FEBRUARI 27, 2021; JUMAMOSI: JUMA LA 1 LA KWARESIMA

Urujuani
Zaburi: Juma 3

SOMO I: Kum 26:16-19
Musa aliwaambia watu: Leo hivi akuamuru Bwana, Mungu wako, kuzifanya amri hizi na hukumu; basi uzishike na kuzifanya kwa moyo wako wote na roho yako yote. Umemwungama Bwana leo, kuwa ndiye Mungu wako, na kuwa yakupasa kutembea katika njia zake, na kushika amri zake na maagizo yake, na hukumu zake, na kusikiliza sauti yake; naye Bwana amekuungama hivi leo kuwa taifa ililotengwa iwe yake yeye, kama alivyokuahidi, na kuwa yakupasa kushika maagizo yake yote; na kuwa atakutukuza juu ya mataifa yote aliyoyafanya kwa sifa, na jina, na heshima, nawe upate kuwa taifa takatifu kwa Bwana, Mungu wako, kama alivyosema.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 119:1-2, 4-5, 7-8

 1. Heri walio kamili njia zao,
  Waendao katika sheria ya Bwana.
  Heri wazitiio shuhuda zake,
  Wamtafutao kwa moyo wote.
  (K)Heri walio kamili njia zao,
  Waendao katika sheria ya Bwana.
 2. Wewe umetuamuru mausia yako,
  Ili sisi tuyatii sana.
  Ningependa njia zangu ziwe thabiti
  Nizitii amri zako. (K)
 3. Nitakushukuru kwa unyofu wa moyo,
  Nikiisha kujifunza hukumu za haki yako.
  Nitazitii amri zako,
  Usiniache kabisa.

INJILI: Mt 5: 43-48
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi; ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi, mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru; je! nao hawafanyi yayo hayo? Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! nao hawafanyi kama hayo? Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.

TAFAKARI:
WAPENDENI MAADUI WENU: Matakwa ya Yesu kwetu si tu kwamba tusijizuie ushirika na maadui zetu wanaoharibu heshima yetu, bali twende mbali zaidi na kwa kuwapenda zaidi adui zetu. Adui zetu si kila mtu anayekuwa kinyume yetu, bali yule mwenye nia mbaya dhidi yetu, asiyependa maendeleo yetu ya kimwili na kiroho pia. Yesu anatufundisha leo kwamba, hawa walio maadui wetu na wasiotutakia mema, hatuna budi kuwachukia bali kuwapenda na kuwaonesha kwamba hatuna kinyongo nao. Si jambo rahisi katika ubinadamu wetu kuwapenda maadui zetu, lakini tukiwa tumeunganika na Mungu, si vigumu hata kidogo kuwapenda maadui wetu. Katika Kwaresma hii, tumuige Kristo, kufa kwa ajili ya adui zetu, kuliko kuwafanya wao wafe kwa ajili yetu. Kwa utayari wa kufa kwa ajili ya adui zako, utaungana na Kristo aliyekuwa rafiki hata wa maadui zake aliowaombea msamaha pale msalabani akisema, “Baba, uwasamehe watu hawa, kwa kuwa hawajui walitendalo” (Lk 23:34).

SALA: Baba, nijalie moyo wa upendo hasa kwa walio maadui zangu.