MACHI 28, 2021; DOMINIKA: DOMINIKA YA MATAWI

KUMBUKUMBU YA MATESO YA BWANA
Nyekundu
Zaburi: Tazama sala ya siku

INJILI: Mk 11:1-10
Hata walipokaribia Yerusalemu karibu na Bethfage na Bethania, kukabili mlima wa Mizeituni, aliwatuma wawili katika wanafunzi wake, akawaambia, Nendeni mpaka kile kijiji kinachowakabili; na katika kuingia ndani yake, mara mtaona mwana-punda amefungwa, asiyepandwa na mtu bado; mfungueni, kamleteni. Na mtu akiwaambia, mbona mnafanya hivi? Semeni, Bwana ana haja naye, na mara atamrudisha tena hapa. Wakaenda zao, wakamwona mwana-punda amefungwa penye mlango, nje katika njia kuu, wakamfungua. Baadhi ya watu waliosimama huko wakawaambia kama Yesu alivyowaagiza, nao wakawaruhusu. Wakamletea Yesu yule mwana-punda, wakatandika mavazi yao juu yake; akaketi juu yake. Watu wengi wakatandaza mavazi yao njiani, na wengine matawi waliyoyakata mashambani. Nao watu waliotangulia na wale waliofuata wakapaza sauti, Hosana; ndiye mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana; umebarikiwa na ufalme ujao, wa baba yetu Daudi. Hosana juu mbinguni.

SOMO 1: Isa 50:4-7
Bwana Mungu amenipa ulimi wa hao wafundishwao, nipate kujua jinsi ya kumtegemeza kwa maneno yeye aliyechoka, huniamsha asubuhi baada ya asubuhi; huniamsha, sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao. Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma. Naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang’oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate. Maana Bwana Mungu atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya.

WIMBO WA KATIKATI: Zab 22:7-8; 16-7a;-19; 22-23

 1. Wote wanionao hunicheka sana
  Hunifyonya, wakitikisa vichwa vyao;
  Husema: Umtegemee Bwana, na amponye;
  Na amwokoe sasa, maana apendezwa naye.
  (K) Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?
 2. Kwa maana mbwa wamenizunguka;
  Kusanyiko la waovu wamenisonga;
  Yamenizuia mikono na miguu.
  Naweza kuihesabu mifupa yangu yote. (K)
 3. Wanagawanya nguo zangu,
  Na vazi langu wanalipigia kura.
  Nawe, Bwana, usiwe mbali,
  Ee Mungu wangu, fanya haraka kunisaidia. (K)
 4. Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu,
  Katikati ya kusanyiko nitakusifu.
  Ninyi mnaomcha Bwana, msifuni
  Enyi nyote mlio wazao wa Yakobo, mtukuzeni. (K)

SOMO 2: Flp 2:6-11
Yesu mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.

SHANGILIO: Flp 2:8-9
Kristo alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.
Kwa hiyo tena, Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina.

INJILI: Mk : 14:1 – 15:47 (Historia ya mateso ya Bwana ya Mwaka “B”)

TAFAKARI:
HOSANNA MWANA WA DAUDI: Katika liturujia ya leo, tunakumbwa na hisia mbili tofauti. Tunaanza liturujia yetu kwa utukufu na shangwe kuenzi jinsi Yesu alivyoingia Yerusalemu kwa shangwe kwa kuimba, ‘Hosanna, hosanna juu mbinguni.’ Watu walifurahi kumuona Yesu akiingia Yerusalemu kwa shangwe, lakini hali hii inaanza kupotea taratibu; baada ya kuanza kuingia kwa undani katika masomo yetu, hali inabadilika na kuwa ya kushtua na huzuni. Injili inaisha kwa Yesu kutundikwa msalabani na Yesu analia kwa sauti kuu na kusema “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha!” na baada ya hayo Yesu anatoa pumzi yake ya mwisho na kukata roho.

Ni nini kilitokea kwa watu ambao walikuwa wakishangilia na kumsifu alivyokuwa anaingia Yerusalemu? Kwa nini ilikuwa rahisi kwao kumgeuka Yesu ndani ya muda mfupi vile? Sisi ndio wenye tabia zinazofanana na huu umati wa Yerusalemu. Wengi wetu ni kigeugeu, tunapenda kujitokeza katika matukio makubwa makubwa tu, tunapendelea kujioneshaonesha. Tunaohudhuria kanisani siku ya Dominika ya Matawi ni wengi kuliko tunaohudhuria katika Dominika nyingine za mwaka. Wengi wetu tunahudhuria kanisani katika Dominika maarufu maarufu kama washabiki wasiokuwa na msimamo Yesu anatuhitaji kila wakati, anatusubiri katika Ekaristi Takatifu lakini sisi hatupo tayari kuungana naye. Kila wakati tunamkana Yesu, tunamkana katika maskini na katika sakramenti. Huu umati ulimuacha Yesu kipindi alipowahitaji zaidi; walimuacha kipindi cha hukumu, mateso na alipokuwa msalabani. Kuna kipindi Yesu anatuhitaji zaidi; yafaaa tujitokeze Yesu anatuhitaji tumwendee tumwabudu katika Ekaristi Takatifu, tusaidie Kanisa kwa zaka, na tutoe mfano kwa kizazi kijacho kwa matendo mema.
Hivyo, tunapaswa tumpokee Yesu kila wakati. Yesu ndiye mwenye kutupatia hadhi na heshima. Punda anayembeba Yesu leo alipata heshima kubwa kwa kumbeba Yesu. Umati ulitandika nguo chini ili apate kupita, hakuna aliyempiga. Lakini wakati anarudishwa nyumbani kwa Bwana wake, hakupatiwa heshima tena kama hapo kwanza. Sisi tusikubali kumpoteza Yesu. Yeye ndiye mwenye kutupatia hadhi na heshima.

Zaburi yetu ya wimbo wa katikati inatoka katika Zaburi ya 22: “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha!” Ni zaburi ya maombolezo ambayo zamani Kanisa iliitumia pia katika siku ya Alhamisi kuu wakati wakivua vitambaa juu ya altare ya Kanisa kuashiria tukio la Yesu kuvuliwa nguo zake na kuachwa mtupu. Ni zaburi iliyobeba unabii wenye kuelezea mateso yatakayompata Masiha wa Israeli. Yanayoelezwa katika zaburi hii yalimpata na Yesu pia. Yesu alitobolewa mikono na miguu, baadhi ya rafiki zake walimkana na askari waligawana mavazi yake. Yote haya tumeyasikia katika historia yetu ya mateso. Katika historia hii, naomba tujifunze yafuatayo:-
Kwanza, tumeona kwamba ni Maria, mama yake, mtume mwaminifu kama Yohane na wengine wachache ndio walioweza kusimama pembeni karibu na Yesu wakati wa mateso yake. Wengine wote walikimbia. Waliobaki ni hawa tu. Sisi tusiache kuwathamini wazazi wetu na ndugu zetu pia. Mara nyingi ndio watakaobakia hadi ile siku yetu ya mwisho. Baadhi ya marafiki ni wa mpito tu. Tukadanganywe nao na kuwadharau ndugu zetu.
Pili, umati wa Yerusalemu ulikuwa geugeu. Umati huu ulimshangilia Yesu lakini mwishowe uliishia kumpenda Baraba kuliko Yesu. Je, mimi ni Mkristo wa makundi tu au Mkristo wa nyakati fulani fulani tu? Je, mimi ni Mkristo tu pale ninapopata pato fulani au sifa fulani? Wengi ni Wakristo wa makundi. Tunakuja kushangilia leo lakini siku nyingine hatupo na Kristo, hatuhudhurii ibada. Yabidi tubadilike. Idadi ya Wakristo wanaobatizwa ni kubwa lakini idadi ya Wakristo hai ni wachache sana. Wengi ni walegevu (T. Lane, Palm Sunday 2019).
Tatu, Petro alimsikia jogoo akiwika na kulia sana na kutubu. Dunia yetu inapaswa kuiga mfano wa Petro, yaani ikubali kutubu. Lakini dhamiri za baadhi ya walimwengu ni mfu. Hazisikii hata jogoo akiwika ndani ya mioyo yao. Sisi tuzijenge dhamiri zetu kuwa hai ili pale jogoo awikapo, tukimbilie sakramenti zake na kujipatanisha na Mungu. Wengi wetu hatuikimbilii sakramenti ya Kitubio. Ni kwa sababu dunia imeua dhamiri zetu. Tufufue dhamiri zetu, tuepuke kuwa kama Yuda aliyekaza moyo wake kuwa mgumu na kushindwa kutubu (T. Lane, Palm Sunday 2019).
Nne, Yesu alipokumbana na magumu, alikimbilia sala. Alisali kwa nguvu zake zote. Nasi tuikimbilie sala wakati wa kujaribiwa kwetu. Tumlilie Mungu, hakika atakuokoa. Sala ni ngao kubwa katika kupambana na mateso ya ulimwengu huu.

SALA: Bwana, ninapojaribiwa mpaka kukaribia kukata tamaa, naomba unipe matumaini. Ninaomba juma hili kuu, libadilishe nyakati zangu za giza na mapungufu yangu.