MACHI 16, 2021; JUMANNE: JUMA LA 4 LA KWARESIMA

Urujuani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Eze 47: 1– 9, 12
Malaika alinileta mpaka lango la nyumba; na tazama, maji yalitoka chini ya kizingiti cha nyumba, kwa njia ya mashariki, maana upande wa mbele wa nyumba ulielekea upande wa mashariki; nayo maji yakashuka toka chini ya upande wa kuume wa nyumba, upande wa kusini wa madhabahu. Ndipo akanileta nje kwa njia ya lango upande wa kaskazini, akanizungusha kwa njia ya nje mpaka lango la nje, kwa njia yake iliyoelekea mashariki; na tazama, maji yalitoka upande wa kuume. Na alipotoka mtu yule, mwenye uzi wa kupima mkononi mwake, kwenda mashariki, akapima dhiraha elfu, akanivusha maji yale; maji yakafika mpaka viweko vya miguu. Kisha akapima dhiraha elfu, akanivusha maji yale, maji yakafika mpaka magoti. Kisha akapima dhiraha elfu, akanivusha, maji yakafika mpaka viuno. Kisha akapima dhiraha elfu, yakawa mto nisioweza kuuvuka; maana maji yamezidi, maji ya kuogelea, mto usiovukika. Akaniambia, mwanadamu, je! Umeona haya? Kisha akanichukua, akanirudisha mpaka ukingo wa mto. Basi nikiisha kurudi, tazama, kando ya ukingo wa mto ilikuwapo miti mingi sana, upande huu na upande huu. Ndipo akaniambia, Maji haya yanatoka kwenda pande za nchi ya mashariki, nayo yanashuka mpaka Araba, na kuingia katika bahari; maji yatokezwayo yataingia baharini, na maji yake yataponyeka. Tena itakuwa kila kiumbe hai kisongamanacho, kila mahali itakapofika mito hiyo, kitaishi; kutakuwapo wingi mkubwa wa samaki, kwa sababu maji haya yamefika huko; maana maji yale yataponyeka, na kila kitu kitaishi po pote utakapofikilia mto huo. Na karibu na mto, juu ya ukingo wake, upande huu na upande huu, utamea kila mti wa chakula, ambayo majani yake hayatanyauka, wala matunda yake hayatatindika kamwe; utatoa matunda mapya kila mwezi, kwa sababu maji yake yanatoka mahali patakatifu; na matunda yake yatakuwa ni chakula; na majani yake yatakuwa ni dawa.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 46:1-2, 4-5, 7-8

 1. Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu,
  Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.
  Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi,
  Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari.
  (K) Bwana wa majeshi yu pamoja nasi,
  Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.
 2. Kuna mto, vijito vyake vyaufurahisha mji wa Mungu,
  Patakatifu pa maskani zake Aliye juu.
  Mungu yu katikati yake hautatetemeshwa;
  Mungu atausaidia asubuhi na mapema. (K)
 3. Bwana wa majeshi yu pamoja nasi,
  Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.
  Njoni myatazame matendo ya Bwana,
  Jinsi alivyofanya ukiwa katika nchi. (K)

INJILI: Yn 5: 1-3, 5-16
Baada ya hayo palikuwa na sikukuu ya Wayahudi; naye Yesu akakwea kwenda Yerusalemu. Na huko Yerusalemu penye mlango wa kondoo pana birika, iitwayo kwa Kiebrania Bethzatha, nayo ina matao matano.Ndani ya hayo jamii kubwa ya wagonjwa walikuwa wamelala, vipofu, viwete, nao waliopooza. Na hapa palikuwa na mtu, ambaye amekuwa hawezi muda wa miaka thelathini na minane. Yesu alipomwona huyu amelala, naye akijua ya kuwa amekuwa hali hiyo siku nyingi, alimwambia, Wataka kuwa mzima? Yule mgonjwa akamjibu, Bwana, mimi sina mtu wa kunitia birikani, maji yanapotibuliwa; ila wakati ninapokuja mimi, mtu mwingine hushuka mbele yangu. Yesu akamwambia, Simama, jitwike godoro lako, uende. Mara yule mtu akawa mzima, akajitwika godoro lake, akaenda. Nayo ilikuwa ni Sabato siku hiyo. Kwa sababu hiyo Wayahudi wakamwambia yule aliyeponywa, Leo ni Sabato, wala si halali kwako kujitwika godoro. Akawajibu, Yeye aliyenifanya kuwa mzima ndiye aliyeniambia, Jitwike godoro lako, uende. Basi wakamwuliza, Yule aliyekuambia, Jitwike, uende, ni nani? Lakini yule mtu aliyeponywa hakumjua ni nani; maana Yesu alikuwa amejitenga, kwa sababu palikuwa na watu wengi mahali pale. Baada ya hayo Yesu akamkuta ndani ya hekalu, akamwambia, Angalia, umekuwa mzima; usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi. Yule mtu akaenda zake, akawapasha habari Wayahudi ya kwamba ni Yesu aliyemfanya kuwa mzima. Kwa sababu hiyo Wayahudi wakamwudhi Yesu, kwa kuwa alitenda hayo siku ya Sabato.

TAFAKARI:
TUWE WATU WA KUJALI WENGINE: Ukitafakari kwa kina katika maisha mara nyingi tunajijali sisi wenywe, hatuoni hitaji la wengine. Mhusika tunayeelezwa katika Injili ya leo alihitaji msaada wa wengine waliokuwa wazima kumsaidia kupata kupona kwa kutupwa katika birika. Tunaambiwa hakuna aliyemjali, baadhi walikuwa wakimwangalia tu na wengine walikuwa wanapita tu pembeni na hata wakirudi walikuwa wanamwacha tu. Ni mpaka Yesu alipofika na kumwuliza akamponya. Na kitu cha kushangaza zaidi hata baada ya Yesu kumponya, wanaokutana naye akiwa mzima badala ya kufurahi kuwa kapona, wanamuongezea maumivu kwa kujifanya kufahamu sheria, “Leo ni Sabato mbona wajitwika godoro?” Kumbe, tuko watu ambao hatufurahii maendeleo ya wengine wala furaha zao. Tunataka wabaki katika hali ya uduni. Kwa kweli tunaombea wabaki katika udhaifu ambao utatufurahisha sisi. Lakini fikra za namna hii ni balaa kubwa mno.

SALA: Ee Yesu, tujalie kuwaonea wengine huruma na kuwasaidia hasa wale tunaokutana nao katika maisha yetu ya kila siku.