FEBRUARI 26 IJUMAA: JUMA LA 1 LA KWARESIMA

Urujuani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Eze 18: 21-28
Bwana asema hivi: mtu mbaya akighairi, na kuacha dhambi zake zote alizozitenda, na kuzishika amri zangu zote, na kutenda yaliyo halali na haki, hakika ataishi, hatakufa. Dhambi zake zote alizozitenda hazitakumbukwa juu yake hata moja wapo; katika haki yake aliyoitenda ataishi. Je! Mimi ninafurahia kufa kwake mtu mwovu? Asema Bwana Mungu; si afadhali kwamba aghairi, na kuiacha njia yake, akaishi? Bali mwenye haki atakapoghairi, na kuicha haki yake, na kutenda uovu, na kufanya machukizo yote kama yale afanyayo mtu mwovu, je, ataishi? Katika matendo yake yote ya haki aliyoyatenda halitakumbukwa hata mojawapo. Katika kosa lile alilolikosa, na katika dhambi yake aliyoitenda, atakufa. Lakini ninyi mwasema, njia ya Bwana si sawa. Sikilizeni sasa, enyi nyumba ya Israeli; je! Njia yangu siyo iliyo sawa? Njia zenu sizo zisizo sawa? Mwenye haki atakapoghairi, na kuiacha haki yake, na kutenda uovu, atakufa katika uovu huo; katika uovu wake alioutenda atakufa. Tena, mtu mwovu atakapoghairi, na kuuacha uovu wake alioutenda, na kutenda yaliyo halali na haki, ataponya roho yake, nayo itakuwa hai. Kwa sababu atafakari, na kughairi, na kuyaacha makosa yake yote aliyoyatenda, hakika ataishi, hatakufa.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 130

 1. Ee Bwana, toka vilindini nimekulilia.
  Bwana, uisikie sauti yangu.
  Masikio yako na yasikilize
  Sauti ya dua zangu.
  (K) Bwana kama Wewe ungehesabu maovu,
  Ee Bwana, nani angesimama?
 2. Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu,
  Ee Bwana, nani angesimama?
  Lakini kwako kuna msamaha,
  Ili Wewe uogopwe. (K)
 3. Nimemngoja Bwana, roho yangu imengoja
  Na neno lake nimelitumainia.
  Nafsi yangu inamngoja Bwana,
  Kuliko walinzi waingojavyo asubuhi,
  Naam, walinzi waingojavyo asubuhi. (K)
 4. Ee Israeli, umtarajie Bwana;
  Maana kwa Bwana kuna fadhili,
  Na kwake kuna ukombozi mwingi.
  Yeye atamkomboa Israeli na maovu yake yote. (K)

INJILI: Mt 5: 20-26
Siku ile Yesu aliwaambia wafuasi wake: Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue; na mtu akiua, itampasa hukumu. Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye ndugu yake hasira itampasa hukumu; na mtu akimfyolea ndugu yake, itampasa baraza; na mtu akimwapiza, itampasa jehanum ya moto. Basi ukileta sadaka yako madhabahuni, na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, uende zako, upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako. Patana na mshitaki wako upesi, wakati uwapo pamoja naye njiani; yule mshitaki asije akakupeleka kwa kadhi, na kadhi akakupeleka kwa askari, ukatupwa gerezani. Amin, nakuambia, Hutoki humo kamwe hata uishe kulipa senti ya mwisho.

TAFAKARI:
MOYO WA JUMUIYA: Anachokisema Yesu katika Injili ya leo ni “Ibada zenu ni lazima ziseme wazi katika maisha yenu.” Na kwamba, usilete sadaka yako altareni, ukadhani umemaliza na kwamba imekubalika. Kristo anatukumbusha kwamba, kama kuna kitu hakiendi sawa kwenye familia yenu, labda kuna chuki na magonvi, sadaka hiyo haikubaliki hadi pale tatizo na tofauti zenu zitakapoondolewa. Kumbe Kristo anatukumbusha moyo wa upendo kati yetu, ili tumtolee Mungu sadaka inayokubalika. Jumuiya ya Kikristo inapaswa kuanzia kwenye familia yako, jirani yake, jumuiya ndogondogo hadi Kanisa zima. Katika umoja uliojaa upendo, sadaka za jumuiya zetu zitakubaliwa na Mungu. Tunapaswa kutengeneza na kujenga familia imara kiimani, ambazo zitadumu katika kuyafuata yale yanayofundishwa na Kanisa, na katika hayo, upendo utatawala na kusababisha maelewano, haki na amani, hali ambayo itawafanya wana jumuiya kukubalika na Mungu wao na sadaka zao. Pamoja katika jumuiya imara kiimani, sadaka yetu itampendeza Mungu

SALA: Ee Mungu, tujalie moyo mwema katika jumuiya zetu.