FEBRUARI 20, 2021; JUMAMOSI BAADA YA MAJIVU

Urujuani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Isa 58: 9b-14
Bwana asema hivi: Kama ukiiondoa nira; isiwapo kati yako, wala kunyoosha kidole, wala kunenea maovu; na kama ukimkunjulia mtu mwenye njaa nafsi yako, na kuishibisha nafsi iliyoteswa; ndipo nuru yako itakapopambazuka gizani; na kiwi chako kitakuwa kama adhuhuri. Naye Bwana atakuongoza daima, ataishibisha nafsi yako mahali pasipokuwa na maji, na kuitia nguvu mifupa yako; nawe utakuwa kama bustani iliyotiwa maji, na kama chemchemi ambayo maji yake hayapungui. Na watu wako watapajenga mahali palipokuwa ukiwa; utaiinua misingi ya vizazi vingi; nawe utaitwa; Mwenye kutengeneza mahali palipobomoka; na, Mwenye kurejeza njia za kukalia. Kama ukigeuza mguu wako usiiharifu Sabato, usifanye anasa yako siku ya utakatifu wangu; ukiita Sabato siku ya furaha, na siku takatifu ya Bwana yenye heshima; ukiitukuza, kwa kutokuzifanya njia zako mwenyewe, wala kuyatafuta yakupendezayo, wala kusema maneno yako mwenyewe; ndipo utakapojifurahisha katika Bwana; nami nitakupandisha mahali pa nchi palipoinuka; nitakulisha urithi wa Yakobo baba yako; kwa maana kinywa cha Bwana kimenena hayo.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 86:1-2, 3-4, 5-6

 1. Ee Bwana, utege sikio lako unijibu,
  Maana mimi ni maskini na mhitaji,
  Unihifadhi nafsi yangu,
  Maana mimi ni mcha Mungu.
  Wewe uliye Mungu wangu,
  Umwokoe mtumishi wako anayekutumaini.
  (K) Ee Bwana, unifundishe njia yako;
  Nitakwenda katika kweli yako.
 2. Wewe, Bwana unifadhili,
  Maana nakulilia Wewe mchana kutwa.
  Uifurahishe nafsi ya mtumishi wako,
  Maana nafsi yangu nakuinulia Wewe Bwana. (K)
 3. Kwa maana Wewe, Bwana, U mwema,
  Umekuwa tayari kusamehe,
  Na mwingi wa fadhili,
  Kwa watu wote wakuitao.
  Ee Bwana, uyasikie maombi yangu;
  Uisikilize sauti ya dua zangu. (K)

INJILI: Lk 5:27-32
Siku ile: Yesu aliona mtoza ushuru, jina lake Lawi, ameketi forodhani, akamwambia Nifuate. Akaacha, vyote, akaondoka, akamfuata. Na Lawi akamfanyia karamu kubwa nyumbani mwake; palikuwa na mkutano mkuu wa watoza ushuru na watu wengineo waliokuwa wameketi chakulani pamoja nao. Ikawa Mafarisayo na waandishi wao kuwanung’unikia wanafunzi wake, wakisema, mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Yesu akajibu akawaambia, wenye afya hawana haja na tabibu, isipokuwa walio hawawezi. Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi wapate kutubu.

TAFAKARI:
JINSI YA KUFUNGA KWARESMA: “Siku ile: Yesu aliona mtoza ushuru, jina lake Lawi, ameketi forodhani, akamwambia Nifuate. Akaacha, vyote, akaondoka, akamfuata” (Lk 5:27-28). Mfungo wetu wa Kwaresma unatumiwa na Yesu kumbadilisha Lawi na kuwa Matayo na kuongoa jamii yote, na hata wenye roho ngumu watafunuliwa na kuwa kweli wafuasi wa Yesu. Ni ukweli usio shaka kwamba Yesu anaweza kutenda kipindi hiki cha Kwaresma, kuwafanya watu wakubali wongofu na kukubaliwa na Mungu kama Isaya anavyosisitiza tuwapokee wenye njaa na kuwalisha, kuisaidia nafsi inayoteswa (Isa 58:10.). Kipindi hiki Yesu anataka tuisikie na tuikubali sauti yake, “Nifuate!” kama alivyomwambia Lawi. Maisha yetu ni lazima yabadilike kabisa na kujishusha kabisa kwa Yesu kwa matendo yetu mema kama wafuasi wa kweli wa Yesu. Kama kweli tunaishi maisha ya Kwaresma, tunapaswa kujitafutia majibu ya maswali haya, “Ninajishusha kabisa kwa Yesu?” “Ninamkubali Yesu kama Bwana wa maisha yangu na kila nilichonacho?”

SALA: Baba, nifundishe matendo mema ya mfungo wa Kwaresma.