FEBRUARI 25, 2021; ALHAMISI: JUMA LA 1 LA KWARESIMA

Urujuani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Esta 14:1-14
Malkia Esta naye alimkimbilia Bwana, akishikwa na uchungu wa mauti. Akazivua nguo zake za fahari akavaa nguo za huzuni na kilio, na badala ya manukato mazuri alijitia majivu na samadi kichwani; akajinyenyekesha mwili wake, hata mahali pa mapambo ya furaha alijifunika kwa nywele zake zilizofumuliwa. Akamwomba Bwana wa Israeli, akisema: Bwana wangu, Wewe peke yako u Mfalme wetu. Unisaidie mimi niliye mkiwa, wala sina msaidizi mwingine ila Wewe; maana hatari yangu imo mkononi mwangu. Tangu nilipozaliwa katika kabila ya jamaa yangu, nimesikia ya kuwa Wewe, Bwana, ulimchagua Israeli katika mataifa yote, na baba zetu katika jamaa zao, kuwa urithi wa daima, ukawatimilizia yote uliyoyaahidi. Utukumbuke, Ee Bwana; ujifunue wakati wa taabu yetu; unipe moyo thabiti, Ee mfalme wa miungu na Bwana wa milki zote. Unitie kinywani mwangu maneno ya kufaa mbele ya simba, ukaugeuza moyo wake apate kumchukia yule anayepigana nasi, ili akomeshwe pamoja na wote wenye nia moja naye. Lakini utuokoe sisi kwa mkono wako; unisaidie mimi niliye peke yangu, bila msaidizi mwingine ila wewe, Bwana.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 138:1-3, 8-9

 1. Nitakushukuru kwa moyo wangu wote,
  Mbele ya miungu nitakuimbia zaburi.
  Nitasujudu nikilikabili hekalu lako takatifu
  Nitalishukuru jina lako.
  (K) Siku ile niliyokuita uliniitikia,
  Ukanifariji nafsi kwa kunitia nguvu.
 2. Kwa ajili ya fadhili zako na uaminifu wako,
  Kwa maana umeikuza ahadi yako,
  Kuliko jina lako lote.
  Siku ile niliyokuita uliniitikia
  Ukanifariji nafsi yangu kwa kunitia nguvu. (K)
 3. Na mkono wako wa kuume utaniokoa.
  Bwana atanitimizia mambo yangu;
  Ee Bwana, fadhili zako ni za milele;
  Usiziache kazi za mikono yako. (K)

INJILI: Mt 7: 7-12
Siku ile Yesu aliwaambia wafuasi wake, Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe? Au akiomba samaki, atampa nyoka? Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao? Basi yo yote myatakayo mtendewe na watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii.

TAFAKARI:
KUOMBA NA KUPATA: Maandiko Matakatifu yanampongeza Mungu mwenye huruma kwa wote wanaomwita na wanaoitwa. Waitwao hukumbuka ahadi ya Mungu kwao kila aombaye kwa jina lake atapewa kwani kila aombaye kwa imani, atapewa. Lakini kuna mwangwi au sauti zingine zinazosikika kwa miaka mingi, kilio cha maradhi, kukosekana kwa haki na kukata tamaa. Na kilio cha sala namna hiyo haipati majibu. Kanisa siku zote husali kwa ajili ya umoja, haki, amani na uhuru ambao mtu anamtumikia Mungu kulingana na anavyoyafahamu. Ni katika mambo hayo, sisi wanadamu tunahakikishiwa na Yesu kwamba, katika, amani, haki, amani na uhuru, tunapaswa kumkimbilia Mungu na kumuomba kwa imani, naye kwa sababu hana historia ya uchoyo, atatupa tu. Hakuna shida ya mwanadamu inayokosa majibu kwa Mungu, hivyo katika kipindi hiki cha Kwaresma, tusisite kuja kwa na kumuomba katika ugonjwa, shida ya ajira na hata upungufu wa imani kwani Yeye si mchoyo.

SALA: Tunakuomba Mungu wetu, utujalie moyo wa kukukimbilia wewe.