FEBRUARI 24, 2021; JUMATANO: JUMA LA 1 LA KWARESIMA

Urujuani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Yon 3: 1-10
Neno la Bwana likamjia Yona mara ya pili, kusema, Ondoka uende Ninawi, mji ule mkubwa, ukaihubiri habari nitakayokuamuru. Basi Yona akaondoka, akaenda Ninawi, kama Bwana alivyonena. Basi Ninawi ulikuwa mji mkubwa mno, ukubwa wake mwendo wa siku tatu, Yona akaanza kuuingia mji kwa mwendo wa siku moja, akapaza sauti yake, akasema, Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa. Basi watu wa Ninawi wakamsadiki Mungu; wakatangaza kufunga, wakajivika nguo za magunia, tangu yeye aliye mkubwa hata yeye aliye mdogo. Habari ikamfikia mfalme wa Ninawi, naye akaondoka katika kiti chake cha enzi, akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia, na kuketi katika majivu. Naye akapiga mbiu, akatangaza habari katika mji wa Ninawi, kwa amri ya mfalme na wakuu wake, kusema. Mwanadamu asionje kitu, wala mnyama wala makundi ya ng’ombe, wala makundi ya kondoo; wasile, wala wasinywe maji; bali na wafunikwe nguo za magunia, mwanadamu na mnyama pia, nao wakamlilie Mungu kwa nguvu, naam, na wageuke, kila mtu akaache njia yake mbaya, na udhalimu ulio mikononi mwake. Ni nani ajuaye kwamba Mungu hatageuka na kughairi, na kuiacha hasira yake kali, ili tusiangamizwe? Mungu akaona matendo yao, ya kuwa wameiacha njia yao mbaya. Basi Mungu akalighairi neno lile baya, ambalo alisema atawatenda; asilitende.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 51:1-2, 10-11, 16-17

  1. Ee Mungu, unirehemu,
    Sawa na fadhili zako.
    Kiasi cha wingi wa rehema zako,
    Uyafute makosa yangu.
    (K) Moyo uliovunjika na kupondeka,
    Ee Mungu, hutaudharau.
  2. Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
    Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
    Usinitenge na uso wako,
    Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. (K)
  3. Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa,
    Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa.
    Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika,
    Moyo uliovunjika na kupondeka. (K)

INJILI: Lk 11: 29-32
Makutano walipokuwa wakimkusanyikia, Yesu alianza kusema, Kizazi hiki ni kizazi kibaya; kinatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya Yona. Maana, kama vile Yona alivyokuwa ishara kwa Waninawi, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu kwa kizazi hiki. Malkia wa Kusini ataondoka siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa na hatia; kwa sababu yeye alikuja kutoka nchi za dunia aisikie hekima ya Sulemani; na hapa pana mkubwa kuliko Sulemani. Watu wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na kizazi hiki, nao watakihukumu kuwa na hatia; kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona, na hapa pana mkubwa kuliko Yona.

TAFAKARI:
KUKUBALI MWALIKO WA KUFANYA TOBA KWA MATENDO: “Akavua vazi lake, akajivika nguo za magunia na kuketi katika majivu” (Yona 3:6). Yona analiongoza kundi kubwa la watu katika kufanya toba Mwanzoni kundi dogo la watu wanayashika kwa moyo mafundisho ya Yona na kuyafundisha kwa wengine wengi hadi kwa mfalme wa Ninawi (Yona 3:6) na mwishowe kwa watu wote wa Ninawi. Watu wa Ninawi kwa ujumla wao walikuwa wadhambi, na Yona anawaletea habari za toba na kumrudia Mungu. Ndiyo maana leo watu hao pamoja na mfalme wao, wana kubali kufanya toba hiyo. Wanavua mavazi yao na kuvaa magunia, hii ni alama ya kufanya toba, kujikatalia ya kale. Wanaketi katika majivu na kuonesha kweli kwamba wana huzuni kwa matendo yao na wanamuonesha Mungu huzuni hiyo kwa ishara ya nje. Kwaresma hii, tunaalikwa kuvua ya kale na kujikatalia mazoea yetu ya dunia hii, kwa huzuni kufanya toba ili kuunganika na Mungu.

SALA: Mungu, naomba Kwaresma hii izae matunda ndani yangu.