MACHI 14, 2021; DOMINIKA: DOMINIKA YA 4 YA KWARESIMA

Urujuani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: 2Nya. 36 :14-16, 19-23
Wakuu wote wa makuhani, na watu, wakakosa mno sawasawa na machukizo yote ya mataifa; wakainajisi nyumba ya Bwana aliyoitakasa katika Yerusalemu. Naye Bwana, Mungu wa baba zao, akatuma kwao kwa mikono ya wajumbe wake, akiondoka mapema, na kutuma; kwa sababu aliwahurumia watu wake, na makao yake; lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mungu, na kuyadharau maneno yake; na kuwacheka manabii wake, hata ilipozidi ghadhabu ya Bwana juu ya watu wake, hata kusiwe na kuponya.
Wakaiteketeza nyumba ya Mungu, wakaubomoa ukuta wa Yerusalemu, wakayateketeza kwa moto majumba yake yote, wakaviharibu vyombo vyake vyote vya thamani. Na wale waliookoka na upanga akawachukua mpaka Babiloni; wakamtumikia yeye na wanawe hata kulipoingia milki ya Uajemi; ili kulitimiza neno la Bwana kwa kinywa cha Yeremia, hata nchi itakapofurahia Sabato zake; kwa maana siku zote ilipokaa ukiwa ilishika Sabato, kutimiza miaka sabini.
Ikawa katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, ili kwamba neno la Bwana alilolisema kwa kinywa cha Yeremia lipate kutimizwa, Bwana akamwamsha roho yake Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata akapiga mbiu katika ufalme wake wote, akaiandika pia, akisema, Koreshi, mfalme wa Uajemi asema hivi; Bwana, Mungu wa mbinguni, amenipa falme zote za dunia; naye ameniagiza nimjengee nyumba katika Yerusalemu, ulioko Yuda. Basi kila mtu katika ninyi nyote mlio watu wake, Bwana, Mungu wake, na awe pamoja naye, na akwee.

WIMBO WA KATIKATI: Zab 137: 1-6

 1. Kando ya mito ya Babiloni ndiko tulipoketi,
  Tukalia tulipoikumbuka Sioni.
  Katika miti iliyo katikati yake
  Tulivitundika vinubi vyetu.
  (K) Ulimi wangu na ugandamane Na kaakaa la kinywa changu, nisipokumbuka.
 2. Maana huko waliotuchukua mateka
  Walitaka tuwaimbie;
  Na waliotuonea walitaka furaha;
  Tuimbeni baadhi ya nyimbo za Sioni.(K)
 3. Tuuimbeje wimbo wa Bwana
  Katika nchi ya ugeni?
  Ee Yerusalemu,nikikusahau wewe,
  Mkono wangu wa kuume na usahau. (K)
 4. Ulimi wangu ugandamane
  Na kaakaa la kinywa changu, nisipokukumbuka.
  Nisipoikuza Yerusalemu
  Zaidi ya furaha yangu iliyo kuu. (K)

SOMO 2: Efe 2 :4-10
Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda: hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani, mmeokolewa kwa neema. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu; ili katika zamani zinazokuja audhihirishe wingi wa neema yake upitao kiasi kwa wema wake kwetu sisi katika Kristo Yesu. Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu. Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo.

SHANGILIO: Yn 3:16
Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanae wa pekee, ili kila mtu amwaminiye awe na uzima wa milele.

INJILI: Yn 3 :14-21
Yesu alimwambia Nikodemo: Kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyo hivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa; ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye.
Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu.
Na hili ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika Mungu.

TAFAKARI:
BABA ALIMTUMA MWANAE WA PEKEE ILI ULIMWENGU USIPOTEE: Kipindi cha Kwaresima ni kipindi cha kuchunguza hali yetu ya dhambi na kumrudia Mwenyezi Mungu, kwa kufanya mapinduzi makubwa ya kiroho. Maneno ya Injili ya Yohane leo, “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanae wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele” (Yn 3:16), yanapaswa kututia hamasa ya kuacha kiburi chetu na kuukaribisha upendo wa Kristo. Aya hii ya Injili umebeba muhtasari wote juu ya upendo wa Baba na Kristo kwetu. Kwanza kabisa unatueleza kwamba Baba wa mbinguni anatupenda kwa upendo usio na kikomo. Upendo wake kwetu ni kamili. Pili, upendo wa Mungu ulidhihirishwa kwa njia ya Mwanae wa pekee. Mwana ni mrithi wa yote aliyonayo Baba (Ebr 1:2); naye Mwana, yaani Kristo, amekuwa tayari kutushirikisha na kutupatia yote, amekubali hata kuyatoa maisha yake kwa ajili yetu.
Tatu, sisi tunapaswa kumwamini Mwana kwa kumpa maisha yetu kama zawadi. Tuikubali nguvu ya Mwana ituingie na kuyabadili maisha yetu. Hii ndiyo zawadi kubwa tuwezayo kumpatia Mwana kwa kipindi chetu cha Kwaresima. Matokeo ya kumpokea Yeye na kumpa maisha yetu kama zawadi ni kuupata ukombozi. Hatutaangamia kwa dhambi zetu bali tutapokea uzima wa milele. Hakuna njia nyingine ya wokovu isipokuwa kwa njia ya Mwana. Tunapaswa kukumbatia ukweli huu.
Teresa wa Mtoto Yesu alichunguza daima mwenendo wa maisha yake na daima aliogopa kumkosea Mungu. Na katika maandishi yake amesema, “Yesu hana haja na kazi zetu, anachohitaji ni upendo wetu.” Ujumbe huu uliangaza moyo wake uliojeruhiwa na kumjaza amani. Akiwa mtoto mdogo, aliyakabidhi kwa Mungu maisha yake na kutegemea huruma yake. Mtume Paulo analiweka hili vizuri anaposema, “Kwa neema ya Mungu, yaani tumekombolewa kwa imani, na siyo kwa nguvu zetu wenyewe bali kwa zawadi ya Mungu” (Efe 2 :6-8).
Tukiwa katika safari yetu ya imani katika kipindi hiki cha Kwaresima, yafaa tutafakari juu ya wema wa Mungu na utayari wake wa kumtoa Mwanae wa pekee kwa ajili yetu. Hakika ameonesha upendo mkubwa wa kutaka kutukomboa sisi. Mimi na wewe tukaribishe na kutamani upendo huu! Kama mtakatifu Teresa, tutamani kujiweka katika mikono ya Mungu anayetupenda na pia tukubali maisha yetu yalete wokovu kwa wengine.

SALA: Ee Bwana, ninajitoa kwako kwa moyo wangu wote, waangalie watu wako kwa huruma, kwani sisi tumegawanyika katika njia mbalimbali, na tukirimie Roho wako atufanye sisi tuwe kitu kimoja katika upendo.