MACHI 13, 2021; JUMAMOSI: JUMA LA 3 LA KWARESIMA

Urujuani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Hos 5:15-6:6
Bwana asema: katika taabu yao watanitafuta kwa bidii: Njoni, tumrudie Bwana; maana yeye amerarua, na yeye atatuponya; yeye amepiga, na yeye atatufunga jeraha zetu. Baada ya siku mbili atatufufua; siku ya tatu atatuinua, nasi tutaishi mbele zake. Nasi na tujue, naam, tukaendelee kumjua Bwana; kutokea kwake ni yakini kama asubuhi; naye atatujilia kama mvua, kama mvua ya vuli iinyweshayo nchi. Ee Efrahimu, nikutendee nini? Ee Yuda, nikutendee nini? Kwa maana fadhili zenu ni kama wingu la asubuhi na kama umande utowekao mapema. Kwa sababu hiyo, nimewakata-kata kwa vinywa vya manabii; nimewaua kwa maneno ya kinywa changu; na hukumu yangu itatokea kama mwanga. Maana nataka fadhili wala si sadaka; na kumjua Mungu kuliko sadaka za kuteketezwa.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 51:1-2, 16-19

 1. Ee Mungu, unirehemu,
  Sawasawa na fadhili zako.
  Kiasi cha wingi wa rehema zako,
  Uyafute makosa yangu.
  Unioshe kabisa na uovu wangu,
  Unitakase dhambi zangu.
  (K) Ninavyotaka ni fadhili, si sadaka.
 2. Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa,
  Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika;
  Moyo uliovunjika na kupondeka,
  Ee Mungu, hutaudharau. (K)
 3. Uitendee mema Sayuni kwa radhi yako,
  Uzijenge kuta za Yerusalemu.
  Ndipo utakapopendezwa na dhabihu za haki,
  Na sadaka za kuteketezwa, na kafara (K)

INJILI: Lk 18:9-14
Yesu aliwaambia mfano huu watu waliojikinai ya kuwa wao ni wenye haki, wakiwadharau wengine wote. Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang`anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; Hutoa zaka katika mapato yangu yote. lakini yule mtoza ushuru alisisima mbali, wala hakudhubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipigapiga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhilie atakwezwa.

TAFAKARI:
NI VIGUMU MWANADAMU KUJIJUA ALIVYO
Ni mara nyingi katika maisha inakuwa rahisi mtu kuona kosa au udhaifu wa mwingine na hivyo kuwa mwepesi wa kutoa hukumu. Wengi tunaishi maisha ya ‘Kifarisayo’. Tunasema, “Oh, fulani ni mlevi, mhuni, mchafu, mzembe, mwongo” na kadhalika. Lakini kuna usemi usemao, “Nyani halioni kundule ila huona la mwenzie.” Tu wepesi wa kunyooshea wengine kidole tunasahau kuwa tunaponyoosha kidole kwa mwingine, vitatu vinatuelekea sisi wenyewe. Kwa maana nyingine ni kuwa, kama unayemnyooshea kidole ni mbaya kwa asilimia 10, basi unayenyoosha ni mara tatu zaidi yake (30%). Kristo anatutaka leo hii tuwe watu wa kujichunguza wenyewe na siyo kudandia lifti kwa kujiona wema kupitia migongo ya wengine. Tujipige kifua na kujikubali kuwa tu wadhambi na hatustahili.

SALA: Bwana tufundishe namna ya kusali.