MACHI 18, 2021; ALHAMISI: JUMA LA 4 LA KWARESIMA

Mt. Sirili wa Yerusalemu, Askofu na Mwalimu wa Kanisa
Urujuani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Kut 32:7-14
Bwana akamwambia Musa, Haya! Shuka; kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao, wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia ndama ya kuyeyusha, wakaiabudu na kuitolea dhabihu, wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri. Tena Bwana akamwambia Musa, Mimi nimewaona watu hawa, na tazama, ni watu wenye shingo ngumu; basi sasa niache, ili hasira zangu ziwake juu yao, niwaangamize; nami nitakufanya wewe uwe taifa kuu. Musa akamsihi sana Bwana, Mungu wake, na kusema, Bwana, kwa nini hasira zako kuwaka juu ya watu wako uliowaleta kutoka nchi ya Misri kwa uweza mkuu, na kwa mkono wenye nguvu? Kwa nini Wamisri kunena, wakisema, Amewatoa kwa kuwatenda uovu, ili apate kuwaua milimani, na kuwaondoa watoke juu ya uso wa nchi? Geuka katika hasira yako kali, ughairi uovu huu ulio nao juu ya watu wako. Mkumbuke Ibrahimu, na Isaka na Israeli, watumishi wako, ambao uliwaapia kwa nafsi yako, na kuwaambia, nitazidisha kizazi chenu mfano wa nyota za mbinguni; tena nchi hii yote niliyoinena nitakipa kizazi chenu, nao watairithi milele. Na Bwana akaughairi ule uovu aliosema ya kwamba atawatenda watu wake.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 106:19-23

  1. Walifanya ndama huko Horebu,
    Wakaisujudia sanamu ya kuyeyusha
    Wakaubadili utukufu wao
    Kuwa mfano wa ng’ombe mla majani.
    (K)Ee Bwana unikumbuke mimi,
    Kwa kibali uliyo nayo kwa watu wako.
  2. Matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu,
    Mambo ya kutisha penye bahari ya Shamu.
    Wakamsahau Mungu, mwokozi wao,
    Aliyetenda makuu katika Misri. (K)
  3. Akasema ya kuwa atawaangamiza,
    Kama Musa, mteule wake, asingalisimama,
    Mbele zake kama mahali palipobomoka,
    Ili aigeuze hasira yake asije akawaharibu. (K)

INJILI: Yn 5:31-47
Yesu aliwaambia Wayahudi: Mimi nikijishuhudia mwenyewe, ushuhuda wangu si kweli. Yuko mwingine anayeshuhudia; nami najua ya kuwa ushuhuda wake anaonishuhudia ni kweli. Ninyi mlituma watu kwa Yohane, naye akaishuhudia kweli. Lakini mimi siupokei ushuhuda kwa wanadamu; walakini ninasema haya ili ninyi mpate kuokoka. Yeye alikuwa taa iwakayo na kung’aa, nanyi mlipenda kuishangalia nuru yake kwa muda.
Lakini ushuhuda nilio nao mimi ni mkubwa kuliko ule wa Yohane; kwa kuwa zile kazi alizonipa Baba ili nizimalize, kazi hizo zenyewe ninazozitenda, zanishuhudia ya kwamba Baba amenituma. Naye Baba aliyenipeleka amenishuhudia. Sauti yake hamkuisikia wakati wo wote, wala sura yake hamkuiona. Wala neno lake hamnalo likikaa ndani yenu, kwa kuwa ninyi hammwamini yule aliyetumwa na yeye.
Mwayachunguza maandiko, kwa sababu mnadhani kwamba ninyi mna uzima wa milele ndani yake; na hayo ndiyo yanayonishuhudia. Wala hamtaki kuja kwangu mpate kuwa na uzima. Mimi siupokei utukufu kwa wanadamu Walakini nimewajua ninyi ya kuwa hamna upendo wa Mungu ndani yenu. Mimi nimekuja kwa jina la Baba yangu, wala ninyi hamnipokei; mwingine akija kwa jina lake mwenyewe, mtampokea huyo.
Mwawezaje kuamini ninyi mnaopokeana utukufu ninyi kwa ninyi, na utukufu ule utokao kwa Mungu aliye wa pekee hamwutafuti? Msidhani kwamba mimi nitawashitaki kwa Baba; yuko anayewashitaki, ndiye Musa, mnayemtumaini ninyi. Kwa maana kama mngalimwamini Musa, mngeniamini mimi; kwa sababu yeye aliandika habari zangu. Lakini msipoyaamini maandiko yake, mtayaamini wapi maneno yangu?

TAFAKARI:
KUMRIDHISHA MWANADAMU KUNAHITAJI JITIHADA KUBWA: Yuko mwanasaikolojia aliyesema, “Mwanadamu saa zote huuliza maswali, hata kichwa chake kimeundwa kwa mfumo wa alama ya kuuliza”, yaani kina kisogo kinachokifanya kifanane na alama hii “?” . Yaani kichwa kiko kama kinauliza, “kwa nini?” Yesu anapowaambia Wayahudi kuwa wanayachunguza Maandiko ili kutafuta uzima wa milele ni dhahiri kuwa binadamu kila mara ni mchunguzi, haridhiki. Ukimweleza jambo bado atatafuta mahali pengine ili ajiridhishe, asikie tena au afanye mlinganisho. Linapokuja swala la kiimani ambalo haliwezi kuthibitishwa kwa namna za kuridhisha za kibinadamu basi ndio kabisa swala hilo halitapewa nafasi ya kukubalika. Wayahudi walitaka wapate uhakika wa Maandiko lakini kwa kutumia namna yao ya kufikiri.

SALA: Ee Yesu, tujalie neema ya kukubaliana na mafunuo yako.