MACHI 19, 2021; IJUMAA: JUMA LA 4 LA KWARESIMA

MTAKATIFU YOSEFU, MUME WA BIKIRA MARIA Sherehe
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO 1: 2 Sam 7:4-5, 12-14, 16
Ikawa usiku huo huo, neno la Bwana likamfikia Nathani kusema, Enenda, ukamwambie mtumishi wangu, Daudi, Bwana asema hivi, Siku zako zitakapotimia, ukalala na baba zako, nitainua mzao wako nyuma yako, atakayetoka viunoni mwako, nami nitaufanya imara ufalme wake. Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha ufalme wake nitakifanya imara milele. Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu, akitenda maovu nitamwadhibu kwa fimbo ya binadamu na kwa mapigo ya wanadamu Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 89:1-4, 26, 28

 1. Fadhili za Bwana nitaziimba milele;
  Kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako.
  Maana nimesema, Fadhili zitajengwa milele;
  Katika mbingu utauthibitisha uaminifu wako
  (K) Wazao wake watadumu milele.
 2. Nimefanya agano na mteule wangu,
  Nimemwapia Daudi, mtumishi wangu.
  Wazao wako nitawafanya imara milele,
  Nitakijenga kiti chako cha enzi hata milele. (K)
 3. Yeye ataniita, Wewe baba yangu,
  Mungu wangu na mwamba wa wokovu wangu.
  Hata milele nitamwekea fadhili zangu,
  Na agano langu litafanyika amini kwake. (K)

SOMO 2: Rum 4:13, 16-18, 22
Ahadi ile ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Ibrahimu na uzao wake, si kwa sheria bali kwa haki aliyohesabiwa kwa imani. Kwa hiyo ilitoka katika imani, iwe njia ya neema, ili kwamba ile ahadi iwe imara kwa wazao wote; si kwa wale wa Torati tu, ila kwa wale wa imani ya Ibrahim; aliye baba yetu sisi sote; (kama ilivyoandikwa nimekuweka kuwa baba wa mataifa mengi). Mbele zake yeye aliyemwamini, yaani Mungu, mwenye kuwahuisha wafu, ayatajaye yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako. Naye aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ili apate kuwa baba wa mataifa mengi, kama ilivyonenwa, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako. Kwa hiyo ilihesabiwa kwake kuwa ni haki.

INJILI: Mt 1:16, 18-21, 24
Yakobo alimzaa Yusufu mumewe Mariamu aliyemzaa Yesu aitwaye Kristo. Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri. Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao. Naye Yusufu alipoamka katika usingizi, alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza; akamchukua mkewe.

TAFAKARI:
FAMILIA NI NGUZO IMARA YA KANISA: Leo Kanisa kwa namna ya pekee linamheshimu Yosefu mume wa Bikira Maria. Tunaelezwa kuwa walipokuwa katika uchumba ndipo Bikira Maria kwa mpango wa Mungu alimchukua mimba Yesu (Mungu nafsi ya pili). Fundisho kubwa tunalojifunza toka kwa Yosefu ni moyo wa usikivu. Malaika alipomweleza wala hakubisha. Leo hii vijana wengi na familia nyingi ziko kwenye magomvi yasiyokoma kwa sababu zimekosa usikivu. Kijana anaamua hivi, mke wake anaamua vile, kila mmoja anapoamua kivyake. Vijana wengi leo hawachumbii, wamesahau kuwa uchumba ni kipindi kitakatifu cha kuhabarishana namna na mfumo wa maisha watakayoendea. Leo hii kijana anakutana na msichana Jumatatu na ndani ya wiki wameshaanza kuishi pamoja bila hata wazazi wa pande zote kufahamu. Hawajali ndoa. Tujifunze kwa Mtakatifu Yosefu kusema, “kabla hawajakaribiana” ina maana wakati wa uchumba wao, yaani kabla hawajaanza kuishi pamoja.

SALA: Ee Mtakatifu Yosefu tunaomba uziombee familia zetu ziweze kuishi maisha yenye usikivu. Wewe uliye msimamizi wa Kanisa utuombee.