MACHI 7, 2021; DOMINIKA: DOMINIKA YA 3 YA KWARESIMA

Urujuani
Zaburi: Juma1

SOMO 1: Kut 20 :1-17
Mungu alinena maneno haya yote akasema, Mimi ni Bwana, Mungu wako, niliyekutoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utuMwa Usiwe na miungu ila mimi. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi Bwana Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu. Usilitaje bure jina la Bwana, Mungu wako, maana Bwana hatamhesabia kuwa hana hatia mtu alitajaye jina lake bure. Ikumbuke siku ya Sabato uitakase. Siku sita fanya kazi, utende mambo yako yote lakini siku ya saba ni Sabato ya Bwana Mungu, siku hiyo usifanye kazi yo yote, wewe, wala mwana wako, wala binti yako, wala mtumwa wako, wala mjakazi wako, wala mnyama wako wa kufuga, wala mgeni aliye ndani ya malango yako. Maana, kwa siku sita Bwana alifanya mbingu, na nchi, na bahari, na vyote vilivyomo, akastarehe siku ya saba, kwa hiyo Bwana akaibariki siku ya Sabato akaitakasa. Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako. Usiue. Usizini. Usiibe. Usimshuhudie jirani yako uongo. Usiitamani nyumba ya jirani yako, usimtamani mke wa jirani yako; wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng’ombe wake, wala punda wake, wala cho chote alicho nacho jirani yako.

WIMBO WA KATIKATI: Zab 19: 7-10

 1. Sheria ya Bwana ni kamilifu,
  Huiburudisha nafsi.
  Ushuhuda wa Bwana ni amini,
  Humtia mjinga hekima
  (K) Wewe, Bwana, ndiwe mtakatifu wa Mungu.
 2. Maagizo ya Bwana ni ya adili,
  Huufurahisha moyo.
  Amri ya Bwana ni safi,
  Huyatia macho nuru. (K)
 3. Kicho cha Bwana ni kitakatifu,
  Kinadumu milele.
  Hukumu za Bwana ni kweli
  Zina haki kabisa (K)
 4. Ni za kutamanika kuliko dhahabu,
  Kuliko wingi wa dhahabu safi.
  Nazo ni tamu kuliko asali,
  Kuliko sega la asali. (K)

SOMO 2: 1 Kor 1 :22-25
Wayahudi wanataka ishara, na Wayunani wanatafuta hekima; bali sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi; bali kwao waitwao, Wayahudi kwa Wayunani, ni Kristo, nguvu ya Mungu, na hekima ya Mungu. Kwa sababu upumbavu wa Mungu una hekima zaidi ya wanadamu, na udhaifu wa Mungu una nguvu zaidi ya wanadamu

SHANGILIO: Yn 3:16
Jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu,
Hata akamtoa Mwanawe wa pekee,
Ili kila mtu amwaminiye awe na uzima wa milele

INJILI: Yn 2 :13-25
Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; naye Yesu akakwea mpaka Yerusalemu. Akaona pale hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng’ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi. Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng’ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao; akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara. Wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa imeandikwa, Wivu wa nyumba yako utanila. Basi Wayahudi wakajibu wakamwambia, Ni ishara gani utuoneshayo, kwamba unafanya haya? Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha. Basi Wayahudi wakasema, Hekalu hili lilijengwa katika muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha katika siku tatu? Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake. Basi alipofufuka katika wafu, wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa alisema hivi, wakaliamini lile andiko na lile neno alilolinena Yesu. Hata alipokuwapo Yerusalemu kwenye sikukuu wakati wa Pasaka, watu wengi waliamini jina lake, walipoziona ishara zake alizofanya. Lakini Yesu hakujiaminisha kwao; kwa kuwa yeye aliwajua wote; na kwa sababu hakuwa na haja ya mtu kushuhudia habari za mwanadamu; kwa maana yeye mwenyewe alijua yaliyomo ndani ya mwandamu

TAFAKARI:
KUABUDU KWA ROHO YA KWELI: Katika somo la kwanza, Mwenyezi Mungu anafananisha uhusiano kati ya amri za Mungu na taifa la Israeli kama uhusiano uliopo katika kumzaa mtoto na kumpatia njia ya kumkuza katika maadili bora. Kwa maneno yake katika amri kumi, Mwenyezi Mungu anawazaa watoto wapya, taifa jipya, na njia mpya ya maisha, na kuandaa maisha mapya ya kutoka jangwani na kulilinda kundi hadi kufikia mwisho na lengo la safari. Amri kumi za Mungu ni kiini cha uhusiano kati ya wana wa Israeli na Mwenyezi Mungu na kati yao wenyewe. Kwa Wakristo, kutolewa utumwani na kupelekwa katika nchi ya ahadi hufanyika kwa njia ya ubatizo. Ubatizo wetu hutuondolea dhambi ya asili, hutufanya kuwa watoto wa Mungu na wa Kanisa; pia tunakubali kuwa kioo cha jamii kwa kuwatoa watu utumwani na kuwafanya kuwa huru. Wimbo wetu wa katikati unatupa muhtasati mzima wa masomo yetu leo “Bwana unayo maneno ya uzima wa milele” (Zab 19). Maneno ya Bwana yana uwezo wa kutufanya huru na kutupatia matumaini mapya. Sheria ya Mungu ni kamilifu na haki, huburudisha nafsi, hutoa mwanga, ukweli na haki. Ni bora zaidi kuliko dhahabu. Ni tamu kuliko asali. Sheria hii inaelezwa na Mwenyezi Mungu katika amri kumi anazotupatia leo.
Mtumee Paulo anawaambia Wakorintho kwamba kusulubiwa kwa Kristo ni alama ya upendo wa Mungu kwa wote. Lakini kwa Wayahudi ni kikwazo na kwa Wayunani ni ujinga. Wayahudi walitegemea upendo wa Mungu ujirudie kama ilivyotokea katika kipindi cha Musa waliposafiri kutoka Misri. Wayunani au Wagiriki waliamini vitu kwa kutumia akili yao. Walithamini falsafa kuliko imani. Kifo cha Yesu msalabani hakikuingia katika mantiki ya akili zao na hivyo ilikuwa ni ujinga tu. Wengi wetu tunaweza kuanguka katika hali kama hizi za Wagiriki na Wayahudi.
Injili yetu leo inatupatia habari za Yesu kulitakasa hekalu kwa kuwafukuza wafanyabiashara ndani yake. Wakati wa Pasaka, Yerusalemu ilikuwa imejawa na mahujaji kutoka katika kila kona ya dunia. Walienda hekaluni kusali, kutafuta ushauri kutoka kwa makuhani, kutolea sadaka kwa Mungu na kutolea mapaji yao kwa Mungu kwa ukarimu, vitu ambavyo vingetumika tu kwenye hekalu. Hela ya Warumi ilioneakana kama hela isiyo na baraka hivyo ilibidi ibadilishwe na hela nyingine na wale wabadilisha fedha. Kipindi hiki wafanyabiashara walitumia muda huu kupata faida zaidi kuliko kipindi kingine chote cha mwaka. Ni kipindi ambacho pia makuhani walipata faida sana. Waliruhusu wafanyabiashara na wabadilisha fedha kutumia hekalu. Sehemu yote ilijaa mahujaji wakifanya biashara mbalimbali. Sehemu ya sala ilibadilishwa na makuhani wenyewe kuwa soko. Kipindi hiki cha Pasaka Yesu alikuja hekaluni. Yesu hakusema neno, alifanyiza kiboko na kuwafukuza hekaluni na kuwatoa mbuzi, kondoo na njiwa nje. Ishara hii ya Yesu, ilikuwa na lengo la kukomesha sadaka za wanyama wa kuteketezwa.
Yesu anaamua kutoa mwili wake mwenyewe, kama sadaka safi yenye kumpendeza Baba. “Hivi ndivyo tulivyotambua jinsi pendo lilivyo, kwamba Baba alimtoa Mwanae wa pekee” (1 Yn 3:16). Yesu aliyejitolea mwenyewe “mpole na mnyenyekevu wa moyo” (Mt 11:29), sasa anatoa amri: “Yatoeni haya, na acheni kuifanya nyumba ya Baba yangu kuwa pango la walanguzi.” Imeandikwa, “Hakutakuwa tena na biashara katika nyumba ya Mungu”(Zek 14:21). Kwa kufanya hivi Yesu, alionesha hatari iliyopo katika kuchanganya dini na pesa, kati ya kumtumikia Mungu na mali.
Kwaresima inatualika kutazama kwa karibu ndani yetu, parokia yetu, na Kanisa letu. Je, mahekalu yetu yanafanana na mwili wa Yesu. Wayahudi walijifunga wenyewe na sheria ambazo hazikutoa sifa kwa Mungu. Kuabudu ni hali ya kweli ya kumwelekea Mungu pekee. Kuabudu kunaleta maana sana ikiwa tunaweza kuishi kile tunachofanya kanisani na kukitendea kazi katika maisha ya kawaida. Ibada ya kweli ni kuwajali jirani zetu na maskini na kuwaheshimu watu wote na kushirikisha kile tulichopewa na Mungu (Yak 1:27) na daima kuelewa kwamba tumekombolewa katika utumwa, utumwa wa dhambi. Ibada bila uaminifu ni kumkosea heshima Mwenyezi Mungu na kuonesha picha mbaya kuhusu Mungu.
Yesu alikuwa sahihi kabisa katika kulitunza na kulilinda hekalu la Mungu. Je, upo tayari kulilinda hekalu la Mungu? Na kumwambudu Mungu katika hali ya kweli na kumshuhudia katika hali zote? Yesu anatimiza unabii wa maneno ya Zaburi ya 69, “Wivu wa nyumba yako hakika umenila.” Ni kitu gani kinachokumaliza wewe? Pesa, kazi, hofu, michezo, watoto, ndoa, umbea/kusengenya? Yesu anaongelea hekalu kama mwili wake mwenyewe. Je, ni namna gani unavyolitendea hakalu la mwili wako? Ni kwa jinsi gani unalitendea hekalu la ndugu yako? Unawatendeaje wagonjwa waliowekwa chini yako, wazee, yatima na watu maskini?.

SALA: Ee Bwana nisaidie nitengeneze njia zangu ili Yesu aweze kupata njia na sehemu ya kukaa ndani yangu.