Urujuani
Zaburi: Juma 3
SOMO I: Mwa 9:8-15
Mungu akamwambia Nuhu, na wanawe pamoja naye, akisema, Mimi, tazama, nalithibitisha agano langu nanyi, tena na uzao wenu baada yenu; tena na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi; ndege, na mnyama wa kufugwa, na kila mnyama wa mwitu katika nchi pamoja nanyi; wote wanaotoka katika safina, hata kila kilicho hai katika nchi. Na agano langu nitalithibitisha nanyi; wala kila chenye mwili hakitafutwa tena kwa maji ya gharika; wala hakutakuwa tena gharika, baada ya hayo, kuiharibu nchi. Mungu akasema, Hii ndiyo ishara ya agano nifanyalo kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi, kwa vizazi vyote hata milele; Mimi nauweka upinde wangu winguni, nao utakuwa ni ishara ya agano kati yangu na nchi. Hata itakuwa nikitanda mawingu juu ya nchi, upinde utaonekana winguni, nami nitalikumbuka agano langu, lililoko kati yangu na ninyi, na kila kiumbe hai katika wote wenye mwili, wala maji hayatakuwa gharika tena kuwaharibu wote wenye mwili.
WIMBO WA KATIKATI: Zab25:4-9
- Ee Bwana, unijulishe njia zako,
Unifundishe mapito yako,
Uniongoze katika kweli yako,
Na kunifundisha
Maana wewe ndiwe Mungu wa wokovu wangu.
(K) Njia zote za Bwana ni fadhili na kweli, Kwao walishikao agano lake na shuhuda zake. - Ee Bwana, kumbuka rehema zako na fadhili zako,
Maana zimekuwako tokea zamani.
Unikumbuke kwa kadiri ya fadhili zako,
Ee Bwana, kwa ajili ya wema wako. (K) - Bwana yu mwema, mwenye adili,
Kwa hiyo atawafundisha wenye dhambi njia.
Wenye upole atawaongoza katika hukumu,
Wenye upole atawafundisha njia yake.
SOMO 2: 1 Pet 3:18-22
Kristo aliteswa mara moja kwa ajili ya dhambi, mwenye haki kwa ajili yao wasio haki, ili atulete kwa Mungu; mwili wake akauawa, bali roho yake akahuishwa, ambayo kwa hiyo aliwaendea roho waliokaa kifungoni, akawahubiri; watu wasiotii hapo zamani, uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja, siku za Nuhu, safina ilipokuwa ikitengenezwa; ambamo ndani yake wachache, yaani, watu wanane, waliokoka kwa maji. Mfano wa mambo hayo ni ubatizo, unaowaokoa ninyi pia siku hizi; (siyo kuwekea mbali uchafu wa mwili, bali jibu la dhamiri safi mbele za Mungu), kwa kufufuka kwake Yesu Kristo. Naye yupo mkono wa kuume wa Mungu, amekwenda zake mbinguni, malaika na enzi na nguvu zikiisha kutiishwa chini yake.
SHANGILIO: Mt 4:4
Mtu hataishi kwa mkate tu,
Ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu
INJILI: Mk 1:12-15
Roho alimtoa Yesu aende nyikani. Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na Shetani; naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu, na malaika walikuwa wakimhudumia. Hata baada ya Yohane kutiwa gerezani, Yesu akaenda Galilaya, akiihubiri Habari Njema ya Mungu, akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili.
TAFAKARI:
TUMEOSHWA TUKATAKATA KWA MAJI: Somo la kwanza linatuambia kwamba Mungu hakatishwi tamaa na sura ya uovu. Anaingilia ili kujenga na kufanya tena upya. Anajenga ubinadamu mpya na kuahidi baraka na mambo mazuri, “Ninaanzisha agano jipya na ninyi, na kila mnyama …maisha hayataharibiwa tena kwa njia ya gharika” (Mwa 9:9-11). Huu ni ujumbe wa matuamiani na faraja kwamba Mungu hasubiri watu wawe wazuri ndio awe mkarimu kwao. Mungu anawabadilisha waweze kuwa viumbe vipya.
Katika somo la pili, Petro naye anatumia habari ya maji ya gharika ya kipindi cha Nuhu kuelezea habari za ubatizo. Nuhu aliokolewa na safina ambayo Mungu alimuagiza aitengeneze; yeye na familia yake pamoja na baadhi ya wanyama waliokolewa. Kwa njia ya Nuhu, uumbaji mpya ulitokea. Maji ya ubatizo ni yenye nguvu ya uumbaji; huharibu na kuangamiza hali ya zamani na kumfanya mwanadamu kuwa mpya na kumpatia roho mpya (Rum 6:3-5).
Injili inatupatia habari za Yesu kukaa jangwani akifunga kwa muda wa siku arobaini, akijaribiwa na Shetani. Lugha inayotumika katika Injili yetu ni ya picha; ina maana kwamba maisha yote ya Yesu yalikuwa ya kupigana kati yake na yule mshawishi. Hali ya namna hii hutupata na sisi sote tunaomfuataYesu. Daima tupo katika mapambano kati ya wema na uovu; muovu anajaribu kutuvuta kwake daima ili tuache njia iliyo nzuri. Yesu alimshinda Shetani na malaika kufika na kumhudumia. Malaika waliomhudumia tunaweza kuwafananisha na wazazi wake, watu waliomsaidia katika utume wake, wale wote walioshiriki katika maisha yake na kuyafuata yale aliyowaambia na kushiriki naye katika kazi ya wokovu.
Vishawishi vipo. Ni matokeo ya maanguko ya wanadamu wa kwanza. Vishawishi huanzia katika udhaifu wetu lakini pia hutoka katika yule mwovu (Yak 1:13-15). Yesu hakukubali kuangushwa na vishawishi alivyokumbana navyo jangwani; pia hakuanguka katika kishawishi katika maisha yake yote. Hili linatuambia kwamba anaweza kuwa kiongozi wetu na mfano wa kuiga pale tukutanapo na vishawishi.
Wakati mwingine tunaweza kujisikia wapweke, tuliotengwa katika jangwa la dhambi zetu. Tunaweza kujisikia kana kwamba yule mwovu anatunyemelea. Yesu alipatwa na haya pia. Aliruhusu kupitia haya kwa kushiriki ubinadamu wetu. Kwa njia hii, Yesu anaweza kukutana nasi katika jangwa letu. Yupo tayari anatusubiri, akitutafuta, akituita sisi. Ni huyu aliyeshinda vishawishi vya muovu jangwani, ndiye atakayetuongoza kuviepuka. Kwa hiyo, kama jangwa lako ni mahangaiko ya maisha sasa, au ni majaribu mbalimbali, Yesu anataka kukutana nawe akuongoze katika njia iliyo njema. Alimshinda yule mwovu jangwani, hivyo anao uwezo wa kushinda jangwa lolote lile katika maisha yako (P. Mosha, The Dragon and the Beasts, 58-59).
Kwaresima ni kipindi cha kuamua kujinasua katika dhambi. Yesu anasema katika Injili ya leo, “Huu ndio wakati mtimilifu. Ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Injili.” Kama tunataka ubatizo wetu ulete maana na kutusaidia, ni lazima tuyaweke maneno ya Yesu katika maisha yetu. Jipatanishe na mwingine ambaye mmekosana naye. Jitahidi katika sala na kujiunga na Mungu. Fanya mabadiliko sahihi na anza vita kati yako na dhambi, hasa dhambi unayoirudia rudia sana. Amua kutoka moyoni, pambana nayo na hakikisha unaachana nayo. Kuwa tayari kusimama katika tunu za Kristo hata pale ambapo kuna vishawishi vingi katika maisha.
Epuka sehemu ambazo wewe mwenyewe ukikaa unajua kabisa zinakupeleka kwenye dhambi. Kwepa marafiki wabaya wanaokupeleka kwenye dhambi. Onesha kwamba imani yako inaambatana na matendo yako. Hata kama utatengwa na kuitwa mbaya, hakika haupo mwenyewe; upo na Yesu. Epuka vishawishi. Ashindaye mpaka mwisho kama Yesu alivyoshinda daima hupokea taji (Uf 2:10). Tumuombe Mungu atusimamie.
SALA: Ee Bwana, ninakubali upendo wako mkamilifu kwangu. Nina amini kwamba unanipenda mimi kiasi kwamba nitaweza kuelewa na kuvumilia mateso yote. Ninakuomba nikutane nawe katika jangwa la maisha yangu. Ninakuomba nikuruhusu wewe uniongoze.