FEBRUARI 23, 2021; JUMANNE: JUMA LA 1 LA KWARESIMA

Mt. Polkarpo, Askofu na Shahidi
Kumbukumbu
Urujuani
Zaburi: Juma 3

SOMO 1: Isa 55: 10-11
Bwana asema: Kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko; bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza, ikampa mtu apandaye mbegu, na mtu alaye chakula; ndivyo litakavyokuwa neno langu, litokalo katika kinywa changu; halitanirudia bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 34:3-6, 15-18

 1. Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
  Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
  Nalimtafuta Bwana akanijibu,
  Akaniponya na hofu zangu zote.
  (K)Wenye haki, Bwana anawaponya
  na taabu zao zote.
 2. Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
  Wala nyuso zao hazitaona haya.
  Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
  Akamwokoa na taabu zake zote. (K)
 3. Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki,
  Na masikio yake hukielekea kilio chao.
  Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya,
  Aliondoa kumbukumbu lao duniani. (K)
 4. Walilia, naye Bwana akasikia,
  Akawaponya na taabu zao zote.
  Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo,
  Na waliopondeka roho huwaokoa. (K)

INJILI: Mt 6: 7-15
Siku ile Yesu aliwaambia wafuasi wake: Mkiwa katika kusali, msipayuke-payuke, kama watu wa mataifa; maana wao hudhani ya kuwa watasikiwa kwa sababu maneno yao kuwa mengi. Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnavyohitaji kabla ninyi hamjamwomba. Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni. Utupe leo riziki yetu. Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu. Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao, wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu.

TAFAKARI:
MASHINDANO YA KUSAMEHE KATIKA KWARESMA: Sala kuu ya Yesu aliyotufundisha yaani sala ya Baba yetu, inahusisha ombi la “msamaha”, na ahadi ya kusamehe. Baada ya hapo hufuatia onyo kutoka kwa Yesu kwamba hatutaweza kusamehewa kama hatuwasamehi wenzetu. Msamaha ambao Yesu anatufundisha, msisitizo wake ni kwamba, lazima utoke ndani ya moyo na siyo mdomoni tu. Kwa kuwa Yesu anatuonesha umuhimu wa msamaha katika maisha yetu, hatuna budi kuwa na mazoezi mbalimbali ya kiroho juu ya msamaha. Mafundisho yote ya Yesu lengo lake ni kutujengea sisi wanadamu maisha bora ya kiroho katika jamii zetu, na kuondoa mitafaruku ya kiroho kwa wanadamu Kusamehe huleta amani ya ndani, amani ya familia na amani ya jamii kwa ujumla. Kwaresma hii, tufanye mashindano ya kiroho, tushindane kusamehe, ili tutakapopata tuzo ya kusamehe, nasi tuweze kusamehewa. Tunaposamehewa na Mungu, tunajiweka pazuri kuirithi mbingu, aliko bingwa wa kusamehe, Mungu mwenyewe.

SALA: Baba, utusamehe makosa yetu, kama tunavyowasemahe wale waliotukosea.