MACHI 3, 2021; JUMATANO: JUMA LA 2 LA KWARESIMA

Urujuani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Yer 18: 18-20
Waliposema, Njoni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima, wala neno halitampotea nabii. Njoni, na tumpige kwa ndimi zetu, wala tusiyaangalie maneno yake yo yote. Niangalie, Ee Bwana, ukasikilize sauti ya wanaoshindana nami. Je! Mabaya yalipwe badala ya mema? Maana wameichimbia nafsi yangu shimo. Kumbuka jinsi nilivyosimama mbele zako, ili niseme mema kwa ajili yao, nikaigeuze ghadhabu yako isiwapate.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 31:4-5, 13-15

 1. Utanitoa katika wavu walionitegea kwa siri,
  Maana Wewe ndiwe ngome yangu.
  Mikononi mwako naiweka roho yangu;
  Umenikomboa, Ee Bwana, Mungu wa kweli.
  (K)Uniokoe kwa ajili ya fadhili zako, Ee Bwana.
 2. Maana nimesikia masingizio ya wengi;
  Hofu ziko pande zote.
  Waliposhauriana juu yangu,
  Walifanya hila wauondoe uhai wangu. (K)
 3. Lakini mimi nakutumaini Wewe, Bwana,
  Nimesema, Wewe ndiwe Mungu wangu.
  Nyakati zangu zimo mikononi mwako;
  Uniponye na adui zangu, nao wanaonifuatia. (K)

INJILI: Mt 20: 17-28
Yesu alipokua akipanda kwenda Yerusalemu, aliwachukua wale wanafunzi kumi na wawili faraghani; na njiani akawaambia, Angalieni, tunapanda kwenda Yerusalemu; na Mwana wa Adamu atatiwa mikononi mwa wakuu wa makuhani na waandishi; nao watamhukumu afe; kisha watampeleka kwa Mataifa wapate kumdhihaki, na kumpiga mijeredi, na kumsulibisha; na siku ya tatu atafufuka. Ndipo mama yao wana wa Zebedayo akamwendea pamoja na wanawe, akamsujudia, na kumwomba neno. Akamwambia, Wataka nini? Akamwambia, Agiza kwamba hawa wanangu wawili waketi mmoja mkono wako wa kuume, na mmoja mkono wako wa kushoto, katika ufalme wako. Yesu akajibu akasema, Hamjui mnaloliomba. Je! Mwaweza kunywea kikombe nitakachonywea mimi? Wakamwambia, Twaweza. Akawaambia, Hakika mtakinywea kikombe changu; lakini kuketi mkono wangu wa kuume na mkono wangu wa kushoto, sina amri kuwapa, bali watapewa waliowekewa tayari na Baba yangu. Na wale kumi waliposikia, waliwakasirikia wale ndugu wawili. Lakini Yesu akawaita, akasema, Mwajua ya kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu ye yote anayetaka kuwa mkubwa kwenu, na awe mtumishi wenu; na mtu ye yote anayetaka kuwa wa kwanza kwenu na awe mtumwa wenu; Kama vile Mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumikia, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.

TAFAKARI:
UKWELI UNAUMA: Kwa sababu walielezwa ukweli wa uovu wao wahusika waliohubiriwa na Yeremia walichomwa mioyo na hivyo wakajenga uadui naye. Binadamu ni kiumbe asiyependa kuelezwa ukweli, anapenda kusifiwa hata kama ameharibu. Katika Injili tunaona mama wa wafuasi wawili anawaombea heri wanawe hadi yeye mwenyewe anajisahau. Tunaloweza kujifunza hapa ni faraja wanayopata wazazi pale watoto wao wanapokuwa na maisha ya heri. Leo hii tunashuhudia wimbi la vijana wengi mitaani ambao wanaishi maisha yasiyo na malezi bora, imefika mahali utadhani wazazi wamechoka kulea. Vijana hawaambiliki mfumo wao wa maisha ni wa kusikitisha, vaa yao ni ya aibu, nguo zisizo na maadili, kunyoa kihuni, utumiaji wa madawa ya kulevya, ulevi uliopindukia, hawafanyi kazi bali kuzurura tu wakati pesa na mali wanataka. Jambo hili kwa mzazi yeyote mwenye mapenzi mema kama huyu mama wa wana wa Zebedayo lazima limuumize na hivyo wote tuwaombee vijana wetu na kuwalea, tusichoke kulea. Tuwe kama huyu mama wa Injili ya leo.

SALA: Baba, wajalie vijana wetu neema ya kuwa wasikivu kwa malezi.