FEBRUARI 22, 2021; JUMATATU: JUMA LA 1 LA KWARESIMA

UKULU WA PETRO, MTUME
Sikukuu
Nyeupe
Zaburi: Tazama sala ya siku

SOMO 1: 1 Pet 5:1-4
Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiyari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi. Na Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 23

 1. Bwana ndiye mchungaji wangu,
  Sitapungukiwa na kitu.
  Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,
  Kando ya maji ya utulivu huniongoza.
  (K)Bwana ndiye Mchugaji wangu, sitapungukiwa na kitu.
 2. Hunihuisha nafsi yangu, na kuniongoza,
  Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
  Naam nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti,
  Sitaogopa mabaya,
  Kwa maana wewe upo pamoja nami,
  Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. (K)
 3. Waandaa meza mbele yangu,
  Machoni pa watesi wangu.
  Umenipaka mafuta kichwani pangu,
  Na kikombe changu kinafurika. (K)
 4. Hakika wema na fadhili zitanifuata,
  Siku zote za maisha yangu,
  nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)

INJILI: Mt 16:13-19
Yesu alienda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa adamu kuwa ni nani? Wakasema, Wengine hunena u Yohane Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii. Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga Kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.

TAFAKARI:
HAKIKA YESU NDIYE KRISTO. Kanisa linaadhimisha sikukuu ya ukulu wa mtume Petro, kwa sababu kiti hicho ni alama ya uwezo wake wa kutawala na kuwaongoza waamini wote. Pia kinatukumbusha kuwa, mtume Petro na mahalifa wake, yaani maaskofu wa Kanisa Katoliki, wanawekwa mawakili wa Yesu Kristo hapa duniani. Kazi yao wote hawa, ni kuyalinda, kuyatetea na kuyafundisha mafundisho ya Yesu Kristo duniani kote. Petro ni mtume wa Yesu aliyepata misukosuko mingi katika ufuasi wake, lakini yote hayo kwake ilikuwa ni kumuimarisha zaidi katika ufuasi wa Yesu. Ndiyo maana katika uimara huo, leo anamtambua Yesu na kukiri wazi kwamba “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai” (Mt 16:16). Petro anatudhihirishia wazi kwamba, ni mfuasi na mtume wa Yesu aliyekomaa kiimani, bila kusita anatamka kuwa Yesu ndiye Kristo. Mimi kama Mkristo napaswa kumkiri Yesu kuwa ndiye Kristo, maisha yangu kwa ujumla, yaoneshe, kwamba, Kristo yumo ndani yangu.

SALA: Ee Mungu, nisaidie ili nimkiri Yesu kuwa ndiye Kristo.