MACHI 9, 2021; JUMANNE: JUMA LA 3 LA KWARESIMA

Mt. Fransiska wa Roma, Mtawa
Urujuani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: Dan 3:25, 34-43
Ndipo Azaria akasimama akasali hivi, akifumbua kinywa chake katikati ya moto na kusema: Usituache kabisa, kwa ajili ya jina lako, wala usilitangue agano lako na kutuondolea rehema zako, kwa ajili ya Ibrahimu umpendaye, na kwa ajili ya Isaka mtumishi wako, na Israeli mtakatifu wako, ambao uliwaahidia ya kuwa utauzidisha uzao wao kama nyota za mbinguni na kama mchanga uliopo pwani. Maana sisi, Ee Bwana, tumekuwa duni kuliko mataifa mengine yote, na kudhulumiwa leo katika ulimwengu wote kwa sababu ya dhambi zetu. Sasa hakuna mfalme wala nabii wala kiongozi; hakuna dhabihu wala kafara wala sadaka wala uvumba; wala mahali pa kukutolea dhabihu na kuona rehema. Lakini kwa moyo uliovunjika na kwa roho nyenyekevu tukubaliwe nawe, na sadaka yetu iwe machoni pako leo kama dhabihu za kondoo waume na ng’ombe, na kama kondoo wanono elfu kumi. Nasi tukufuate kwa unyofu, maana wanaokutumaini Wewe hawataaibika. Na sasa tunakufuata kwa moyo wote; tunakucha, na kuutafuta uso wako. Usitufedheheshe, bali ututendee kwa kadiri ya fadhili zako, sawa sawa na wingi wa huruma zako. Utuokoe kwa kadiri ya maajabu yako, na kulitukuza jina lako, Ee Bwana.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 25:4-9

 1. Ee Bwana unijulishe njia yako,
  Unifundishe mapito yako,
  Uniongoze katika kweli yako,
  Na kunifundisha.
  (K) Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako.
 2. Ee Bwana kumbuka rehema zako na fadhili zako,
  Maana zimekuwako tokea zamani.
  Usiyakumbuke makosa ya ujana wangu,
  Wala maasi yangu.
  Ee Bwana, kwa ajili ya wema wako. (K)
 3. Bwana yu mwema, mwenye adili,
  Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
  Wenye upole atawaongoza katika hukumu,
  Wenye upole atawafundisha njia yake. (K)

INJILI: Mt 18: 21-35
Petro alimwendea Yesu akamwambia, Bwana, ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe? hata mara saba? Yesu akamwambia, Sikuambii hata mara saba, bali hata saba mara sabini. Kwa sababu hii ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyetaka kufanya hesabu na watumwa wake. Alipoanza kuifanya, aliletewa mtu mmoja awiwaye talanta elfu kumi. Naye alipokosa cha kulipa, bwana wake akaamuru auzwe, yeye na mkewe na watoto wake, na vitu vyote alivyonavyo, ikalipwe ile deni. Basi yule mtumwa akaanguka, akamsujudia akisema, Bwana, nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Bwana wa mtumwa yule akamhurumia, akamfungua, akamsamehe ile deni. Mtumwa yule akatoka, akamwona mmoja wa wajoli wake, aliyemwia dinari mia; akamkamata, akamshika koo, akisema, Nilipe uwiwacho. Basi mjoli wake akaanguka miguuni pake, akamsihi, akisema, Nivumilie, nami nitakulipa yote pia. Lakini hakutaka, akaenda, akamtupa kifungoni, hata atakapoilipa ile deni. Basi wajoli wake walipoyaona yaliyotendeka, walisikitika sana, wakaenda wakamweleza bwana wao yote yaliyotendeka. Ndipo bwana wake akamwita, akamwambia, Ewe mtumwa mwovu, nalikusamehe wewe deni ile yote, uliponisihi; nawe je! haikukupasa kumrehemu mjoli wako, kama mimi nilivyokurehemu wewe? Bwana wake akaghadhibika, akampeleka kwa watesaji, hata atakapoilipa deni ile yote. Ndivyo na Baba yangu wa mbinguni atakavyowatenda ninyi, msiposamehe kwa mioyo yenu kila mtu ndugu yake.

TAFAKARI:
MAISHA YA MSAMAHA YANAHITAJI KUJISADAKA: Swali la Petro kwa Yesu, “Ndugu yangu anikose mara ngapi nami nimsamehe?” ingependeza lingekuwa swali la kila mmoja wetu. Katika mambo ambayo yanamwia magumu mwanadamu ni msamaha. Utasikia mtu anamwambia mwenzake, “Nimekusamehe lakini sitasahau.” Kiuhalisia hapa hapana msamaha. Msamaha unahitaji maandalizi na kujisadaka. Mara nyingi tunafikiri aliyekosea ndiye anayetakiwa aombe msamaha na kumbe hilo linamfanya aliyekosewa amsubiri aliyemkosea aje. Tunakosea. Msamaha mzuri ni ule unaotengenezwa na pande zote, kila mmoja akitakiwa kuchukua hatua ya kutafuta maridhiano. Kumbe, kila mmoja aone umuhimu wa kuishi kwa amani na uelewano na utulivu na mwenzake. Mazingira kama haya yatafanya maisha yawe mazuri, la sivyo visa na visasi vitadumu kati yetu.

SALA: Yesu mwema, utusamehe hasa pale tunaposhindwa kuwasamehe wengine.