MACHI 17, 2021; JUMATANO: JUMA LA 4 LA KWARESIMA

Patrisi, Askofu
Urujuani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Isa 49: 8-15
Bwana asema hivi, Wakati uliokubalika nimekujibu, na siku ya wokovu nimekusaidia; nami nitakuhifadhi, nitakutoa uwe agano la watu hawa, ili kuiinua nchi hii, na kuwaridhisha urithi uliokuwa ukiwa; kuwaambia waliofungwa, Haya, tokeni; na hao walio katika giza, Jionesheni. Watajilisha katika njia, na juu ya majabali watapata malisho. Hawataona njaa, wala hawataona kiu; hari haitawapiga, wala jua; kwa maana yeye aliyewarehemu atawatangulia, naam, karibu na chemchemi za maji atawaongoza. Nami nitafanya milima yangu yote kuwa njia, na njia kuu zangu zitatukuzwa zote. Tazama, hawa watakuja kutoka mbali; na tazama, hawa kutoka kaskazini, na kutoka magharibi, na hawa kutoka nchi ya Sinimu. Imbeni, enyi mbingu; ufurahi, Ee nchi; pazeni sauti ya kuimba, enyi milima; kwa kuwa Bwana amewafariji watu wake, naye atawahurumia watu wake walioteswa. Bali Sioni alisema, Mungu ameniacha, Bwana amenisahau. Je! Mwanamke aweza kumsahau mtoto wake amnyonyaye, hata asimhurumie mwana wa tumbo lake? Naam, hawa waweza kusahau, lakini mimi sitakusahau wewe.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 145:8-9, 13-14, 17-18

 1. Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma,
  Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema.
  Bwana ni mwema kwa watu wote,
  Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote.
  (K) Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma.
 2. Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
  Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote.
  Bwana huwategemeza wote waangukao,
  Huwainua wote walioinamia chini. (K)
 3. Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote,
  Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote.
  Bwana yu karibu na wote wamwitao,
  Wote wamwitao kwa uaminifu. (K)

INJILI: Yn 5: 17-30
Yesu aliwajibu Wayahudi: Baba yangu anatenda kazi hata sasa, nami ninatenda kazi. Basi kwa sababu hiyo Wayahudi walizidi kutaka kumwua, kwa kuwa hakuivunja Sabato tu, bali pamoja na hayo alimwita Mungu Baba yake, akijifanya sawa na Mungu. Basi Yesu akajibu, akawaambia, Amin, amin, nawaambia, mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vilevile. Kwa kuwa Baba ampenda Mwana, naye humwonesha yote ayatendayo mwenyewe; hata na kazi kubwa zaidi kuliko hizi atamwonesha, ili ninyi mpate kustajaabu. Maana kama Baba awafufuavyo wafu na kuwahuisha, vivyo hivyo na Mwana awahuisha wale awatakao. Tena Baba hamhukumu mtu ye yote, bali amempa Mwana hukumu yote, ili watu wote wamheshimu Mwana kama vile wanavyomheshimu Baba. Asiyemheshimu Mwana hamheshimu Baba aliyempeleka. Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani. Amin, amin, nawaambia, Saa inakuja, na sasa ipo, wafu watakapoisikia sauti ya Mwana wa Mungu, na wale waisikiao watakuwa hai. Maana kama vile Baba alivyo na uzima nafsini mwake, vivyo hivyo alimpa na Mwana kuwa na uzima nafsini mwake. Naye akampa amri ya kufanya hukumu kwa sababu ni Mwana wa Adamu Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake. Nao watatoka; wale waliofanya mema kwa ufufuo wa uzima, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu. Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe; kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo; na hukumu yangu ni ya haki, kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mimi, bali mapenzi yake aliyenipeleka.

TAFAKARI:
KUTENDA WEMA NDANI YA JAMII ILIYOJAA UOVU LAZIMA UTAPINGWA: Katika utume aliofanya Yesu alikumbana na vikwazo vingi toka kwa wale wale waliokusudiwa. Upinzani huu ulitokana hasa na jamii ile kuelezwa ukweli wao ambao uliwauma na kuwaumiza. Hata leo hii, wapo wengi wanaopingana na utume alioachiwa mama Kanisa. Padri aweza kuwa kiongozi mzuri tu wa kuelekeza watu kiimani, lakini ikitokea kuna kosa kafanya na likajulikana, hilo ndilo litakalobebwa na kuenezwa kwa nguvu zote na hivyo kufifisha utume wake. Tunaona Yesu anapingwa vikali eti “kwa kumwita Mungu Baba yetu” na hivi wanapanga kumuua. Wengi kwa njia za namna hii hii wameua na kufifisha utume wa Kanisa.

SALA: Tunaomba Baba utusamehe pale tulipofifisha utume wa Kanisa.