Urujuani
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: Isa 58: 1-9
Bwana Mungu asema hivi: Piga kelele, usiache, paza sauti yako kama tarumbeta; uwahubiri watu wangu kosa lao, na nyumba ya Yakobo dhambi zao. Walakini wanitafuta kila siku; hupenda kujua njia zangu; kama vile taifa waliotenda haki, wasioacha sheria ya Mungu wao, hutaka kwangu amri za haki; hufurahi kumkaribia Mungu. Husema, mbona tumefunga, lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu, lakini huangalii? Fahamuni, siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu. Tazama, ninyi mwafunga mpate kushindana na kugombana, nakupiga kwa ngumi ya uovu. Hamfungi siku hii ya leo hata kuisikizisha sauti yenu juu. Je! kufunga namna hii ni saumu niliyoichagua mimi? Je! Si siku ya mtu kujitaabisha nafsi yake? Ni kuinama kichwa kama unyasi, na kutanda nguo za magunia na majivu chini yake? Je! Utasema ni siku ya kufunga, na ya kukubaliwa na Bwana. Je! saumu niliyoichagua, siyo ya namna hii? Kufungua vifungo vya uovu, kuzilegeza kamba za nira, kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira? Je! Siyo kuwagawia wenye njaa chakula chako, na kuwaleta maskini waliotupwa nje nyumbani kwako? Umwonapo mtu aliye uchi, umvike nguo; wala usijifiche na mtu mwenye damu moja nawe? Ndipo nuru yako itakapopambazuka kama asubuhi, na afya yako itatokea mara; na haki yako itakutangulia; utukufu wa Bwana utakufuata nyuma ukulinde. Ndipo utaita na bwana ataitika; utalia, naye atasema, Mimi hapa.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 51:3-6a, 18-19
- Maana nimejua mimi makosa yangu,
Na dhambi yangu i mbele yangu daima.
Nimekutenda dhambi Wewe peke yako,
Na kufanya maovu mbele za macho yako.
(K) Moyo uliovunjika na kupondeka,
Ee Mungu, hutadharau. - Tazama mimi naliumbwa katika hali ya uovu;
Mama yangu alinichukua mimba hatiani.
Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni
Nawe utanijulisha hekima kwa siri. (K) - Uitendee mema Sayuni kwa radhi yako,
Uzijenge kuta za Yerusalemu.
Ndipo utakapopendezwa na dhabihu za haki;
Na sadaka za kuteketezwa, na kafara. (K)
INJILI: Mt 9: 14-15
Siku ile: Yesu alipofika ng’ambo, katika nchi ya Wagerasi, wanafunzi wake Yohane wakamwendea, wakasema, Kwa nini sisi na Mafarisayo twafunga, bali wanafunzi wako hawafungi? Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga.
TAFAKARI:
KUFUNGA KUNA FAIDA: “Husema, mbona tumefunga, lakini huoni? Mbona tumejitaabisha nafsi zetu, lakini huangalii? Fahamuni, siku ya kufunga kwenu mnatafuta anasa zenu wenyewe, na kuwalemea wote watendao kazi kwenu”(Isaya 58:4). Mfungo wa Kwaresma ni kumfuata Kristo na kumuiga kwani hata yeye alifunga tena kwa siku arobaini, ikiwa ni maandalizi ya kuanza utume wake hadharani (Mt 4:2). Wapendwa, wapo watu wasiothamini kufunga, na wanaendekeza malimwengu zaidi, lakini Yesu anatuhakikishia kwamba, kwa kufunga, Baba yetu aonaye sirini, atatujazi (Mt 6:18). Ni kwa kusali na kufunga, tunapata nguvu za kuwafukuza pepo wabaya (Mt17:21). Kumbe mfungo huu una maana kubwa sana kwetu kama tukifunga vizuri na kufuata tabia ya mfungo ya kusali bila kuchoka, kufanya maungamo mara kwa mara, kujinyima kwa ajili ya maskini na kuwafikia wagonjwa. Maisha yetu yaunganike na Yesu kiongozi wetu aliyefunga kujiimarisha kwa kazi ya uinjilishaji. Mfungo mwema mwisho wake ni Pasaka njema kiroho.
SALA: Baba, mfungo wa Kwaresma mwaka huu unijalie neema zako.