MACHI 21, 2021; DOMINIKA: DOMINIKA YA 5 YA KWARESIMA

Urujuani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Yer 31 :31-34
Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda. Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema Bwana. Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile asema Bwana; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue Bwana; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongo mwao, asema Bwana; maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena.

WIMBO WA KATIKATI: Zab 51: 1-2, 10-13.

 1. Ee Mungu unirehemu,
  Sawasawa na fadhili zako.
  Kiasi cha wingi wa rehema sako,
  Uyafute makosa yangu.
  Unioshe kabisa na uovu wangu,
  Unitakase dhambi zangu.
  (K) Ee Mungu, uniumbie moyo safi.
 2. Ee Mungu uniumbie moyo safi,
  Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
  Usinitenge na uso wako,
  Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. (K)
 3. Unirudishie furaha ya wokovu wako;
  Unitegemeze kwa roho wa wepesi.
  Nitawafundisha wakosaji njia zako,
  Na wenye dhambi watarejea kwako. (K)

SOMO 2: Ebr 5 :7-9
Yesu, siku hizo za mwili wake, alimtolea yule awezaye kumwokoa na kumtoa katika mauti, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu; na, ingawa ni Mwana, alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata; naye alipokwisha kukamilishwa, akawa sababu ya wokovu wa milele kwa watu wote wanaomtii.

SHANGILIO: Yn 12:26
Mtu akinitumikia, na anifuate, asema Bwana;
Nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo.

INJILI: Yn 12 :20-33
Palikuwa na Wayunani kadha wa kadha miongoni mwa watu waliokwea kwenda kuabudu kwenye sikukuu. Basi hao walimwendea Filipo, mtu wa Bethsaida ya Galilaya, wakamwomba, wakisema, Bwana, sisi tunataka kumwona Yesu. Filipo akaenda, akamwambia Andrea; kisha Andrea na Filipo wakamwambia Yesu. Naye Yesu akawajibu, akasema, Saa imefika atukuzwe Mwana wa Adamu Amin, amin, nawaambia, chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi. Yeye aipendaye nafsi yake ataingamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele. Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu. Sasa roho yangu imefadhaika; nami nisemaje? Baba, uniokoe katika saa hii? Lakini ni kwa ajili ya hayo nilivyoifikia saa hii. Baba, ulitukuze jina lako.
Basi ikaja sauti kutoka mbinguni, Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena. Basi mkutano uliosimama karibu wakasikia, walisema ya kwamba kumekuwa ngurumo; wengine walisema, Malaika amesema naye. Yesu akajibu, akasema, Sauti hiyo haikuwako kwa ajili yangu, bali kwa ajili yenu. Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje. Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu. Aliyanena hayo akionesha ni mauti gani atakayokufa.

TAFAKARI:
KIFO CHA YESU KIMETUWEKA HURU KUTOKA DHAMBI: Tunapoanza kukaribia mwisho wa kipindi cha Kwaresima, Kanisa linataka sisi tukaze macho yetu juu ya mafumbo ya mateso na kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo. Yesu katika Injili anajilinganisha na punje ya ngano ambayo ni baada tu ya kufa ardhini ndipo huweza kuzaa matunda. Kwa kifo cha Yesu, mwanadamu alipata uzima kwa kukombolewa kutoka katika mamlaka ya Shetani. Hivyo, kifo cha Yesu ni ishara ya baraka na matumaini mapya kwa ulimwengu mzima.
Katika somo la kwanza, nabii Yeremia anatufungulia tumaini jipya kwa kutangaza nyakati za matumaini ambapo Mwenyezi Mungu ataweka agano jipya na watu wake. Ni agano jipya atakalolitafanya katika Mlima wa Kalvari litakalokamilisha agano la kwanza la mlimani Sinai. Haya yote yatawezeshwa kwa nguvu ya kifo cha Yesu. Yesu ambaye alikufa na kufufuka na kutoa matunda kama punje ya ngano ndiye tumaini letu leo. Mungu alimtoa Mwanae msalabani ili katika msalaba watu wote waweze kupata tumaini jipya. Sisi tunaalikwa kukumbatia mateso ya Bwana wetu Yesu Kristo kwa kuyakubali mateso yetu wenyewe na ya wenzetu.
Katika Injili yetu ya leo, baadhi ya Wagiriki wanamfuata Filipo na kumwomba kumwona Yesu. Yesu anaposikia habari za Wagiriki hawa, mara moja anatangaza kwamba “Muda umefika wa Mwana wa Mtu kutukuzwa.” Muda wa kutukuzwa ni muda wa ufunuo, muda wa msalaba, kujaribiwa na kutoa ukombozi. Yesu anatumia picha ya punje ya ngano kuelezea kwa ufasaha kuhusu nguvu ya kifo chake. Anasema kwamba ili punje ya ngano iweze kuchipua na kutoa mazao, yabidi ife kwanza. Isipofanya hivyo, itabaki kuwa punje ya ngano. Pale inapokufa kwa kuoteshwa katika udongo, na kupata maji, hali nzuri ya hewa na kupaliliwa, huzaa matunda na kuleta faida zaidi. Yesu anatumia mfano huu kuelezea kifo chake. Kifo chake ndicho kitakachoiletea dunia faida kwa kumkomboa mwanadamu katika shimo la dhambi. Sisi nasi tunapaswa kuwa tayari kujitolea nafsi zetu na kuwafanya wenzetu kuwa karibu zaidi na Mungu. Bila majitoleo, hakika tutabakia hivi hivi. Ubinafsi utatufanya tubakie punje tu (punje moja tu); lakini tukiwa tayari kufa kwa kuyatoa maisha yetu tukiwahudumia wenzetu, hakika tutawaletea wengi baraka nyingi sana na Mungu atatukuzwa, nasi tutapata utakatifu. Pia yatupasa kuonesha utayari wa kufa katika vilema vyetu ili tufufuke katika utu mpya. Tuangamize utu wa kale kwa kuuzika ardhini (kuacha dhambi zetu) na kuchipua kwa kuanza maisha mapya.
Liturujia yetu leo inatukumbusha pia kuhusu mwaliko wetu wa kutambua huruma ya Mungu. Yafaa tujifunze kutumia vyema huruma ya Mungu. Tupendelee kuipokea sakramenti ya Kitubio. Kwaresima ni muda wa wongofu, ni muda wa kuanza maisha mapya katika Kristo, ambaye alipokea msalaba kama ishara kamili ya kutukomboa katika utuMwa

SALA: Ee Mungu wa huruma, tunakuomba utusaidie tuweze kuishi katika mapendo yale ambayo yalimfanya Mwanao afe kwa ajili yetu sisi.