Kijani
Zaburi: Juma 2
SOMO 1: Mwa 6:5 – 8, 7:1-5, 10
Bwana akaona ya kuwa maovu ya mwanadamu ni makubwa duniani na kwamba kila kusudi analowaza moyoni mwake ni baya tu siku zote. Bwana akaghairi kwa kuwa amemfanya mwanadamu duniani, akahuzunika moyo. Bwana akasema, Nitamfutilia mbali mwanadamu niliyemwumba usoni pa nchi; mwanadamu na mnyama, na kitambaacho na ndege wa angani kwa maana nagairi ya kwamba nimewafanya. Lakini Nuhu akapata neema machoni pa Bwana. Bwana akamwambia Nuhu, ingia wewe na jamaa yako yote katika safina; kwa maana nimekuona wewe u mwenye haki mbele zangu katika kizazi hiki. Katika wanyama wote walio safi ujitwalie saba saba, mume na mke; na katika wanyama wasio safi wawili wawili, mume na mke; tena katika ndege wa angani saba saba,mume na mke; ili kuhifadhi hai mbegu juu ya uso wa nchi yote. Kwa maana baada ya siku saba nitainyeshea dunia mvua, siku arobaini mchana na usiku; na kila kilichohai nilichokifanya juu ya uso wa nchi nitakifutilia mbali. Nuhu akafanya kama vile Bwana
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 29:1-4,9-10
- Mpeni Bwana, enyi wana wa Mungu,
Mpeni Bwana utukufu wa jina lake,
Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu.
(K) Bwana atawabariki watu wake kwa amani. - Sauti ya Bwana i juu ya maji,
Bwana yu juu ya maji mengi.
Sauti ya Bwana ina nguvu,
Sauti ya Bwana ina adhama. (K) - Sauti ya Bwana wayazalisha ayala,
Na ndani ya hekalu lake wanasema wote: Utukufu.
Bwana ameketi juu ya gharika,
Naam, Bwana ameketi hali ya mfalme milele. (K)
INJILI: Mk 8:14-21
Wafuasi wake Yesu walisahau kuchukua mikate, wala chomboni hawana ila mkate mmoja tu. Akawaagiza, akasema, Angalieni, jihadharini na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode. Wakabishana wao kwa wao, kwa kuwa hawana mikate. Naye Yesu akatambua, akawaambia, Mbona mnabishana kwa sababu hamna mikate? Hamfahamu bado, wala hamjaelewa? Je! Mioyo yenu ni mizito? Mna macho, hamwoni; mna masikio, hamsikii? Wala hamkumbuki? Nilipoivunja ile mikate mitano na kuwapa wale elfu tano, mlichukua vikapu vingapi vimejaa vipande? Wakamwambia, Kumi na viwili. Na ile saba kuwapa wale elfu nne, mlichukua makanda mangapi yamejaa vipande? Wakamwambia, Saba. Akawaambia, Hamjafahamu bado?
TAFAKARI:
MOYO WA MUNGU WENYE HUZUNI: Moyo wa mwanadamu ulijaa maovu mengi sana wakati wa Nuhu. Hakuna aliyetamani mema ila uovu tu. Hali hii ya uovu, ilimvunja moyo Mungu na akawa na huzuni sana dhidi ya mwanadamu aliyemuumba, na kuamua kumfutilia mbali kutoka duniani ((Mwa 6:7). Mungu “anamkatia tamaa” mwanadamu sababu ya kutoyafuata maelekezo yake. Waliishi katika anasa za ajabu, rushwa, magomvi na chuki. Hatima yake waliadhibiwa na Mungu kwa kufyekelewa mbali kwa gharika ya maji, kasoro Nuhu na uzao wake na wanyama, ndege na wadudu jinsi Mungu alivyopendezwa. Maovu ndiyo yaliyomponza mwanadamu, lakini bado hata katika ulimwengu wetu huu, bado watu hawajifunzi kutoka kwenye gharika hii, bado maovu yapo duniani tena kwa wingi kiasi cha kumsononesha Mungu. Tunasikia habari za vita na mauaji, utoaji mimba, habari za ushoga, chuki na machukizo kwa wanadamu hata bila kumuogopa Mungu. Tumrudie Mungu ili atuongoze katika njia zake.
SALA: Yesu mpole na mnyenyekevu, ufanye moyo wangu ufanane na moyo wako.