuda Iskariote akiomba kupewa kitu ili atimize azma yake ya kumsaliti Yesu, yaani kumkabidhi kwa watesaji. Sehemu nyingi duniani watu wanadhulumiwa haki zao kwa sababu ya rushwa. Mwenye nacho ndiye mwenye nguvu. Hali hii ndiyo inayosababisha watu wanaondolewe uhai wao ambao ni zawadi ya pekee kutoka kwa Mungu. Yuda alijua fika ni yeye msaliti, lakini tunaona mbele ya mitume wenzake naye anajifanya kuuliza, “Ni mimi Rabi?” Huku kulikuwa kuendelea kuidanganya jumuiya angali anajua kinachoendelea. Ulikuwa unafiki mtupu. Wakati mwingine, katika unafiki wa namna hiyo, anaweza kufikiriwa au kutuhumiwa mtu mwingine wakati siye mwovu halisi. Tujifunze kuwa na moyo mweupe kama meno yetu yalivyo.

SALA: Baba tunaomba neema zako ili tuweze kujitambua na kutenda haki na tuache kuishi maisha ya kinafiki.