MACHI 1, 2021; JUMATATU: JUMA LA 2 LA KWARESIMA

Urujuani
Zaburi: Juma 4

SOMO 1: Dan 9: 4b-10
Ee Bwana, Mungu mkuu, mwenye kutisha, ashikaye maagano ya rehema kwao wampendao, na kuzishika amri zake; tumefanya dhambi, tumefanya ukaidi, tumetenda maovu, tumeasi, naam, hata kuyaacha maagizo yako na hukumu zako; wala hatukuwasikiliza watumishi wako, manabii, ambao kwa jina lako walisema na wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, na watu wote wa nchi. Ee Bwana, haki i na wewe lakini kwetu sisi kuna haya ya uso, kama hivi leo; kwa watu wa Yuda, na kwa wenyeji wa Yerusalemu, na kwa Israeli wote, walio karibu na hao walio mbali, katika nchi zote ulikowafukuza, kwa sababu ya makosa yao waliyokukosa. Ee Bwana, kwetu sisi kuna haya ya uso, kwa wafalme wetu, na wakuu wetu, na baba zetu, kwa sababu tumekutenda dhambi. Rehema na msamaha ni kwa Bwana Mungu wetu, ingawa tumemwasi; wala hatukuitii sauti ya Bwana, Mungu wetu, kwa kwenda katika sheria zake, alizoziweka mbele yetu kwa kinywa cha watumishi wake, manabii.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 79:8-9, 11, 13

 1. Usikumbuke juu yetu maovu ya baba zetu,
  Rehema zako zije kutulaki hima,
  Kwa maana tumeadhilika sana.
  (K)Usitutende sawasawa na hatia zetu, Ee Bwana.
 2. Ee Mungu wokovu wetu utusaidie.
  Kwa ajili ya utukufu wa jina lako.
  Utuokoe, utughofiri dhambi zetu,
  Kwa ajili ya jina lako. (K)
 3. Kuugua kwake aliyefungwa na kuingie mbele zako.
  Kwa kadiri ya uweza wa mkono wako
  Uwahifadhi wana wa mauti.
  Na sisi tulio watu wako, na kondoo za malisho yako,
  Tutakushukuru milele;
  Tutazisimulia sifa zako kizazi kwa kizazi. (K)

INJILI: Lk 6:36-38
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma. Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa. Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa.

TAFAKARI:
UTII KATIKA MAISHA HULETA UTULIVU: Wahenga wana msemo usemao, “Asiyesikia la mkuu huvunjika guu.” Ujumbe wa somo la kwanza umeonesha wazi mahangaiko ya taifa la wateule wa Mungu kwa kutokuwa wasikivu kwa yale waliyokuwa wanaaswa na hivi wameona matokeo yake. Wanaomba huruma ya Mungu na msamaha wake, ndiyo maana Kristo katika Injili anaonesha kuwa Mungu ni Baba wa huruma na hivyo kututaka hata sisi wafuasi wake tuishi huruma hiyo tungali hapa duniani. Tutendeane huruma. Mwanadamu akikosa huruma inakuwa rahisi kuhukumu mwingine. Tu wepesi kuona makosa na madhaifu ya wengine na hivyo kuishia kuwarushia lawama, “Oh fulani ni mzembe, hafai!” na kadhalika. Kufika hatua hii husababishwa na kukosa huruma.

SALA: Ee Bwana Yesu utuhurumie kutusamehe kwa kutotii kwetu.