MACHI 2, 2021; JUMANNE: JUMA LA 2 LA KWARESIMA

Urujuani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Isa 1: 10, 16-20
Lisikieni neno la Bwana, enyi waamuzi wa Sodoma; tegeni masikio msikie sheria ya Mungu wetu, enyi watu wa Gomora. Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane. Haya, njoni, tusemezane; asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sUfu Kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi; bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa upanga; maana kinywa cha Bwana kimenena haya.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 50:8-9, 16-17, 21-23

 1. Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako,
  Na kafara zako ziko mbele yangu daima.
  Sitatwaa ng’ombe katika nyumba yako,
  Wala beberu katika mazizi yako.
  (K) Autengenezaye mwenendo wake,
  Nitamwonyesha wokovu wa Mungu.
 2. Una nini wewe kuitangaza sheria yangu,
  Na kuliweka agano langu kinywani mwako?
  Maana wewe umechukia maonyo,
  Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako. (K)
 3. Ndivyo ulivyofanya, nami nikanyamaza,
  Ukadhani ya kuwa Mimi ni kama wewe,
  Atoaye dhabihu za kushukuru, ndiye anayenitukuza.
  Naye autengenezaye mwenyendo wake,
  Nitamwonyesha wokovu na Mungu. (K)

INJILI: Mt 23: 1-12
Yesu aliwaambia makutano na wanafunzi wake, akasema, Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa; basi, yo yote watakayowaambia, myashike, na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi. Wao hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani mwao; wasitake wenyewe kuigusa kwa kidole chao. Tena matendo yao yote huyatenda ili kutazamwa na watu; kwa kuwa hupanua hirizi zao, huongeza matamvua yao; hupenda viti vya mbele katika karamu, na kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni, na kuitwa na watu, Rabi. Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu. Wala msimwite mtu baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni. Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo. Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu. Na ye yote atakayejikweza, atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa.

TAFAKARI:
KUMBADILI MWANADAMU KWAHITAJI SADAKA KUBWA: Katika somo la kwanza tunaona wazi jinsi watu wa Sodoma na Gomora walivyotenda maovu hadi kutibua hasira ya Mungu. Mungu pamoja na hayo yote bado anachukua hatua ya kutoa muda wa kutubu. Anaonesha wazi kuwa msamaha wake ni zaidi ya matarajio ya binadamu, anasema, “Ijapo dhambi zetu zitakuwa nyekundu kama bendera”bado msamaha wake upo ili mradi mhusika ajitambue na kutubu. Katika Injili Yesu anagusia swala la kuwa kiongozi na tahadhari inayotakiwa kuchukuliwa. Jamii inatakiwa kuelewa kuwa uongozi ni zawadi toka kwa Mungu na hivyo kuutimiza kwa unyenyekevu wote na ipasavyo. Katika jamii ya leo tunashuhudia viongozi wetu wengine wakitenda kwa kupendelea na hivyo kuumiza wengine, viongozi kuwa watendaji kwa maneno, kupenda sana kuheshimiwa, na akikosolewa kujenga chuki na uadui na aliyemkosoa. Kristo anatutaka leo tuwaombee viongozi kama hao kusudi wajitambue na hivyo watende kwa haki na busara.

SALA: Ee Yesu utujalie tuwe viongozi wema na uwasaidie viongozi wetu watuongoze vyema.