2021 MACHI 23 JUMANNE: JUMA LA 5 LA KWARESIMA

Mt. Turibio wa Mongrovejo, Askofu
Urujuani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Hes 21: 4-9
Wakasafiri kutoka mlima wa Hori kwa njia ya bahari ya Shamu; ili kuizunguka nchi ya Edomu, watu wakafa moyo kwa sababu ya ile njia. Watu wakamnung’unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu. Bwana akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa. Watu wakamwendea Musa, wakasema, tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung’unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa Bwana, atuondolee nyoka hawa. Basi Musa akawaombea watu. Bwana akamwambia Musa, jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo, ataishi. Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikawa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 102:1-2, 15-20

 1. Ee Bwana, usikie kuomba kwangu,
  Kilio changu kikufikie.
  Usinifiche na uso wako siku ya shida yangu,
  Unitegee sikio lako, siku niitapo unijibu upesi.
  (K)Ee Bwana, usikie kuomba kwangu,
  Kilio changu kikufikie.
 2. Kisha mataifa wataliogopa jina la Bwana,
  Na wafalme wote wa dunia utukufu wako;
  Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni,
  Atakapoonekana katika utukufu wake,
  Asiyadharau maombi yao. (K)
 3. Kizazi kitakachokuja kitaandikiwa hayo,
  Na watu watakaoumbwa watamsifu Bwana.
  Maana ametazama toka patakatifu pake pa juu,
  Ili akusikie kuugua kwake aliyefungwa,
  Na kuwafungua walioandikiwa kufa. (K)

INJILI: Yn 8: 21-30
Yesu aliwaambia Mafarisayo: Mimi naondoka, nanyi mtanitafuta; nanyi mtakufa katika dhambi yenu; mimi niendako ninyi hamwezi kuja. Basi Wayahudi wakasema, Je! Atajiua! Kwa kuwa asema, Mimi niendako ninyi hamwezi kuja? Akawaambia, Ninyi ni wa chini, mimi ni wa juu; ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu. Kwa hiyo naliwaambieni ya kwamba mtakufa katika dhambi zenu; Kwa sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu. Basi wakamwambia, U nani wewe? Yesu akawaambia, Hasa neno lilo hilo ninalowaambia. Ninayo mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu; lakini yeye aliyenipeleka ni kweli, nami niliyoyasikia kwake ndiyo ninenayo katika ulimwengu. Wala hawakutambua ya kuwa anawatajia Baba. Basi Yesu akawaambia, mtakapokuwa mmekwisha kumwinua Mwana wa Adamu, ndipo mtakapofahamu ya kuwa mimi ndiye; na ya kuwa sifanyi neno kwa nafsi yangu, ila kama baba alivyonifundisha ndivyo ninenavyo. Naye aliyenipeleka yu pamoja nami; hakuniancha peke yangu; kwa sababu nafanya siku zote yale yampendezayo. Naye alipokuwa akisema hayo, wengi walimwamini.

TAFAKARI:
MWANADAMU HATOSHEKI: Katika somo la kwanza tumeona wana wa Israeli wanalalamika, wanasahau kuwa Mungu hajawaacha. Wakati mwingine mtu akipatwa na tatizo dogo anasahau mema yote aliyotendewa. Kuna wakati unaweza kukumbwa na kikwazo katika maisha na hivyo kikakukumbusha kuona ulikotoka. Mfano, ukiugua malaria baada ya kulala bila chandarua cha mbu unaweza kukumbuka uzembe au ukaidi wako. Wana wa Israeli hawakupaswa kulalamika vile hadi kusahau wema aliowatendea Mungu. Na Yesu katika Injili anakazia swala la kuwa wasikivu. Kuna wakati inatokea mtu anaamua kutokuwa msikivu kwa jambo analoelekezwa huku akiuliza maswali mengi yasiyo na tija kwa vile tu hana mpango wa kufuata analoelekezwa. Tuache tabia ya namna hii.

SALA: Tunaomba utujalie neema ya kuwa watu wa shukrani hasa pale tunapotendewa mema.