MACHI 25, 2021; ALHAMISI: JUMA LA 5 LA KWARESIMA

KUPASHWA HABARI YA KUZALIWA BWANA
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO 1: Isa 7: 10-14
Bwana alisema na Ahazi akinena, jitakie ishara ya Bwana, Mungu wako; itake katika mahali palipo chini sana, au katika mahali palipo juu sana. lakini Ahazi akasema, sitaitaka, wala sitamjaribu Bwana. Naye akasema, sikilizeni sasa, enyi nyumba ya Daudi; Je! ni neno dogo kwenu kuwachosha wanadamu, hata mkataka kumchosha Mungu wangu Pia? Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachukua mimba, atamzaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.
WIMBO WA KATIKATI Zab.40:6-10
WIMBO WA KATIKATI:

  1. Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,
    Masikio yangu umeyazibua,
    Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
    Ndipo niliposema, Tazama nimekuja.
    (K)Tazama, nimekuja, Ee Bwana,
    kuyafanya mapenzi yako.
  2. Katika gombo la chuo nimeandikiwa
    Kuyafanya mapenzi yako,
    Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu;
    Naam, sheria yako imo moyoni mwangu. (K)
  3. Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa,
    Sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, unajua. (K)
  4. Sikusitiri haki yako moyoni mwangu;
    Nimetangaza uaminifu wako na wokovu wako.
    Sikuficha fadhili zako wala kweli yako
    Katika kusanyikko kubwa. (K)

SOMO 2: Ebr 10:4-10
Haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi. kwa hiyo ajapo ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo; Ndipo niliposema, tazama, nimekuja, (katika gombo la chuo nimeandikiwa) Niyafanyie mapenzi yako, Mungu. Hapo juu asemapo, dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo, (Zitolewazo kama ilivyoamuru torati), Ndipo aliposema, tazama, nimekuja niyaqfanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza ili kusudi alisimamishe la pili. Katika mapenzi hayo tumepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.

INJILI: Lk 1:26-38
Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni MariAmu Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema. Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elizabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.

TAFAKARI:
KUFIKISHA UJUMBE KWA MLENGWA KAMA UNAVYOTAKIWA: Leo Mama Kanisa anaadhimisha tukio la kupashwa habari Bikira Maria. Jambo mojawapo kati ya yale tunayoweza kujifunza ni utayari na unyenyekevu. Bikira Maria alipata bahati hii kwa sababu alikuwa na hizi fadhila. Lakini tujifunze pia ufikishaji taarifa kwa walengwa kama inavyotakiwa. Malaika Gabriel alipotumwa na Mungu hakuongeza neno. Katika jamii zetu za leo, wengi wetu hatufikishi ujumbe kama inavyotakiwa, tunaongeza vionjo vyetu na mawazo yetu. Jambo hili linasababishwa na tabia ya kujitafutia umaarufu. Lakini mwisho linatuondolea unyenyekevu. Hali kadhalika leo tunaalikwa kuelewa kuwa hatuwezi kuzuia mpango wa Mungu. Mungu akiamua jambo lake lazima atalitekeleza tu. Hata ipite miaka mingi kiasi gani, ahadi ya Mungu lazima itekelezwe. Yeye haongopi.

SALA: Bikira Maria mama mnyenyekevu, utuombee