MACHI 20, 2021; JUMAMOSI: JUMA LA 4 LA KWARESIMA

Urujuani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Yer 11: 18-20
Bwana akanijulisha haya, nami nikayajua; ndipo uliponionesha matendo yao. Lakini mimi nalikuwa kama mwana-kondoo mpole, achukuliwaye kwenda kuchinjwa wala sikujua ya kuwa wamefanya mashauri kinyume changu, wakisema, Na tuuharibu mti pamoja na matunda yake, na tumkatilie mbali atoke katika nchi ya walio hai, ili jina lake lisikumbukwe tena. Lakini, Ee Bwana wa majeshi, uhukumuye haki ujaribuye viuno na moyo, nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 7:1-2, 8-12

 1. Bwana, Mungu wangu, nimekukimbilia Wewe,
  Uniokoe na wote wanaonifuatia, uniponye.
  Asije akaipapura nafsi yangu kama simba,
  Akiivunja vunja pasipokuwa na wa kuponya.
  (K) Bwana, Mungu wangu, nimekukimbilia Wewe.
 2. Bwana, unihukumu mimi,
  Kwa kadiri ya haki yangu,
  Sawasawa na unyofu nilio nao.
  Ubaya wao wasio haki na ukome,
  Lakini mthibitishie mwenye haki. (K)
 3. Ngao yangu ina Mungu,
  Awaokoaye wanyofu wa moyo.
  Mungu ni mwamuzi mwenye haki,
  Naam, Mungu aghadhibikaye kila siku. (K)

INJILI: Yn 7: 40-52
Wengine katika mkutano walipoyasikia maneno ya Yesu, walisema, Hakika huyu ndiye nabii yule. Wengine walisema, Huyu ndiye Kristo. Wengine wakasema, Je! Kristo atoka Galilaya? Andiko halikusema ya kwamba Kristo atoka katika uzao wa Daudi, na kutoka Bethlehemu, mji ule alioukaa Daudi? Basi kukaingia matengano katika mkutano kwa ajili yake. Baadhi yao wakataka kumkamata, lakini hakuna mtu aliyenyosha mikono yake ili kumshika. Basi wale watumishi wakawaendea wakuu wa makuhani na Mafarisayo. Nao wakawaambia, Mbona hamkumleta? Wale watumishi wakajibu, Hajanena kamwe mtu ye yote kama huyu anavyonena. Basi Mafarisayo wakawajibu, Je! ninyi nanyi mmedanganyika? Ni nani katika wakuu amwaminiye, au katika Mafarisayo? Lakini makutano hawa wasioifahamu torati wamelaaniwa. Akawaambia Nikodemo, (naye ni yule aliyemwendea zamani, maana ni mmoja wao), Je! Torati yetu humhukumu mtu kabla ya kumsikia kwanza, na kujua atendavyo? Wakajibu, wakamwambia, Je! Wewe nawe umetoka Galilaya! Tafuta, ukaone ya kuwa kutoka Galilaya hakutokea nabii.

TAFAKARI:
TUKUBALI KUWAJIBISHWA: Wakuu wa makuhani na Mafarisayo kama tulivyosikia katika Injili, waliwalaumu wale watumishi kwamba hawajatimiza majukumu yao wakiwauliza, “Mbona hamkumleta?” Yanapotokea mabishano kutokana na jambo fulani, kila mtu husema lake. Inakuwa ni makelele, kila mmoja atamlaumu na kumnyooshea kidole mwingine akilalamika, “Oh fulani ndiyo kazembea!” Hakuna anayekubali kupokea jukumu la kuwajibishwa, kila mmoja anakwepa, anasukumia mpira kwa mwenzake. Ndiyo maana hata wale walioleta habari za Yesu naye wanarushiwa lawama. Hata sisi mara nyingi katika maisha yetu tunapenda kuwarushia wengine lawama huku tukijiona wenyewe tuko sahihi na wenzetu ndiyo waliokosea.

SALA: Bwana tujalie neema ya kutowalaumu wengine hasa pale ambapo nasi tumekosea.