FEBRUARI 15, 2021; JUMATATU: JUMA LA 6 LA MWAKA

Kijani
Zaburi: Juma 2

SOMO 1: Mwa 4:1 – 15, 25
Adamu alimjua Hawa mkewe; naye akapata mimba akamzaa Kaini, akasema, nimepata mtoto mwanamume kwa Bwana. Akaongeza akamzaa ndugu yake, Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo, na Kaini alikuwa mkulima ardhi. Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa Bwana. Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizo nona za wanyama. Bwana akamtakabali Habili na sadaka yake. Bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana. Bwana akamwambia Kaini, kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana? Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde. Kaini akamwambia Habili nduguye, twende uwandani. Ikawa walipokuwapo uwandani, Kaini akamwinukia Habili nduguye akamwua. Bwana akamwambia Kaini, yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? Akasema, umefanya nini? Sauti ya damu ya ndugu yako inanililia kutoka katika ardhi. Basi sasa, umelaaniwa wewe katika ardhi, iliyofumbua kinywa chake ipokee damu ya ndugu yako kwa mkono wako; utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani. Kaini akamwambia Bwana, adhabu yangu imenikulia kubwa, haichukuliki. Tazama, umenifukuza leo katika uso wa ardhi, nitasitirika mbali na uso wako, nami nitakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani; hata itakuwa kila anionaye ataniua. Bwana akamwambia, kwa sababbu hiyo ye yote atakaye muua Kaini atalipizwa kisasi mara saba. Bwana akamtia Kaini alama, mtu amwonaye asije akampiga. Adamu akamjua mke wake tena; akazaa mwana mwanamume, akamwita jina lake Sethi; maana alisema, Mungu ameniwekea uzao mwingine mahali pa Habili; kwa sababu Kaini alimwua.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 50: 1, 8, 16-17, 20-21

 1. Mungu, Mungu Bwana, amenena, ameiita nchi,
  Toka maawio ya jua hata machweo yake.
  Sitakukemea kwa ajili ya dhabihu zako,
  Na kafara zako ziko mbele zangu daima.
  (K) Umtolee Mungu dhabihu za kushukuru.
 2. Bali mtu asiye haki, Mungu amwambia,
  Una nini wewe kuitangaza sheria yangu,
  Na kuliweka agano langu kinywani mwako?
  Maana wewe umechukia maonyo,
  Na kuyatupa maneno yangu nyuma yako. (K)
 3. Umekaa na kumsengenya ndugu yako
  Na mwana wa mama yako umemsingizia.
  Ndivyo ulivyofanya, nami nikanyamaza,
  Ukadhani ya kuwa Mimi ni kama wewe.
  Walakini nitakukemea;
  Nitayapanga hayo mbele ya macho yako. (K)

INJILI: Mk 8:11-13
Walitokea Mafarisayo, wakaanza kuhojiana na Yesu; wakitafuta kwake ishara itokayo mbinguni; wakimjaribu. Akaugua rohoni mwake, akasema, Mbona kizazi hiki chatafuta ishara? Amin, nawaambieni, Hakitapewa ishara kizazi hiki. Akawaacha akapanda tena chomboni, akaenda zake hata ng’ambo.

TAFAKARI:
ZAWADI YA IMANI: Inashangaza kusoma katika Injili kwamba Mafarisayo wanasubiri ishara toka mbinguni kuthibitisha ufalme wa Mungu. Kuna ishara na miujiza mingi imeandikwa kwenye Biblia aliyofanya Kristo, ambayo huthibitisha kwamba, ametoka kwa Mungu. Kwa Mafarisayo, miujiza hii haitoshi. Wanaonesha uhaba, imani yao inajikita kwenye mafundisho ya Kiyahudi kwamba Masiha atakapokuja, atafanya miujiza ya pekee ambayo itawaridhisha watu wote wakiwamo Mafarisayo. Mafarisayo wanaonesha kutokuwa wazi mbele ya Kristo mbali ya kumuuliza maswali ya kumjaribu. Imani inahitaji uwazi na ukweli, ikiwa ni pamoja matarajio ya kukubali sababu za kawaida za kuamini. Kwa kuponya ugonjwa, kutoa pepo, kuwalisha watu na miujiza mingine ya kimungu hazitoshi kuwashawishi Mafarisayo, ni wazi watabaki daima bila imani. Wewe je, una imani kwa miujiza ya Kristo na kwamba ina nguvu za kimungu? Lazima tuondoe shaka na kubaki ndani ya Kristo, ambaye hatujamuona kwa macho yetu bali kupitia matendo na miujiza yake.

SALA: Mungu wangu, niongoze katika njia ya imani.