Urujuani
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: Kum 30: 15-20
Musa aliwaambia watu akisema: Angalia, nimekuwekea leo mbele yako uzima na mema, na mauti na mabaya; kwa hivi nikuagizavyo leo kumpenda Bwana, Mungu wako, kuenenda katika njia zake, na kushika maagizo yake, na amri zake, na hukumu zake, upate kuwa hai na kuongezeka; Bwana, Mungu wako, apate kukubarikia katika nchi uingiayo kuimiliki. Lakini moyo wako ukikengeuka, usipotaka kusikiza, lakini ukavutwa kando kwenda kuabudu miungu mingine, na kuitumikia; nawahubiri hivi leo hakika mtaangamia, hamtazifanya siku zenu kuwa nyingi juu ya nchi, uivukiayo Yordani, uingie kuimiliki. Nazishuhudiza mbingu na nchi juu yenu hivi leo, kuwa nimekuwekea mbele yako uzima na mauti baraka na laana; basi chagua uzima, ili uwe hai, wewe na uzao wako; kupenda Bwana, Mungu wako, kuitii sauti yake, na kushikamana naye; kwani hiyo ndiyo uzima wako, na wingi wa siku zako; upate kukaa katika nchi Bwana aliyowaapia baba zako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kuwa atawapa.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 1:1-4,6
- Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki;
Wala hakusimama katika njia ya wakosaji;
Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha.
Bali sheria ya Bwana ndiyo impendezayo,
Na sheria yake huitafakari mchana na usiku.
(K) Heri mtu aliyemfanya Bwana kuwa tumaini lake. - Naye atakuwa kama mti uliopandwa
Kandokando ya vijito vya maji,
Uzaao matunda yake kwa majira yake,
Wala jani lake halinyauki;
Na kila alitendalo litafanikiwa. (K) - Sivyo walivyo wasio haki;
Hao ni kama makapi yapeperushayo na upepo.
Kwa kuwa Bwana anaijua njia ya wenye haki,
Bali njia ya wasio haki itapotea. (K)
INJILI: Lk 9: 22-25
Siku ile: Yesu aliwaambia wafuasi wake kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi, na kukataliwa na wazee na wakuu wa makuhani na waandishi, na kuuawa na siku ya tatu kufufuka. Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha. Kwa kuwa yamfaa nini mtu kuupata ulimwengu wote, kama akijiangamiza, au kujipoteza mwenyewe?
TAFAKARI:
FURAHA YA KUJINYIMA: Kristo anatuambia, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe” (Lk 9:23). Kumfuata Yesu, hatuna budi kujikana kila wakati. Kipindi chote cha Kwaresma ni cha kujikana na si Kwaresma tu bali maisha yetu yote. Walimwengu kwa starehe zao hupenda raha, ambayo ni ya muda na haileti furaha, kwani furaha ya kweli hutoka kwa Mungu tu. Furaha hiyo ya kweli huja tu pale tutakapojikana na kuibeba misalaba yetu na kumfuata Yesu bila kuchoka. Matendo ya kuwasaidia maskini, kutoa zaka, moyo wa ibada ya kweli, kusalimia wagonjwa na walio kifungoni, kuwalisha wenye njaa na kuwanywesha wenye kiu (Mt 25:35-36), ndiyo yatakayotupatia furaha ya kweli. Mara kadhaa tunasahau kufanya ukarimu kwa watu na kutenda kama wale tusiomjua Mungu, na wakati mwingine tunatenda vibaya hata zaidi ya wasiomjua Mungu. Tubadilike ili kujiwekea nafasi ya furaha ya milele. Tufurahie kujinyima ili kupata furaha ya kweli.
SALA: Bwana, nijalie kujinyima ili nipate furaha ya kudumu.