MACHI 26, 2021; IJUMAA: JUMA LA 5 LA KWARESIMA

Urujuani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Yer 20:10-13
Nimesikia mashutumu ya watu wengi; hofu ziko pande zote. Rafiki zangu wote wanaonivizia nisite, husema, Mshitaki, nasi tutamshitaki; huenda akahadaika; nasi tutamshinda, tutajilipiza kisasi kwake. Lakini Bwana yu pamoja nami, mfano wa shujaa mwenye kutisha; kwa hiyo hao wanaonionea watajikwaa, wala hawatashinda; watatahayarika sana. Kwa sababu hawakutenda kwa akili, wataona aibu ya milele, ambayo haitasahauliwa kamwe. Lakini, Ee Bwana wa majeshi, wewe wawajaribu wenye haki, waona viuno na mioyo, nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu. Mwimbieni Bwana; msifuni Bwana; kwa maana ameiponya roho ya mhitaji katika mikono ya watu watendao maovu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 18:1-6

 1. Wewe, Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana;
  Bwana ni jabali langu, na boma langu, na mwokozi wangu
  Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia,
  Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome yangu.
  Nitamwita Bwana astahiliye kusifiwa,
  Hivyo nitaokoka na adui zangu.
  (K)Katika shida yangu nalimwita Bwana,
  Akaisikia sauti yangu.
 2. Kamba za mauti zilinizunguka,
  Mafuriko ya uovu yakanitia hofu.
  Kamba za kuzimu zilinizunguka,
  Mitego ya mauti ikanikabili. (K)
 3. Katika shida yangu nalimwita Bwana,
  Na kumlalamikia Mungu wangu.
  Akaisikia sauti yangu hekaluni mwake,
  Kilio changu kikaingia masikioni mwake. (K)

INJILI: Yn 10:31-42
Wayahudi waliokota mawe ili wampige. Yesu akawajibu, Kazi njema nyingi nimewaonesha, zitokazo kwa baba; kwa ajili ya kazi ipi katika hizo mnanipiga kwa mawe? Wayahudi wakamjibu, Kwa ajili ya kazi njema hatukupigi kwa mawe; bali kwa kukufuru, na kwa sababu wewe uliye mwanadamu wajifanya mwenyewe u Mungu. Yesu akawajibu, Je! Haikuandikwa katika torati yenu ya kwamba, Mimi nimesema, Ndinyi miungu? Ikiwa aliwaita miungu wale waliojiliwa na neno la Mungu; (na maandiko hayawezi kutanguka); je! Yeye ambaye Baba alimtakasa, akamtuma ulimwenguni, ninyi mnamwambia, Unakufuru; kwa sababu nalisema, Mimi ni Mwana wa Mungu? Kama sizitendi kazi za Baba yangu, msiniamini; lakini nikizitenda, ijapokuwa hamniamini mimi, ziaminini zile kazi; mpate kujua na kufahamu ya kuwa Baba yu ndani yangu, nami ni ndani ya Baba. Wakatafuta tena kumkamata; lakini akatoka mikononi mwao. Akaenda zake tena ng’ambo ya Yordani, mpaka mahali pale alipokuwapo Yohane akibatiza hapo kwanza, akakaa huko. Na watu wengi wakamwendea, wakasema, Yohane kweli hakufanya ishara yo yote, lakini yote aliyoyasema Yohane katika habari zake huyu yalikuwa kweli. Nao wengi wakamwamini huko.

TAFAKARI:
TUHUKUMU KWA HAKI: Kuna usemi wa Kiingereza usemao, “Mob has no face.” Ujumbe ulioko katika usemi huu ndio unaojitokeza katika Injili ya leo. Tumesikia Wayahudi waliokota mawe ili wampige Yesu. Huenda katika kundi hilo ni wawili au watatu waliokuwa na chuki na Yesu lakini wakawashawishi wengine wawaunge mkono. Kwa ulimwengu wetu huu, jambo hili hutokea sana. Utakuta watu wanamfukuza mtu kwa kisa cha wizi, lakini ukimwuliza mmoja wao swali, ‘Ameiba nini?”usishangae akakosa jibu au akajibu tu, ‘Nimekuta watu wanamfukuza nami nikajiunga nao.’ Kumbe, ni tabia hii inayosababisha watu wengine wauawe wakati siyo wezi. Kwa kweli, hayo ni mapato ya ufuataji mkumbo tu. Tunakuwa wepesi wa kuhukumu pasipo taarifa sahihi; tunakuwa watu wa kuongozwa na makelele ya wengi tu. Shime, tujitegemee katika kufikiri na kutenda.

SALA: Ee Yesu, tusamehe pale tulipohukumu wengine bila hatia.