MACHI 8, 2021; JUMATATU: JUMA LA 3 LA KWARESIMA

Mt. Yohane wa Mungu
Urujuani
Zaburi: Juma 1

SOMO 1: 2 Fal 5: 1-15
Naamani, jemadari wa jeshi la mfalme wa Shamu, alikuwa mtu mkubwa mbele ya bwana wake, na mwenye kuheshimiwa, kwa sababu kwa mkono wake Bwana alikuwa amewapa Washami kushinda; tena alikuwa mtu hodari wa vita; lakini alikuwa mwenye ukoma. Na Washami walikuwa wametoka vikosi vikosi, wakachukua mfungwa mmoja kijana mwanamke kutoka nchi ya Israeli; naye akamhudumia mkewe Naamani. Akamwambia bibi yake, Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake. Mtu mmoja akaingia, akamwambia bwana wake, akasema, Yule kijana mwanamke aliyetoka nchi ya Israeli asema hivi na hivi. Mfalme wa Shamu akasema, Haya! Basi, mimi nitampelekea mfalme wa Israeli waraka. Basi, akaenda zake, akachukua mikononi mwake talanta kumi za fedha, na vipande vya dhahabu elfu sita, na mavazi kumi. Akampelekea mfalme wa Israeli waraka ule, kusema, waraka huu utakapokuwasilia, tazama, nimemtuma mtumishi wangu Naamani kwako, ili upate kumponya ukoma wake. Ikawa, mfalme wa Israeli alipousoma waraka, alirarua mavazi yake, akasema, Je! Mimi ni Mungu, niue na kuhuisha, hata mtu huyu akanipelekea mtu nimponye ukoma wake? Fahamuni, basi, nakusihini, mwone ya kuwa mtu huyu anataka kugombana nami. Ikawa, Elisha, yule mtu wa Mungu, aliposikia ya kwamba mfalme wa Israeli ameyararua mavazi yake, ndipo akatuma mtu kwa mfalme, akisema, mbona umeyararua mavazi yako? Na aje sasa kwangu mimi, naye atajua ya kuwa yuko nabii katika Israeli. Basi Naamani akaja na farasi wake na magari yake, akasimama mlangoni pa nyumba ya Elisha. Naye Elisha akampelekea mjumbe, akisema. Enenda ukaoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itakurudia nawe utakuwa safi. Lakini Naamani akakasirika, akaondoka, akasema, Tazama, nalidhania, Bila shaka atatoka kwangu, na kusimama, na kuomba kwa jina la Bwana, Mungu wake, na kupitisha mkono wake mahali penye ugonjwa, na kuniponya mimi mwenye ukoma Je! Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora kuliko maji yote ya Israeli? Je! Siwezi kujiosha ndani yake, na kuwa safi? Akageuka, akaondoka kwa hasira. Watumishi wake wakamkaribia, wakamwambia, wakasema, Baba yangu, kama yule nabii angalikuambia kutenda jambo kubwa, usingalilitenda? Je! Si zaidi basi, akikuambia, Jioshe, uwe safi? Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi, ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi. Akamrudia yule mtu wa Mungu, yeye na mafuatano yake yote. Akaja, akasimama mbele yake; akasema, Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika Israeli, basi nakuomba upokee baraka kwa mtumwa wako.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 42:1-2, 43:3-4

 1. Kama ayala aioneavyo shauku mito ya maji.
  Vivyo hivyo nafsi yangu inakuonea shauku, Ee Mungu.
  (K) Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu,
  Mungu aliye hai,
  Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu.
 2. Nafsi yangu inamwonea kiu Mungu, Mungu aliye hai,
  Lini nitakapokuja nionekane mbele za Mungu? (K)
 3. Niletewe nuru yako na kweli yako ziniongoze,
  Zinifikishe kwenye mlima wako mtakatifu
  Na hata maskani yako. (K)
 4. Hivyo nitakwenda madhabahuni kwa Mungu,
  Kwa Mungu aliye furaha yangu na shangwe yangu. (K)

INJILI: Lk 4: 24-30.
Yesu alifika Nazareti akawaambia makutano hekaluni: Amin, nawaambia ya kuwa, Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe. Lakini, kwa hakika nawaambia, Palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati mbingu zilipofungwa miaka mitatu na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima; wala Eliya hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni. Tena, palikuwa na wenye ukoma wengi katika Israeli zamani za nabii Elisha, wala hapana aliyetakaswa ila Naamani, mtu wa Shamu Wakajaa ghadhabu wote waliokuwa katika sinagogi walipoyasikia hayo. Wakaondoka wakamtoa nje ya mji, wakampeleka mpaka ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu yake, wapate kumtupa chini; lakini yeye alipita katikati yao, akaenda zake.

TAFAKARI:
UTU NI BORA KULIKO SADAKA: Masomo yote ya leo yanamzungumzia Naamani mtu wa Shamu, jinsi alivyokuwa hodari lakini mhitaji wa huruma ya Mungu kwa vile alivyokuwa mkoma. Katika jamii ya Kiyahudi, ukoma ulikuwa ni ugonjwa ambao haumruhusu mhusika kuchangamana na wengine. Mgonjwa alitengwa. Naamani alipoambiwa na nabii wa Mungu aende akajichovye majini mara saba anakasirika na kukaidi. Anapanda kiburi na kujiona. Anajisikia mtu maarufu sana na anatoa dharau hadi watumishi wake wanachukua hatua ya kumshauri na kumshawishi akubaliane na alichoambiwa. Jamii yetu ya leo inayo waamini wengine wenye tabia kama ya Naamani. Wanaweza kushauriwa mambo zuri lakini hawatatenda kutokana na hadhi yao. Badala yake hujaa majivuno na kujiona. Ndiyo kisa, Yesu katika Injili anagusia mkasa wa kwamba inatokea jamii kukosa heshima na utii kwa mhusika hasa pale inapojua ni nani. Kumbe, jambo hili linasababishwa na kukosa unyenyekevu. Hima, tujifunze unyenyekevu.

SALA: Ee Yesu utujalie neema ya kutii wajumbe wako.